KISA CHA NABII LUUT
KISA CHA NABII LUUT
Luut bin Haaraan nae ni mtoto wa ndugu yake Ibrahim (AS), pia anakuwa mtoto wa khaloo yake. Kwa hivyo Taarikh na mwanawe Haaraan wameowa ndugu wawili watoto wa Laahij na wakazaliwa Ibrahim bin Taarikh na Luut bin Haaran (AS). Na Bibi Sarah mkewe Ibrahim (AS) ni ndugu yake Luut (AS) kwa mama. Ametajwa Luut katika Quraan mara ishirini na saba katika sura kumi na nne. Baba yake alifariki nae ni mdogo na akalelewa na Taarikh pamoja na ami yake, Ibrahim (AS) wakakulia pamoja, na Ibrahim alikuwa akimpenda sana.
Kama tulivyotaja kabla katika kisa cha Ibrahim (AS), aliondoka yeye na Luut (pia Bibi Sarah) huko Misri, wakaelekea Falastini. Luut (AS) alikaa pamoja na ami yake, Ibrahim (AS), katika nyumba yake. Lakini hapa Ibrahim (AS) akamuamuru Luut (AS) ahamie katika kijiji kinachoitwa Sadoum ambacho pia kinajulikana kwa jina la Al-Muutafika. (Hapa pana ziwa katika Dead Sea linalojulikana kwa jina la ziwa la Luut.) Kwani katika kijiji hichi kulikuwa umeenea ukafiri na ufisadi, basi Ibrahim (AS) alimtaka Luut (AS) ende huko ili akawaligane watu hawa ili waache mambo mabaya wanayoyafanya na wamuabudu Mwenyenzi Mungu.
Watu wake walikuwa ni wenye ufisadi mkubwa na nia mbaya nao wakifanya maasi na walikuwa watu makhabithi na majambazi. Wakiiba mali za watu na kuwaacha masikini za Mungu wanalia, nao walikuwa hawasikii nasaha za mtu yeyote. Na katika maasi yao makubwa walikuwa wakiwatenda vitendo vibaya wanaume kwa kuwaingilia na kuacha wanawake, waliohalalishiwa na Mwenyenzi Mungu. Hawajapatapo kuwa na watu walio waovu kama hawa watu wake Luut (AS) na Mwenyenzi Mungu kawataja katika Quraani kwa kila namna ya majina mabaya, Wafujaji, Mafisadi, Waovu na kadhalika.
Anasema Mwenyenzi Mungu:
“ Na (tulimpeleka) Luut. Basi (wakumbushe watu wako) alipowaambia kaumu yake: ‘Jee! Mnafanya ufasiki ambao hajakutangulieni yeyote kwa ufasiki huo katika walimwengu! Nyinyi mnawaendea wanaume kwa kuwa ndio mnaowatamani badala ya wanawake! Ama nyinyi watu wafujaji.’ #
Basi Luut (AS) aliwanasihi sana waache mambo hayo na wamuabudu Mwenyenzi Mungu lakini alishindwa, na inasemekana kuwa hakuamini mtu isipokuwa watoto wake wawili wanawake. Alipoona hivi aliwatisha kuwaambia kuwa wataletewa adhabu ya Mwenyenzi Mungu, wala haikufaa kitu.
Anasema Mwenyenzi Mungu katika aya hizi:
“ Watu wa Luut waliwakadhibisha Mitume # (Wakumbushe) alipowaambia ndugu yao, (Nabii) Luut: ‘Jee, hamuogopi? # Bila shaka mimi kwenu ni Mtume muaminifu #Basi mcheni Mwenyenzi Mungu na nitiini # Wala sikutakini ujira juu yake; ujira wangu hauko ila kwa (Mwenyenzi Mungu) Mola wa walimwengu wote.’ # 1
Mwito ule ule wa Mitume wote anapowalingana watu waamini, na nini jawabu lao lilikuwa baada ya kuwaambia haya? Walisema:
“ Tuletee adhabu ya Mwenyenzi Mungu ikiwa umiongoni mwa wasemao kweli.!’
Yale yale waliosema watu wa Nouh, wa Huud na wale wa
Saleh (AS) kabla ya hapa. Vile vile walisema: “ Wafukuzeni katika mji wenu, maana hao ni watu wanaojitakasa (hawataki haya machafu tunayoyafanya). Basi nawatoke. Wanakalia nini?’
Angalia namna gani watu hawa walivyopindukia kiasi katika ufisadi wao, hawataki kuwaona watu waliotakasika katika mji wao, wanataka watu wote wawe sawa sawa na wao.
Luut (AS) akamwomba Mola wake amuepushe na watu hawa waovu mafisadi na awaletee adhabu, jaza yao kwa kukufuru.
“ Akasema: ‘Mola wangu! Ninusuru juu ya watu mafisadi (hawa).’
Mwenyenzi Mungu akamwitikia mwito wake na akampelekea Malaika kwa watu wa kijiji hichi, madhalimu awaletee adhabu wanayostahiki. Hao Malaika ni wale walioingia kwa Ibrahim (AS) kwanza, naye aliwafikiri wageni wapita njia, kama tulivyoona katika hadithi hiyo. Akawakirimu inavyopasa kukirimiwa wageni, lakini alipoona mikono yao haikufikilia chakula walicholetewa, Ibrahim (AS) aliwaogopa kudhania maadui. Basi Ibrahim (AS) baada ya kuzipokea habari (za kubashiriwa kupata mtoto) kwa furaha, aliwauliza nini makusudiyo yao, baada ya haya?
“Akasema: ‘Basi makusudio yenu (mengine) ni nini, enyi mliotumwa?’ Wakasema: ‘Hakika sisi tumetumwa tukawaangamize wale watu waovu. (Watu wa Nabii Luut). # Ili tuwatupie juu yao mawe ya udongo (wa Motoni). # Yaliyotiwa alama kwa Mola wako kwa ajili ya hao watu wanaopindukia mipaka katika maasia.’ #
Ibrahim (AS) aliwaomba waakhirishe hiyo kazi yao asa huenda hao watu wake Luut (AS) wakasikia na kujirudi.
“Akasema (Nabii Ibrahim): ‘Hakika humo yumo Luut.’ Wakasema: “Sisi tunawajua sana waliomo humo, kwa yakini tutamuokoa yeye na watu wake ila mkewe aliye miongoni mwa watakaokaa nyuma.’
Akamwomba Mola wake kuchelea asije Luut naye ikamfika hiyo adhabu wanapoteremshiwa watu wake, na yeye ni katika watu walioamini. Malaaika wakamwambia kuwa asisikitike juu ya watu hawa wasiosikia na wakamwambia kuwa Luut (AS) hatofikwa na kitu, na atakuwa yeye na watu wake wa nyumbani salama, isipokuwa mkewe kwani yeye yumo pamoja na hao wanaofanya maasi.
Malaika walipokwisha ondoka kwa Ibrahim (AS) wakenda Sadoum, (kwa sura ya vijana wazuri). Walipofika wakataka kuingia katika kijiji hicho, walimwona mwanamke mmoja alikuwa akitilia maji katika shamba. Wakamwomba ikiwa wanaweza kuwa wageni kwake. Akawaonea huruma kwa kuwaogopea watu wake naye hawezi kuwanusuru. Akenda kumwita baba yake akamwambia: “Ewe baba yangu kuna vijana wanakutaka, nao sijapata kuwaona sura zao kabla hapa kwetu, inaonesha ni wageni. Nami nachelea wasije wakajuwa watu wa mji wakawadhuru.”
Huyu baba mtu alikuwa ni Luut (AS) na huyu mwanamke ni mwanawe, basi alishituka kusikia khabari hii na akawa anamuuliza mwanawe khabari ya vijana hawa. Kwanza alifikiri asende kuwakabili na atoe udhuru, lakini mwito wao ulimvuta ende kuonana nao. Basi akenda akawakabili wageni wake kwa uzuri akawachukuwa kwake. Akachelea kuwa habari zao zitawafikia watu wake; lakini kwa vile mkewe alikuwa pamoja nao watu hao katika maasi, habari za wageni hao mara zikawafikia.
Waliposikia tu mara walikuja kutaka kujuwa habari za hao vijana. Luut (AS) alioogopa alipoona umma wa watu umekusanyika nje ya nyumba yake, wanataka shari. Luut (AS) alijaribu kuwanasihi wasifanye maovu kwa wageni hawa lakini wasimsikilize bali walifanya stihizai na mizaha, nae akaingia ndani akafunga mlango. Baadae akatoka akawaambia:
“ Enyi kaumu yangu! Hao binti zangu (binti za umma wangu walioolewa katika nyumba zenu) ndio wametakasika kwenu (kuwaingilia si wanaume wenzenu). Basi mcheni Mwenyenzi Mungu wala msinifedheheshe mbele ya wageni wangu. Je, miongoni mwenu hakuna mtu mwongofu (hata mmoja)?’
Luut (AS) aliwanasihi sana watu wake waache maasi ya kuwaingilia wanaume na akawaambia wachukuwe wanawake ambao wamehalalishiwa na Mwenyenzi Mungu. Akawaomba wasimfedhehi mbele ya wageni wake, wakakataa wakasema:
“ Wakasema: ‘Bila shaka umekwisha juwa haki tulizonazo juu ya binti zako, (lakini hatuzitaki), na unayajuwa tunayoyataka.’ # Akasema: ‘Laiti ningalikuwa na nguvu kwenu (mimi mwenyewe) au nategemea kwenye nguzo yenye nguvu (watu wenye nguvu ili wanisaidie juu yenu).’ # (Wale wajumbe) wakasema: ‘Ewe Luut sisi ni wajumbe wa Mola wako (Malaika). Hawatakufikia (kwa baya lolote). Na ondoka pamoja na watu wako katika sehemu ya pingapinga (katikati) la usiku. Wala yoyote miongoni mwenu asitazame nyuma (ataposikia vishindo vya kuangamizwa hao wabaya asije akarukwa na akili kwa kuona adhabuu kali hiyo). Isipokuwa mke wako (mwanamke mbaya huyo hatakufuata). Nae utampata msiba utakaowapata hao. Hakika miadi ni asubuhi. Jee, asubuhi si karibu tu? (Basi tuliza moyo wako. Umekwishafika wakati wao wa kuangamizwa).’ # 1
Basi walitaka kuingia katika nyumba yake kwa nguvu. Hapa alitoka (Jibril) mmoja katika wale wageni wake akawapa adhabu ya mwanzo.
Anasema Mwenyenzi mungu:
“ Na walimtaka (awape) wageni wake (ili wawafanye
machafu) Tukayapofusha macho yao; (na tukawaambia) ‘Onjeni adhabu yangu na maonyo yangu!’ # 2
Juu ya haya hawakutubu, wakasema kuwa huu ni uchawi, nao wamerogwa tu. Wakapapasa kuta wakarejea makwao. Hapa Jibril (AS) akamwambia Luut (AS): “Waache kwani adhabu yao itawafikia asubuhi, nayo haipo mbali.”
Akaamrishwa Luut (AS) atoke na watu wake kwenye kijiji hicho awaache hao watu walioandikiwa kushushiwa adhabu, na alikatazwa kumchukuwa mkewe kwani alikuwa mmoja katika wao waliokufuru. Hapa baadae iliwajia hiyo adahbu waliyokuwa wakiikanusha.
Anasema Mwenyenzi Mungu:
“ Basi ilpofika amri yetu, tuliifanya (ardhi hiyo iwe juu chini); juu yake kuwa chini yake, na tukawateremshia mvua ya changarawe za udongo mgumu (wa Motoni
uliyokamatana). (Changarawe) zilizotiwa alama kwa Mola wako (kila moja kuwa ya mtu fulani). Na (adhabu) hii haiko mbali na madhalimu (wengine kama hawa watu
wa umma huu wanaofanya machafu haya).
Kama tulivyoona, mkewe Luut (AS) alikuwa ni katika wale waliokufuru nae aliangamizwa pamoja nao. Anasema Mwenyenzi Mungu katika aya hizi juu mwanamke huyu na yule mke wa Nouh (AS): “ Mwenyenzi Mungu amepiga (anapiga) mfano wa wale wabaya waliokufuru, ni mkewe Nuuh na mkewe Luut. Walikuwa chini ya Watumwa wetu wema wawili hao miongoni mwa watumwa wetu (wema); lakini (wanawake hao) waliwafanyia hiana (waume zao watukufu hao), na (waume zao hao) hawakuweza kuwasaidia cho chote mbele ya Mwenyenzi Mungu na ikasemwa: ‘Uingieni Moto pamoja na hao wanaouingia.’
Ukaangamizwa mji wa Sadoum na kuachwa mfano kwa walimwengu wote waone ili wasome na watahadhari na adhabu za Mwenyenzi Mungu kwa vitendo vibaya, hasa kama vitendo vya hao watu wa Luut (AS). Akatoka Luut (AS) na watu wake wamesalimika na adhabu hiyo iliyowajia watu hao. Anasema Mwenyenzi Mungu:
“ Basi tukamuokoa yeye na watu wake wote. Isipokuwa kikongwe (aliyekhitari kuwa) katika wakaao nyuma. (Wasimfuate Nabii Luut, naye ni mkewe mwenyewe Nabii
Luut). Kisha tukawaangamiza wale wengine (aliokwenda mke wa Nabii Luut kuchanganyika nao).

Comments
Post a Comment