Nabii Adam A.S
KISA CHA KUUMBWA NABII ADAM (A.S) & MAUAJI YA KABIL KWA NDUGU YAKE KABIL
Allah (S.W) kitu cha kwanza kukiumba ulimwenguni ni Qalam ambayoameiumba kwa ajili ya kuandika mema na maovu ya viumbe, aliumba Lauhul-Mahfuudh na vyenginevyo. Allah aliumba mbingu saba (7) siku sita (6) katika matabaka mbali mbali pamoja na mchanga (ardhi) siku ya Jumaamosi, aliumba majabali katika siku ya Jumaapili, miti siku ya Jumaatatu, vitu vyote vyenye kuchukiza aliviumba Allah katika siku ya Jumaane, nuru siku ya Jumaatano, viumbe katika siku ya Alhamis na mwisho alimuumba Adam (AS) katika siku ya Ijumaa nyakati za Alaasiri ndio siku ya mwisho ambayo wanaadamu wote wataondoka ulimwenguni.
Lakini kabla ya kuumbwa Nabii Adam, Allah alikuwa tayari amekwishawaumba majini ambao walifanya ufisadi katika ardhi na walimwaga damu za wengine. Hatimae Allah aliwapelekea majini hao jeshi la malaika na wakateketezwa majini wote.
Mara tu baada ya Allah kuwateketeza majini hao, malaika Jibriil alimbakisha mmoja katika kizazi cha majini aliyeitwa AZAAZIIL (Iblis )kwa vile jinni huyo alimuabudu sana Allah, hivyo Allah alimuweka pamoja na malaika peponi. Iblis aliendelea kumwabudu Allah mpaka akafikia kuitwa Abaasijda, kutokana na wingi wa sijda zake kumsujudia Allah. Hivyo ijapokuwa hakuumbwa kwa nuru (aliumbwa kwa moto), lakini Iblis alishirikiana na malaika katika ibada kumwabudia Allah.
Siku moja Allah aliwadokeza malaika kuwa anataka kuumba kiumbe mwingine duniani. Malaika wakafikiri mambo yaliyowatokea kabla ya Adam, najinsi wale majini walivyofanya ufisadi katika ardhi.
Hivyo malaika hao wakasema kwa kumuuliza katika quran tukufu,“Ewe molaunataka kuweka katika ardhi anaetaka kufanya ufisadi na kumwaga damu, kamawalivyomwaga damu waliopita. Au unataka kuleta kiumbe atakaekuabudu kwa wingi na je sisi tumepunguza kitu katika ibada yako? Na hali sisi tunakutukuza natunakusabbihi kila usiku na mchana?”.
Nae Allah akawaambia katika qurani tukufu, “Mimi ninajuwa vilemsivyovijuwa nyinyi”. Kutokana na uchamungu wao malaika wakasema ,”Basi aumbe Allah vileanavyovipenda katika viumbe. Lakini hawatokua viumbe hao wabora na wajuzi kuliko sisi”.
Hivyo Allah akauchukuwa mchanga wa aina mbali mbali na akaufinyanga kwa hatua mbali mbali mpaka ukafikia kwenye kiumbe mfano wa sanamu. Hivyo Allaha kasimamisha sanamu hiyo ya Adam kwa muda wa siku arubaini (40), na wakati ikiwa imesimama kila siku malaika walikuwa wakipita na kuiangalia sanamu hiyo iliyoweka uwanjani hapo. Hivyo hapo sasa ikawa ni mwanzo wa fitna na kejeli kwa iblis kwani alihisi kiumbe huyo atakuja kupewa thamani kubwa kuliko wao, lakini mmoja wa malaika alipewa elimu ya kujuwa kitu cha baadae na Allah hivyo akawa anawatoa wasiwasi wenzake juu ya kiumbe hicho.
Katika siku ya arubaini Allah akaileta roho na kuanza kukipuliziakiwiliwili hicho. Hapo Adam akapiga chafya na ndipo malaika wakamwambia Adam, “Ewe Adam sema alhamdulillahi kwani roho ndio kwanza imewasili”. Adam hapo hapo kwa kushukuru akasema alhamdulallahi na Allah akamuitikia na ndipo roho ikaingia machoni ambapo Adam akaona matunda ya aina kwa aina peponi akaanza kuyatamani matunda yale ilhali roho haijafika hata tumboni, akataka pia kutembea wakati roho haijafika hata miguuni, na ndio maana mwanaadamu akawa ana tabia ya kuwa na pupa katika mambo yake siku zote.
Roho taratibu ikaingia kiungo kimoja baadaya kingine mpaka ikamalizia miguuni. Hapo ndipo Allah akamuamrisha Adam apite mbele ya malaika na awatolee salam na hapo ikawa ni mwanzo wa salam katika Uislam. Allah akasema, “Haya yatakuwa ni maamkizi kwa umma wako”. Allah alimfundisha Adam majina ya vitu vyote duniani, pamoja na matumizi ya vitu hivyo. Allah alivileta vitu hivyo mbele ya malaika na akawaambia,”Nielezeni majina ya vitu hivyo ikiwa nyinyi ni wakweli”. Malaika wakashindwa na wakajibu kumwambia Allah,”Utakasifu ni wako ewe mola, na sisi hatuvijui vitu hivyo ispokuwa vile ulivyotufundisha tu”. Allah akamleta Adam na akamwambia avitaje vitu hivyo vyote, nae Adam hakusita akavitaja vitu hivyovyote. Hapo ndipo Allah akawaambia malaika, “Ninayajuwa yale msiyoyajuwa, basimsujudieni Adam”.
Hapo malaika wote walisujudu ispokuwa Iblisi pekee akakataa na akafanya kiburi na akawa ni miongoni mwa waliokufuru. Allah akamuuliza Iblisi, “Ni kipi kilichokuzuia kumsujudia Adam pale nilipokuamrisha?”. Iblisi akajibu,”Mimi ni bora kuliko yeye umeniumba kwa moto naye umemuumba kwaudongo”. Hapo ndipo Allah akamjibu,”Toka katika rehma zangu, huna uwezo wakukataa amri yangu. Basi utakuwa ni miongoni mwa madhalili”. Iblisi akasema kwaAllah,” Ewe mola umenilaani kwa sababu ya kutomsujudia kiumbe hichi. Nipe muda niishi”. Allah akamkubalia ombi lake kwa kusema,”Utaishi mpaka mwisho wa ulimwengu”. Iblisi akasema, ”Hakika nitawazuia waja wako katika kukuabudu na nitajitahidi, hivyo hutowapata wengi wao walionusurika”. Allah akamjibu,”Basi ondoka hali ya kuwa ni dhalili na yeyote atakaekufuata nyote mtakuwa motoni”. Adam aliishi peponi pekee hali ya kuwa ni mpweke, na Allah alimuonaAdam akiwa ni mynonge peponi akiranda huku na kule bila ya mtu wa kumliwaza. Hivyo siku moja Adam alihisi maumivu makali ubavuni mwake kushoto, kumbe Allah alikuwa anamtoa kiumbe mwengine katika mwili wake kutokana na yeye. Adam alipoteza fahamu na mara tu baada ya kushtuka alikuta kiumbe kimemsimamia. Malaika ambao walikuwa karibu wakataka kumpa mtihani Adam kama ni kweli anafahamu kila kilchomo ulimwenguni, wakasema kumuuliza,”Ewe Adam ni nani huyo?”.
Adam akawajibu, “Huyu ni utulivu kwangu”. Malaika wakamuuliza tena,”Je! Unamjuwa jina lake?” Adam akajibu,”Jina lake ni Hawaa”. Hawaa ni jina lenye maana ya ubavuni na alikuwa ni mwanamke mzuri zaidi duniani kuliko wanawake wote. Hapo ndipo malaika wakamuuliza tena Adam,”Kwa nini ameitwa Hawa?” Adam akawajibu,”Kwa sababu ametokana na kiumbe hai”.
Allah akamwambia Adam,”Ewe Adam ishi na mkeo peponi na kuleni kila kitu ispokuwa kimoja tu msikikaribie (mti). Kwani mtakuwa ni miongoni mwamadhalimu.” Maisha ya Adam na Hawa yalikuwa ni mazuri tu peponi kwa vile walistarehe kwa kupata kila kitu walichokihitaji, na wakawa na hadhari kubwa sana kwa kufuata waliyoamrisha na kujiepusha na waliyokatazwa.
Kila walipo ukaribia ule mti haraka walijiweka mbali nao, matunda yake hayakuwa ni mazuri kama yalivyokuwa matunda mengine na Allah aliwakataza tu ili kuwapa mtihani. Iblisi aliumia na kuwaonea choyo na alikuwa Adam ndiye aliyesababisha kutolewa kwake katika rehma za Allah peponi. Hapo Iblisi akaanza kuwaza jinsi ya kuwafanya Adam na Hawa wamuasi Allah ili nao wafukuzwe katika neema hizo. Mwishowe akaona awafanye wavunje lile sharti walilopewa na Allah yaani wakalile tunda la ule mti uliokatazwa.
Iblisi aliona kuwa wanapendana sana na akatumia mapenzi yao kuwaondosha peponi, akaanza kujirusha rusha na kupiga ngoma nakufurahi kwa vile aliona njia hii ni sahihi. Hivyo Iblis akaanza kujiwe kamahala ambapo Adam na Hawa watamouna na bila ya wao kumtambuwa kama ni Yule aliyefukuzwa peponi. Akawa analia sana na ndipo Adam na Hawa walipo mshangaa kumwona mtu analia katika eneo hilo, hapo hapo wakamsogelea na kumuuliza. Iblis akawajibu, “Nakulilieni nyinyi.” Adam akamuuliza huku akimsogelea,” Ki vipi?”.Iblis aliendelea,”Kwa sababu mtakufa na kuziwacha nyuma neema zote mlizonazo.”
Ghafla Adam na Hawa wakaingia huzuni, ndipo Iblis alipoona kuwa ameshawaweza kwa namna ya kwanza ya kuwatia huzuni. Adam na Hawa hawakumjuwa Iblis kwa taswira aliyoyojifanani sha. Juu ya yote hayo Allah alishawaambia kuwa watakaa humo milele, lakini Iblis akawashawishi na kuwapa fikra nyengine kuwa watakufa na wataiacha pepo. Hawaa alivutwa ziadi na Iblis na akawa anamhakikishia Adam ya kuwa neema zao hizo zitawatoka, lakini Adam alikaza moyo na akaamuwa aachane na mawazo hayo. Pia Adam moyoni mwake akawa na hofu juu yamaneno hayo, na ndipo wakawa hawana tena furaha wakati wlipokuwa wakitembea peponi. Siku chache mbele walikutana tena na Iblis, Iblis akawauliza, “Je! Mumefikiria jambo ambalo litakufanyeni mkae milele humu peponi?” Kwa pupa Hawaa akamuuliza, “ Ni jambo gani hilo na inawezekanaje?”. Iblis alijifanya anajuwa zaidi ukweli wa mambo na ndipo akamgeukia Adam na kumwambia, “Ewe Adam nikujuulishe mti utakaokufanyeni mkae milele?” Wote wakaitikia na Iblis akaendelea kusema, “Kuleni matunda ya mti ulee (mti uliokatazwa).” Adam akajibu kwa mshangao, “Lakini sisi tumeshakatazwa na mola wetu.”Mola wenu hajakukatazeni ila msijekuwa nyinyi malaika au kuwa wenye kukaa milele.”
Iblis akawapia kwa kusema, “Hakika mimi kwenu ni mtoaji nasaha mzuri hivyo msije mkakataa na mkajuta”. Hivyo Adam akawa tayari kula tunda la mti huo na alishawishiwa zaidi na mkewe Hawaa, ingawa hapo awali alikuwa ni mpinzani mkuu. Sauti ya mwanamke ilimhadaa na hapo hapo walikula matunda yale wote wawili.
Mara tu walipokula nguo zao zikawavuka na ikadhihirika aibu yao iliyokuwa imefichwa na wakawa uchi huku wakitafuta majani ya humo peponi ili wajifunike tupu zao. Adam akamuasi mola wake na Iblis akatimiza kwa mara ya kwanza lengo lake (Suratu ttwaaha). Allah akawaita, “Ewe Adam, ewe Hawa! Je!Mimi sikukukatazeni kuwa msile matunda ya mti huu? Na nimekwambieni mbele kuwa shetani ni adui aliye wa wazi kwenu?” Wote wawili wakasema kwa majuto,” Ewe mola wetu hakika sisi tumejudhulumu wenyewe nafsi zetu, na usipotusamehe na kuturehemu tutakuwa ni miongoni mwa waliokula hasara”.
Adam akaanza kukimbia peponi kwa haya ya kumwogopa mola wake. Allah akamwambia, “Ewe Adam leo hii unanikimbia?” Adam akajibu, “Ewe mola wangu, nakimbia kwa sababu ya kuona haya.” Allah akamwambia, “Shukeni huko peponi kwani baadhi yenu na baadhi ya wengine ni maadui, nendeni katika ardhi.”
Wote wakatereshwa ardhini na kila mmoja akateremshwa sehemu tafauti na mwenzake. Adam aliteremshwa India na Hawa aliteremshwa sehemu iitwayo Jidaa(Khaleej Mamlakatu –Aaraabiyyah) na Iblis akateremshwa Baabiil. Hawa akaanza kumtafuta Adam na Adam nae akaanza kumtafuta Hawa. Hivyo wote wakaanza kuhangaika na uzito wa maisha ukaanza, kama alivyokwisha ambiwa na Allah kuwa atapatashida. Baada ya mahangaiko marefu wote wawili wakakutana sehemu iitwayo Arafah (Wanazuoni wamepaita jina hilo kwa sababu ya kujuana kwa Adam na Hawa).
Hivi leo Hivi leo tu ni sehemu ambayo hukutana mahujjaj ndani ya mfunguo tatu (30) mwezi tisa(9). Hivyo katika sehemu hiyo Adam na Hawa wakaanza maisha mapya. Huku awali Allah aliwaambia, “Shukeni huko huko iwapo utakujieniuongofu. Basi mwenye kufuata uongofu wangu hatopotea wala hatokuwa mbaya. Lakini Yule atakaeupa mgongo utajo (uongofu) wangu, basi ajuwe kuwa atakuwa na maisha ya dhiki na tutamfufua siku ya kiama hali ya kuwa ni kipofu. Atauliza : Ewe mola wangu mbona umenifufuwa kipofu. Allah atamjibu : Wewe ulizipuuza aya zetu...”
HABIL NA KABIL :
Kuanza kwa ndoa
Mara tu baada ya kukutana Allah akawapa kizazi wote wawili. Allah akawajuulisha jinsi ya kupata watoto, na wakaingiliana mpaka ikaja ishara kuwa Hawa atapata mtoto wa kwanza aliyeitwa Kabil na dada yake, na mwengine ni Habil na dada yake mpaka watoto wote wakafika arubaini (40). Kila mimba iayozaliwailikuwa ni pacha (wa kike na kiume). Wakwanza aliitwa Habil na wa mwisho aliitwa Abdul- Mughiir na dada yake. Kizazi kikaenea kidogo kidogo na watoto wakawa na ndugu kila mmoja na pacha wake. Kabil kazi yake ilikuwa ni kulima na Habil alifuga wanyama na Adam alifanya shughuli zake za kawaida na maisha yaliendelea vizuri tu.
Watoto wakawa ni watu wazima na walihitaji kuoa. Lakini ikatoka sheria kutoka kwa baba yao Adam ambae ni mtume wao kuwa kila mmoja ikiwa anataka utulivu basi aoe pacha wa mwenzake. Hivyo ikawa Habil anatakiwa amuoe pacha wa Kabil na Kabil amuoe pacha wa Habil. Hapo ugomvi ukaanza ya kuwa itakuwaje Kabil amuoe pacha wa Habil ilihali pacha wa Habil si mzuri, Kabil alitaka amuoe pacha wake mwenyewe. Adam akamwambia Kabil , ‘’Haiwezekani wewe huyu ni dada yako, huwezi kumuoa, muoe yule kwani ndivyo ruhsa ilivyotolewa’’.
Kabil alikataa na Adamu akamwachia Allah (S.W) mwenyewe apitishe hukumu baina yao. Kabil akachukuwa nafaka na Habil akapeleka kondoo mnene katika uwanja wa hukumu. Hapo ndipo Allah (S.W) akapeleka umeme ambao ulimchukuwa kondoo wa Habil, kuonesha kwamba Habil amekubalika mbele ya Allah (S.W) amuoe pacha wa Kabil, na nafaka zikaachwa palepale kuashiria ya kwamba hakukukubalika amuoe pacha wake mwenyewe.
Kifo Cha Habil
Hivyo Kabil alipoona Habil amekubaliwa akamwambia: ‘’Madam Mungu amekukubalia wewe, basi nitakuuwa’’. Habil akamjibu: ‘’Mimi nimekubaliwa kwa kuwa ni mchamungu, na ukinyanyuwa mkono wako kuniua mimi sitokufanya lolote nitamuachia Mungu kwani namuogopa Allah (S.W)’’.
Hapo hapo Kabil akafanya njama za kumuua na Iblisi akamfundisha kwa kumwambia: ‘’Wewe unataka kummaliza huyo? Basi mnyatie kalala, mpige jiwe atakufa’’ (Kwa mujibu wa wanazuoni).
Basi akatumia njia hiyo na akamuua na akawa ni miongoni mwa wale waliokula khasara. Kwani Mtume (S.A.W) anasema : ‘’Jiepusheni na madhambi saba (7) yenye kuangamiza...’’ Ambapo miongoni mwao ni kuuwa.
Baada ya hapo Kabil akambeba ndugu yake Habil mgongoni na akawa hajui cha kufanya kwa vile alimuona tayari ameshakufa. Habil alikuwa ni mwenye nguvu kuliko Kabil lakini alimuachia amdhuru kwa vile Habil alikuwa ni mstaarabu na Mchamungu.
Kama Mtume (S.A.W) anavyosema kuwa ukakamavu si kuwa maguvu mengi, lakini ukakamavu (hodari) ni yule ambae anaimiliki nafsi yake wakati wa ghadhabu. Hivyo mpaka hii leo mtu akiuwa kwa makusudi duniani, Kabil anapata adhabu kaburini kwa vile yeye ndiye wa kwanza kuanzisha njia hii mbaya. Allah (S.W) alipomuona Kabil anahangaika akampelekea kunguru wawili.Kunguru hao wakapigana mpaka mmoja wao akamuuwa mwenzake. Baada ya kumuua akachimba shimo ardhini na alipomaliza akambeba mwenzake na kumfukia shimoni humo. Kabil baada ya kuona tukio hilo naye akasema :’’Kwa nini nami nisichimbe shimo ili niifukie maiti ya ndugu yangu.’’ Hapo hapo nae akamzika ndugu yake Habil na akawa ni mwenye kujuta. Adam (A.S) baada ya kusikia habari za kifo hicho akahuzunika huzuni kubwa sana ya kifo cha Habil. Allah (S.W) anasema : ‘’Kwa ajili ya hayo tuliwaambia Banuu-Israiil kwa yoyote atakayeua nafsi kwa dhulma ni sawa na kumwaga damu ya viumbe vyote’’.
Mtume (S.A.W) pia anasema :’’Mwenye kuuwa akashiriki japo kwa nusu neno, anaandikwa katika kipaji chake cha uso kuwa amekata tama na rehma zaAllah (S.W)’’.
-Maradhi na Kifo Cha Adam (A.S)-
Adam (A.S) alimlaumu Kabil na tokea hapo akaishi umri wake mrefu tu mpaka siku moja alipopata maradhi kitandani. Aliwaita watoto wake na kuwaambia:’’Enyi wanangu nina hamu ya kula tunda la peponi, hebu nendeni mkanitafutie’’.
Watoto wakatoka kwenda kumtafutia baba yao tunda la peponi, na kama ilivyo ada ya mtu anaekaribia kufa hutamani vitu vingi tu pengine vyengine haviwezekani kupatikana kwa wakati huo. Njiani wakakutana na malaika Jibriil nae akawauliza, ‘’Mnakwenda wapi?’’. Watoto wakamjibu, ‘’Tunakwenda kumtafutiababa yetu tunda la peponi. Malaika akawaambia, ‘’Rudini kwani baba yenu ameshakufa’’.Waliporudi wakamkuta baba yao kweli ameshakufa, lakini Adam (A.S)alisha waahidi kuwa yeye na watoto wake watarudi peponi baada ya kufa kwa kutenda mambo mema. Pia Bi Hawa hakuwa na hali nzuri na hivyo ulipofika muda malaika wakafika tayari kwa kuichukuwa roho yake.
Hapa wanazuoni wanasema kuwa malaika wenyewe wakamtia sanda, wakamsalia kwa takbira nne (4) na wakamchimbia kaburi na kuwaambia watoto wake kwamba, ‘’ Hii itakuwa ndiyo sunna yenu na vizazi vyenu’’.
Wanazuoni wengi walitofautiana kuhusu sehemu aliyozikwa Adam (A.S),yaani husema kuwa alizikwa India, wengine husema alizikwa jabali maarufu yaaniJabal Abiy Qubays pale Maka, wengine husema alizikwa Baitul Maqdis, ilhalimiaka michache tu baada ya kifo cha Adam (A.S) alikufa Bi Hawa. Kizazi cha Adamkikawa na dini ile ile ya Uislamu na sheria zile zile za Adam (A.S) nahawakuabudia masanamu. Mtoto maarufu aliyepatikana katika zama hizo alikuwa ni Shiif ambae alikuwa ni nabii na kupewa suhuf (kurasa) baada ya Adam (A.S)ambapo nae pia aliendeleza daawa na kalmia yake ilikuwa ni: Muabuduni Allah(S.A) na jiepusheni na ibada ya masanamu. Hivyo umma huu mpaka kufikia kwaNabii Nuhu (A.S) ulikuwa ni mmoja na haukuwa na mabadiliko yoyote, walimfuataMungu mmoja na ibada ya masanamu ilikuwa ni mwiko
MWISHO
MAREJEO:
QURAN:
- Baqarah - 30,
- Ghafir - 67,
- Taha - 55,
- Rahman -14-15,
- Saad - 72,
- Anbiya-a -37,
- Baqarah - 31,
- A-alaaq - 1-5,
- Faatwir - 28,
- Twaaha - 114,
- Baqarah
- -32,163-4,
- Imraan - 190,
- Yunus 5-6,
- Yunus - 101,
- Namli - 60-64

Comments
Post a Comment