SIYRAH YA MTUME MUHAMMAD S.A.W
SIYRAH YA MTUME MUHAMMAD S.A.W
KUZALIWA KWA MTUME
Bwana Mtume – Allah amshushie rehma na amani – alizaliwa katika mji wa Makkah, siku ya Jumatatu mwezi wa mfungo sita, mwaka wa tembo sawa na tarehe 20 ya mwezi April mwaka 571 – Miyladia (tangu kuzaliwa Nabii Issa).
Bwana Mtume alizaliwa hali ya kuwa ni yatima kwani baba yake alikufa akimuacha mkewe ana mimba ya Mtume. Mama yake alipojifungua tu alimpeleka mjumbe kwa babu yake Mtume Mzee Abdul -Mutwalib kumpa khabari njema za kuzaliwa mjukuu wake. Mzee Abdul – Mutwalib akafurahikia sana mjukuu wake akamchukua na kumzungusha katika Al-Kaaba na akamuita Muhammad.
Tumesema Bwana Mtume amezaliwa mwaka wa tembo. Qur-ani Tukufu imeuzungumza mwaka huu katika sura maalum iliyoitwa kwa jina la Suuratul –Fiyl (Sura ya tembo).
Kisa cha mwaka wa tembo kinaanzia pale Abraha mfalme wa Habashah na Yaman alipowaona Waarabu wakihiji Makkah na ibada hii ya Hijjah ikaufanya mji wa Makkah kuwa ni kitovu cha biashara . Mfalme Abraha akadhamiria kuihamisha ibada hii ya Hijjah kutoka Makkah na kuipeleka katika milki ya himaya yake ya Yaman.
Ili kuutekeleza mkakati wake huu akajenga kanisa kubwa sana na kulipamba kwa mapambo ya fakhari ili watu wavutike na kuja kufanya ibada ya Hijjah hapo. Baada ya ujenzi huo, akawaamrisha watu waje kuhiji hapo, amri hii ikawa nzito kwa Waarabu kuitekeleza na hawakuiridhia.
Ili kuonyesha chuki yao dhidi ya amri hii alitoka mtu mmoja wa kabila ya kinaanah akaja kufanya haja kubwa ndani ya kanisa lile. Kitendo hiki cha kulichafua kanisa kilimkasirisha sana Mfalme Abraha, hasa baada ya kugundua kwamba mhusika wa kitendo hicho ni mtu kutokea pande za Makkah.
Akaandaa jeshi kubwa lililokuwa limesheheni tembo wengi ili kwenda kuivunja Al-kaaba na yeye mwenyewe alikuwa amempanda tembo mkubwa sana kuliko wote.
Waarabu wa Makkah waliogofya sana na jeshi lile. Jeshi la Abraha lilipofika katika viunga vya mji wa Makkah likawakuta ngamia, kondoo na mbuzi wa watu wa Makkah na wengine walikuwa ni milki ya babu yake Mtume Mzee Abdul-Mutwalib, Abraha awachukua wanyama wale wote. Mzee Abdul-Mutwalib kiongozi wa kabila la Kikurayshi, mtumishi wa Al-Kaab na mtawala wa Makkah akamuendea Abraha na kumtaka amrejeshee wanyama wake aliowachukua Abraha akamshangaa sana Mzee Abdul – Mutwalib akamwambia:
"Mimi nilitazamia umekuja kuniomba nisiivunje Al-Kaab, kumbe umekuja kunitaka nikurudishie wanyama wako!" Mzee Abdul – Mutwalib akamjibu:
"Mimi wa kwangu ni hawa wanyama, ama hii nyumba yupo mwenyewe atayeihami".
Kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu alishushia jeshi la Abraha jeshi la ndege wanaolidondoshea jeshi la Abraha mawe kutoka motoni.
Jiwe likimpata mtu anasagikasagika yeye na tembo wake na kuwa kama majani yaliyoliwa na wadudu kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani.
Tokea hapo Waarabu wakawa wanaitaja kalenda yao kwakuinasibisha na tukio hili kubwa na hii ndio maana tunasema Bwana Mtume alizaliwa mwaka wa tembo.
KUNYONYESHWA KWA MTUME
Bwana Mtume- Allah amshushie Rehema na Amani- mara baada ya kuzaliwa alinyonyeshwa na mama yake Bi Amina Bint Wahab kwa siku kadhaa.
Kisha akanyonyeshwa na Bibi Thuwaybatul Aslamiyyah ambaye alikuwa ni mjakazi wa wa Ammi yake Mtume Abuu Lahab.
Baada ya hapo ndipo waliamua kumtafutia mlezi na mnyonyeshaji kama ilivyokuwa ada na desturi ya Waarabu wakati huo.
Wakampata Bibi Haliymah Assaadiyyah, Bibi huyu alimchukua Bwana Mtume na kwenda kuishi naye katika kitongoji cha Baniy Saad kwa muda wa miaka miwili akimnyonyesha.
Akamuachisha ziwa baada ya miaka miwili, na hili liliashiria kuisha kwa mkataba na kulazimika kumrudisha mtoto kwa mama yake.
Kutokana na jinsi mama huyu mlezi alivyompenda mwanawe huyu wa kumlea kwa sababu ya baraka walizozipata tangu kuanza kumlea mtoto huyu alimsihi sana mama yake Mtume amruhusu aendelee kuishi na kumlea mtoto huyu mwenye baraka.
Kitongoji cha Baniy Saad kilikuwa ni ardhi iliyo na upungufu mkubwa wa mvua, lakini mara tu baada ya kufika Bwana Mtume katika kitongoji kile, hali ilibadilika kabisa, ukame ukatoweka, ardhi ikaotesha mimea, mazao yakakithiri, wanyama wakapata malisho mengi na hivyo kutoa maziwa ya kutosha.
Hali na afya za watu wa kitongoji kile zikaboreka kutokana na baraka za mtoto huyu yatima. Kwa kuyazingatia yote haya mama yake Mtume alimkubalia Bibi Haliymah aendelee kumlea Mtume kwa kipindi kingine cha miaka miwili.
Ada na desturi hii ya waarabu kuwapeleka watoto kulelewa mashambani ilijengeka juu ya sababu mbili kuu :
MOSI Mashambani ndiko kuna mazingira safi yaliyosheheni hewa safi yenye afya. Kutokana na hewa hii safi na chakula freshi watoto huwa na afya njema.
PILI Wakazi wa mashambani ndio waliokuwa wakizungumza lugha fasaha. Hivyo mtoto alipata fursa ya kujifunza na hatimaye kuzungumza lugha fasaha.
Bibi Haliymah alikuwa akiishi na mumewe Bwana Abuu Kabshah. Bibi huyu anasimulia ukuaji na tabia za mtoto huyu wa ajabu, anasema :
"Mtoto huyu alikuwa akikuwa haraka haraka kuliko kawaida ya watoto, alikuwa akizungumza maneno fasaha ilhali yungali mtoto bado, kila aliyemuona alimpenda na kuvutiwa naye. Alikuwa halii na kupiga makelele kama wafanyavyo watoto wengine ila akiachwa bila ya nguo. Akipatwa na mshtuko ghafla wakati wa usiku nilikuwa nikitoka naye nje ya nyumba, naye huziangalia nyota mbinguni kwa muda mrefu mpaka akalala". Haya ni machache tu miongoni mwa mengi aliyoyaeleza Bibi Haliymah juu ya mtoto huyu yatima.
TUKIO CHA KUPASULIWA KIFUA
Katika kipindi hiki ambacho Bwana Mtume alikuwa chini ya ulezi na uangalizi wa Bibi Haliymah alitokewa na tukio muhimu sana.
Hili lilikuwa ni tukio la kupasuliwa kifua chake na kutolewa fungu/uchafu wa shetani ili shetani asiwe na nafasi ya kumlaghai, kumshawishi na hatimaye kumpotosha.
Tukio hili lilikuwa kama ifuatavyo :
Mwenyezi Mungu alimpelekea Mtume wake wake naye akingali mtoto malaika wawili.
Wakati huo Mtume alikuwa akichunga mbuzi na kondoo pamoja na nduguze wa kunyonya (Watoto wa Bi Haliymah) jirani na makazi yao.
Malaika wale wakambeba Mtume wakamlaza chali na kumpasua kifua chake, wakautoa moyo wake na kuukosha.
Baada ya kuukosha wakaurudisha mahala pake na pale pale kifua kikawa kama kilivyokuwa mwanzo bila ya athari yeyote.
Yote haya yalitendeka mbele ya macho ya watoto wenzake, wakakimbia haraka kwenda kumueleza mama yao yaliyompata ndugu yao huyu.
Bibi Haliymah na mumewe wakatoka mbio kwenda kuangalia kulikoni, wakamkuta Mtume amesimama, wakamkumbatia na kumuuliza yaliyomsibu naye akawahadithia tukio zima lilivyojiri.
Wakamshukuru MwenyeziMungu kwa kumsalimisha salama lakini wakachelea yasije kumpata tena kama haya yaliyompata leo, hivyo wakaamua kumrudisha kwa mama yake......
SIYRAH NZIMA INAPATIKANA KATIKA APP YA SIRAH YA MTUME MUHAMMAD kupitia Google Playstore

Comments
Post a Comment