SIRA YA NABII YUNUS

SIRA YA NABII YUNUS


Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemtaja Yunus kuwa ni katika Mitume na katika watu wema. Vile vile amemwita kwa jina sahiba wa samaki. Pia akamwita mwenye kughadhibika. Kwa sababu aliwalingania watu wake kwenye imani, lakini hawakumwitikia ndipo akawaombea maangamizo na akawaondokea kwa kukata tamaa na imani yao.

Katika Sura Al-Qalam Mwenyezi Mungu amemwamrisha Mtume wake Muhammad (s.a.w.), avumilie na asifanye haraka ya kuwaombea adhabu watu wake, kama alivyofanya Yunus.

فَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ وَلَا تَكُنْ كَصَاحِبِ الْحُوتِ إِذْ نَادَىٰ وَهُوَ مَكْظُومٌ {48}

“Basi subiri hukumu ya Mola wako, wala usiwe kama sahiba wa samaki, aliponadi na hali amezongwa.” (68:48).

Watu wa Yunus walikuwa kiasi cha laki moja (100,000). Mwenyezi Mungu anasema:

وَأَرْسَلْنَاهُ إِلَىٰ مِائَةِ أَلْفٍ أَوْ يَزِيدُونَ {147}

“Na tulimtua kwa watu elfu mia moja au zaidi.” (37:147).

Wapokezi na wafasiri wanasema kuwa watu wa Yunus walikuwa wakikaa katika ardhi ya Mousel, na kwamba wao walikuwa wakiabudu masanamu. Nabii Yunus (a.s.) akawakataza kufru hiyo na kuwaamrisha Tawhid, lakini wakang’ang’ania ushirikina wao; kama ilivyokuwa kwa watu wa Mitume wengine.

 Allaah Mtukufu alimtuma Nabii Yunus (Alayhis salaam) ili awahubirie watu wake katika kumwamini Allaah pekee na kumwabudu Yeye Aliyetukuka. Lakini watu wa mji wa Ninawaa walikataa kumwamini Allaah mmoja na wakaendelea kuishi katika giza la ushirikina na ukafiri. Wakati Nabii wa Allaah, Yunus (Alayhis salaam), alipokata tamaa aliondoka katika mji wa Ninawaa na akawaahidi wakazi wake adhabu ya Allaah itakayowashukia baada ya siku tatu. 

Toba ya watu wa Nabii Yunus Nabii Yunus (Alayhis salaam) hakusubiri kupata maelekezo kutoka kwa Mola wake Mlezi ya amri ya kuondoka Ninawaa ambako watu walikataa mafundisho ya Allaah. Badala yake Nabii Yunus akajichukulia mwenyewe maamuzi ya kutoroka huku akiwa na huzuni pamoja na ghadhabu. Hakutambua kuwa kufanya hivyo ni kosa na kwamba kuongoa watu si jukumu lake, bali jukumu lake ni kuwahubiria watu mafundisho ya Allaah. Hakika anayemiliki suala la kuongoa si binadamu wala malaika isipokuwa Allaah aliyetukuka. Nabii Yunus alipoondoka katika mji wa Ninawaa, ambako watu walizidhulumu nafsi zao, naye akaamini kuwa wapo tayari kuikabili adhabu itakayoshuka juu yao; Allaah alizilainisha nyoyo zao wakaleta toba na kumrejea Yeye na kujutia mabaya waliyokuwa wakimfanyia Mtume wao Yunus. 

Watu wa Ninawaa wakaleta toba kwa kumtenganisha kila mnyama na mtoto wake, kisha wakamrejea Allaah aliyetukuka na kumyenyekea pamoja na kujikurubisha kwake. Watu wazima wanaume kwa wanawake, watoto wa kike na wa kiume walilia, mifugo yao ikapiga kelele, majike ya ngamia, ng’ombe na kondoo wakatenganishwa na ndama zao. Hali ilikuwa nzito, Allaah kutokana na uwezo wake, upole wake na rehema zake aliwaondoshea adhabu kali mfano wa usiku wenye kiza kinene ambayo lau kama si toba yao ingeliwapata, (Taz: Albidaya Wannihaya:1/232) 

Na kwa kuzingatia hilo, Allaah aliyetukuka anasema: “Kwa nini usiwepo mji mmoja ukamwamini na imani yake ikafaa isipokuwa kaumu ya Yunus? Waliamini na Sisi tukawaondolea adhabu ya hizaya katika maisha ya dunia, na tukawastarehesha kwa muda.” (Yunus aya ya 98). 

Mola wetu Mlezi aliyetukuka ametuhabarisha kwamba imani ya watu wa Yunus iliwanufaisha Allaah akawaondolea adhabu baada ya kuwa imeshawazunguka wao kila upande. Na siku tatu zilipopita, Yunus alirudi kutazama adhabu aliyowaahidi jamaa zake, na ni kitu gani Allaah angefanya. Yunus aliamua kujitenga nao na wala hakuwa anajua kwamba walileta toba na kumrejea Muumba wao. Nabii Yunus aliwakuta watu wa Ninawaa wapo hai, salama salimini, jambo lililomkasirisha Nabii Yunus. Na kwa desturi ya mji wa Ninawaa, malipo ya mtu muongo ni kuuwawa. Hivyo, Nabii Yunus, haraka, akawatoroka kwa jamaa zake kwa kuhofia kuuwawa. Wajibu wake Yunus ulikuwa ni kuridhia maamuzi ya Mola wake Mlezi na kukubali matokeo yake. Mja hana ruhusa ya kughadhibika kwa uamuzi wa Allaah. 

Na ilikuwa haitakikani kwa Yunus kuondoka bila ya maelekezo ya Mola wake. Kwa kuzingatia hilo, ndiyo maana Allaah amemkataza Mtume wetu Muhammad (Swallah Allaahu alayhi wa aalihi wasallam) asiwe kama Yunus aliyemezwa na samaki katika mkasa ambao Allaah aliyetukuka ametuhabarisha ndani ya Qur’an pale aliposema: *”Basi ingojee hukumu ya Mola wako, wala usiwe kama mmezwa na samaki”*(Al-Qalam aya ya 48).

Allash alimtuma Yunus kwa watu wa mji ule ambao waliishi katika mazingira ya ujinga na ushirikina kwa muda mrefu. Kisa cha Nabii Yunus aliyemezwa na samaki mini kwa jamaa zake kulimfanya Yunus (Alayhis salaam) aghadhibike na kuamua kupanda jahazi baharini, lakini jahazi hilo likakumbwa na mtikisiko wa bahari na kuyumba kwa kuzidiwa uzito hadi wasafiri waliomo ndani yake kukaribia kughariki. Kutokana na hali hiyo, wasafiri wakashauri ipigwe kura, na ambaye kura itamwangukia basi ndiye mwenye nuksi na watamtumbukiza baharini ili wapate wepesi katika safari yao. Kwa mara ya kwanza walipopiga kura ilimwangukia Nabii wa Allaah Yunus (Alayhis salaam). 

Mara ya pili ikamwangukia tena Yunus. Hivyo, akataka kuvua nguo zake na kujitupa baharini mwenyewe lakini wasafiri wenzake wakamkatalia kufanya hivyo Kisha wakarudia tena kupiga kura mara ya tatu, na kwa mara nyingine kura ikamwangukia Yunus. Na hii iliyokea kwa sababu kuna jambo kubwa Allaah alitaka litokee kwa Nabii Yunus. Allaah aliyetukuka anasema: “Na hakika Yunus alikuwa miongoni mwa Mitume. Alipokimbia katika jahazi lililosheheni. Akaingia katika kupigiwa kura, na akawa katika walioshindwa. Samaki akammeza hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa” (As-Safaat aya ya 139- 142). 

Yunus alitumbukizwa katika bahari, na Allaah aliyetukuka akamwamuru samaki mkubwa sana wa bahari ya kijani ammeze Nabii Yunus. Vilevile, Allaah aliyetukuka alimwamuru samaki huyo asimtafune na wala asivunje mifupa yake. ”Huyu Yunus si riziki yako.” Hivyo, akammeza na kuzunguka naye bahari zote. “Wakasema: Yunus alipothibiti katika tumbo la samaki alidhani ya kuwa amekufa, akatikisa viungo vyake vikatikisika, ghafla akajikuta yu hai. Hivyo akamnyenyekea Mola wake kwa kusujudu na kusema: ‘Ewe Mola wangu, ewe Mola wangu nimekujaalia msikiti katika sehemu ambayo hajawahi kukuabudu wewe yeyote’” (Taz: Kisasaul Anbiyaai uk 329). 

Ghafla, Nabii Yunus (amani iwe juu yake) akastushwa kwa kujikuta yupo katika viza vitatu, kiza cha usiku, kiza cha kina cha bahari na kiza cha ndani ya tumbo la samaki. Hapa Yunus akahisi kosa lake na kukubali yakuwa amefanya kosa, pale alipotoka katika mji wa Ninawaa bila ya idhini ya Allaah aliyetukuka. Hivyo, ikawa anaswali na kuleta tasbihi na kumtaka msamaha Allaah aliyetukuka akiwa katika tumbo la samaki. Uwezekano wa Yunus kubaki katika tumbo la samaki hadi Siku ya Kiyama ulikuwepo, lakini kulikuwa na jambo moja tu lilimuokoa kutoka katika adhabu hii chungu, nalo ni kumsabihi, na kumdhukuru Allaah pamoja na kuleta dua. Allaah anasema: _*”Na ingeli kuwa hakuwa katika wanaomtakasa Allaah. Bila ya shaka angelikaa ndani yake mpaka siku ya kufufuliwa“*_ (As-Safaat aya ya 143-144).

Katika kisa hicho tuliona kuwa Nabii Yunus alimezwa na samaki baharini ambako aliomba dua akiwa ndani ya tumbo la samaki na hatimaye Allaah akajaalia samaki yule akamcheua. 

Malaika wamwombea Yunus kwa Allaah Aliyetukuka Akiwa ndani ya tumbo la samaki, Nabii Yunus (Alayhis salaam), aliomba dua isemayo: ”Lailaaha illa Anta Sub-hanaka Inniy kuntu Minadhwalimiyn,” (Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu). Maombi haya ya Nabii Yunus yakawa yanazunguka katika Arshi Tukufu ya Allaah. Malika wakasema:  “Ewe Mola wetu Mlezi, hivi hii siyo sauti dhaifu na maarufu inayotoka katika miji migeni ya mbali?” Allah aliyetukuka Akasema: “Hivi hamuijui sauti hiyo?” Wakasema: “Ewe Mola wetu ni nani huyo?” Allaah Aliyetukuka Akasema: “Huyu ni mja wangu Yunus.” Malaika wakauliza: “Mja wako Yunus ambaye bado maombi na amali zake zinakubaliwa?!” Malaika wakasema: “Ewe Mola wetu, tunakuomba umuhurumie kupitia amali zake za kipindi cha raha zimwokoe yeye na balaa hili.” Hivyo, Allaah akakubali maombi ya Malaika na akamwokoa Nabii Yunus kwa kumwamuru samaki ammeze kisha kumtupa ufukweni.”*_ (Taz: Mukhtasar wa Ibin Kathir4/ 18-19). 

Yunus (Alayhis salaam) alitoka katika tumbo la samaki akiwa dhoofu kutokana na maradhi na shida huku kiwiliwili chake kikiwa hakina nguvu. Allaah aliyetukuka anasema: ”Lakini tulimtupa ufukweni patupu, hali yumgonjwa” (As-Safaat aya ya 145). 

Na Allaah aliyetukuka akamuoteshea yeye katika ufukwe wa bahari mti wa Yaqtwini, mmea wenye majani mapana, wenye faida nyingi katika mwili. Nabii Yunus ikawa anakula katika majani ya mti huo na kujificha chini ya kivuli chake kutokana na jua kali. Nabii Yunus akabaki kuwa katika hali hiyo kwa muda mpaka siha yake ikaanza kurejea kidogo kidogo. Imepokewa Hadiyth na Ibn Abii Waqqas (Radhwiya Allaahu an'hu) amesema amemsikia Mtume (Swallah Allaahu alayhi wasallam) akisema: “Jina la Allaah ambalo akiombwa kupitia jina hilo hujibu haraka na anapoombwa haja yoyote ile hutoa, ni dua ya Nabii Yunus.” Ibn Abii Waqqas akamuuliza Mtume: “Ewe, Mjumbe wa Allaah, dua hii ni mahususi kwa Yunus pekee ama ni kwa Waislamu wote?” Mtume akasema: ”Dua hiyo ilikuwa ni mahususi kwa Nabii Yunus, na pia ni kwa waumini wote pindi wanapoisoma.” Kwani hukusikia kauli yake Allaah aliyetukuka pale aliposema: “Na Dhan-Nuni (Yunus) alipoondoka hali ameghadhibika, na akadhani ya kwamba hatutakuwa na uwezo juu yake. Basi aliita katika giza: ‘Hapana Mungu asipokuwa wewe Subhanaka uliyetakasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu.’ Basi tukamwitikia na tukamwokoa kutokana na dhiki. Na hivi ndivyo tunavyowaokoa waumini” (Al-Anbiyaa aya ya 87-88) [Taz: Tafsiri ya Bin Jariri Atwabari,sura ya Al-anbiyaai 17/82] 

Na imekuja katika Hadiyth nyingine ya Mtume (Swallah Allaahu alayhi wa aalihi wasallam) iliyopokewa na Imamu Tirmidhiy na An-Nasai. Mtume amesema: _

Dua ya Dhan-Nuni (Yunus) ‘Lailaahaillaanta Subhaanaka inniy kuntu minadhwaalimiyn,” Muislam akimuomba Mola wake dua hii kwa shida yoyote ile Allaah humtatulia shida yake.”

Simulizi za Nabii Yunus na kijana mmoja Mtume wetu Muhammad (Swallah Allaahu alayhi wa aalihi wasallam) ametuhabarisha kwamba Nabii Yunus alijificha katika kivuli cha mti wa Yaqtwin, na kwamba aikuwa akila majani yake na kwamba kipindi fulani, mti huu ulinyauka na kukauka. Hivyo, Nabii wa Allaah Yunus akalia kutokana na kukauka kwa mti huu, Allaah akamfahamisha kwa kumlaumu: |Hivi unalia kwa sababu ya mti huu kukauka, na wala hukulia kwa watu laki moja au zaidi ya hao uliotaka kuwahilikisha?!”

Na siku moja afya ya mwili wake ilipoanza kurejea vyema, alikuwa anatembea akamkuta kijana mmoja anachunga mbuzi na kondoo. Nabii Yunus akamuuliza kijana yule anatoka katika kaumu gani? Kijana yule akamjibu kuwa yeye anatoka katika kaumu ya Yunus. Hivyo akamtaka amfikishie salamu zake kwa kaumu yake, na awajulishe ya kuwa yeye amekutana na Yunus. Huyu kijana aliyekuwa na busara na utambuzi wa hali ya juu, kwa kuwa alijua hukumu iliyopo kwa jamaa zake kuhusu adhabu ya mtu mwongo, hivyo, akasema kumwambia Yunus: _*“Ikiwa ni Yunus bila shaka unafahamu kwamba adhabu ya mwongo asiyeleta ushuhuda wa kile anachokisema kwa desturi yetu ni kuuliwa. Hivyo basi ni nani atakayenishuhudilia mimi hayo unayoyasema? Yunus akasema: “Mti huu na eneo hili vinatosha kuwa ni shuhuda kwako wewe.” Kijana yule akamwambia Yunus: “Basi mti huu pamoja na ardhi yake viamrishe vinitolee ushahidi.”

Yunus (Alayhis salaam) akawaambia atakapowajieni kijana huyu mtoleeni ushuhuda, mti na ardhi vikajibu: “Ndiyo”. Na yote haya yamefanyika kwa uwezo wake Allaah aliyetukuka. Kijana akarejea kwa watu wake. Naye alikuwa na ndugu wenye hadhi na madaraka katika kaumu yake ambao humkinga yeye na kila anayetaka kumdhuru. Hivyo, kijana yule akamwendea mfalme na akamjulisha ya kuwa amekutana na Yunus, na akafikisha salamu za Yunus kwa mfalme na jamaa zake. Na habari iliyothibiti kwa Mfalme ni kwamba Yunus alikuwa tayari ameshakufa siku nyingi. Wasafiri walimuhadithia Mfalme kuwa Yunus amehiliki baharini kwa kumezwa na samaki. Habari ya kijana huyu kudai kuwa Yunus yu-hai ni uongo shahiri dhahiri. Hivyo mfalme akaamuru kijana yule auliwe palepale. Kijana akasema ana ushahidi unaothibitisha maneno yake. Hivyo Mfalme akatuma watu wake kwenda kuthibitisha jambo hilo. Na walipofika katika mti na eneo ambalo Yunus aliamrisha vitoe ushuhuda, kijana yule akaziuliza ardhi na mti kwa kusema: “Tunakuombeni kwa Allaah, je, nyie mmemshuhudia Yunus kuhusu kadhia hii.” Vikajibu: ”Ndiyo”. Wajumbe wale wakarudisha majibu kwa mfalme wakiwa na hofu na wasiwasi. Mfalme alivyosikia habari hiyo alijivua madaraka yake, akaushika mkono wa kijana yule na kumkalisha katika kiti chake cha ufalme, na kisha kumsimika ufalme kwa kumwambia: “Wewe unastahiki zaidi wadhifa huu kuliko mimi.” Na Mtume wetu (Swallah Allaahu alayhi wa aalihi wasallam) ametuhabarisha kuwa kijana huyo alihukumu kwa kipindi cha miaka 40, akisimamia mambo ya watu wake kwa kusuluhisha baina yao.

Na Allaah Ni Mjuzi Zaidi

(Al Kamaalu Lillaah)..


Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA YA NABII SULEIMAAN

The Story of the Prophet Idris (AS)

The Story of Prophet Dhul Kifl