KISA CHA NABII IBRAHIM 1

KISA CHA NABII IBRAHIM 


بسم الله الرحمن الرحيم

 الحمد لله رب العالمين والصلاة والسلام على اشرف الانبياء والمرسلين نبينا محمد وعلى اله وصحبه اجمعين و بعد

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alizaliwa Iraq, inavyosemekana Babylonia. Baba yake akiitwa Aazar na kauli nyingine inasema kuwa huyu ni ami yake aliyemlea tokea mdogo baada ya kufa baba yake. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ni Mjuzi zaid. Na huyu Aazar alikuwa akichonga masanamu.

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) ni Khaliylul-Allaah. yaani kipenzi wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amemchagua kumpa Risala Yake na Akamfadhilisha zaidi ya viumbe Vyake vingine. 

Alikuwa akiishi na watu waliokuwa wakiabudu sayari (nyota, mwezi, jua na kadhalika), na wengine wakiabudu masanamu na wengine wakiabudu wafalme wao.  Hakuridhika na ibaada hizo zao, bali alihisi kuwa yupo Aliyeanzisha uumbaji wa yote na kwamba Muumba Huyo Ndiye Anayestahiki kuabudiwa. Akawa anawaza na kutafuta uhakika hadi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamwongoza na kumchagua kumpa Unabii na Urasuli. Akaanza Ibraahiym (‘alayhis-salaam) kuwalingania watu wake katika Tawhiyd ya Allaah (Kumpwekesha), lakini watu wake hawakumuamini bali walimkanusha na wakajaribu kutaka kumwangamiza kwa kumtia katika moto waliouasha kwa kuni nyingi, lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Alimuokoa mbele ya macho yao. Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamjaalia kupata watoto wawili ambao ni Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) na Is-haaq (‘alayhis-salaam) ambao Manabii wote waliobakia, wametokana nao kama ifuatavyo:   

Is-haaq (‘alayhis-salaam) alimzaa Ya'quub ambaye ndiye aliyejaaliwa kutoa kizazi cha Manabii wote waliobakia hadi Nabii 'Iysa (‘alayhis-salaam). Baada ya hapo ikapita miaka takriban mia sita bila ya kutokea Nabii yeyote yule mpaka tena akazaliwa Nabii Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ametokana na kizazi cha Nabii Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) aliyeachwa Makkah na baba yake Nabii Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akiwa pamoja na mama yake Haajar. 

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) na mwanamwe Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) ndio waliojenga Al-Ka'bah Makkah, mji mtukufu kabisa  ambao  Waislamu wote  wanafika kutimiza Hajj.

Fadhila Na Sifa Za Nabii Ibraahiym (‘Alayhis-salaam)

Fadhila na Sifa za Nabii Ibraahiym (‘alayhis-salaam) ni nyingi mno kutokana na mafundisho tunayopata katika Qur-aan na Hadiyth, na katika Qur-aan ametajwa mara nyingi katika Suwrah kadhaa na katika Hadiyth mbalimbali. Miongoni mwazo ni zifuatazo:   

Miongoni Mwa Fadhila Za Nabii Ibraahiym (عليه السّلام):

(i) Allaah (سبحانه وتعالى) Amemteua yeye Nabii Ibraahiym na mwanawe Nabii Ismaa’iyl (عليهما السّلام) waijenge Al-Ka’bah. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akamteua Nabii Ibraahiym (عليه السّلام) awatangazie watu kwenda kutekeleza Hajj. Hivyo basi, akawa yeye (عليه السّلام)  na ahli wake ni mwongozo kwa watu katika utekelezaji wa manaasik (ibaada na taratibu) za Hajj na ‘Umrah. Rejea Al-Hajj (22:26-37). Na miongoni mwa manaasik hizo, ni kuswali katika Maqaam Ibraahiym baada ya kutufu Al-Ka’bah. Rejea Al-Baqarah (2:125). Pia, kusai baina ya  Swafaa na Marwah, rejea Al-Baqarah (2:158)  kama ni kigezo cha mkewe Haajar alipokuwa akihangaika kumtafutia maji mwanawe Ismaa’iyl (عليه السّلام). Na huko ndiko palipotokea mbubujiko wa maji ya Zamzam  ambayo watu wanakunywa kwa niya tofauti kama alivyogusia hilo Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Pia kuchinja mnyama baada ya yeye kupewa mtihani au majaribio makubwa, pindi alipoona njozini kuwa anamchinja mwanawe, naye kutokana na utiifu wake, akataka kutekeleza njozi hiyo akiamini kuwa ni Amri ya Allaah (سبحانه وتعالى). Lakini kumbe ilikuwa ni mtihani na jaribio, hivyo akafaulu katika hili, na hapo Allaah (سبحانه وتعالى) Akambadilishia kwa kumteremshia kondoo  kutoka mbinguni ili amchinje badala ya mwanawe.  Rejea Asw-Swaaffaat (37:101-107). Pia kutupia vijiwe Jamaraat ambayo ni katika waajibaat za Hajji na Sunnah zake nyenginezo.

(ii) Ni kipenzi cha Allaah. Rejea An-Nisaa (4:125).

(iii) Ameitwa Baba wa Manabii:  Kama ilivyokuwa hali ya  Nabii Nuwh (عليه السّلام): Al-‘Ankabuwt (29:27). Na katika Al-Hadiyd (57:26), ametajwa yeye Nabii Ibraahiym (عليه السّلام) pekee kuwa amejaaliwa kuwa na Unabii na kupewa Kitabu.

Imaam Ibn Kathiyr amesema kuhusu Aayah ya Suwrah Al-‘Ankabuwt: “Hii ni fadhila na baraka kubwa sana. Sio tu kwamba Allaah Alimfanya (Nabii Ibraahiym) kuwa ni kipenzi Chake na kumfanya Imaam wa watu, bali pia Alijaalia Unabii na Kitabu kuwa katika dhuriya zake. Baada ya zama za Ibraahiym, hapakuwa na Nabii ambaye hakutokana na kizazi chake. Manabii wote wa Wana wa Israaiyl (Ya’quwb) walikuwa katika kizazi chake, kuanzia Ya’quwb bin Is-haaq bin Ibraahiym hadi wa mwisho wao, `Iysa bin Maryam, ambaye alisimama kuwatangazia kaumu yake, bishara ya kuja kwa Nabii Mwarabu, Al-Qurashiy, Al-Haashimiy, Nabii wa mwisho wa Manabii wote, bwana wa wana wa Aadam katika dunia hii na Aakhirah, ambaye Allaah Alimteua kutoka kwa Waarabu safi wa asili  kutoka kwa kizazi  cha Ismaa’iyl bin Ibraahiym (عليهما السلام).  Hakuna Nabii yeyote katika ukoo wa Ismaa’iyl isipokuwa yeye Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم). [Tafsiyr Ibn Kathiyr] 

(iv) Ameomba duaa  kizazi chake kitoe Nabii wa mwisho; Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) baada ya kujenga Al-Ka’bah. Rejea (2:129).

(v) Ibraahiym (عليه السّلام)  ni Imaam wa Tawhiyd:

Allaah (سبحانه وتعالى) Amemfanya kuwa ni Imaam wa watu wa kufuatwa katika Tawhiyd. Rejea Al-Baqarah (2:124). Na pia Ummah umeusiwa kufuata mila yake. Rejea Al-Baqarah (2:135), Aal-‘Imraan (3:95), An-Nisaa (4:125), Al-An’aam (6:161), na An-Nahl (16:123). Na pia, Amewausia wanawe na kizazi chake Uislamu. Rejea Al-Baqarah (2:130-132). Na pia Amefanya neno la Tawhiyd (laa ilaaha illa-Allaah) lenye kubakia katika kizazi chake. Rejea Az-Zukhruf (43:28). Ingawa Rusuli wengineo wote wamekuja pia katika kulingania Tawhiyd, ila Nabii Ibraahiym (عليه السّلام)  amekuwa ni makhsusi kwa Tawhiyd. Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (رحمه الله)  amesema alipoulizwa:

Kwa nini Nabii Ibraahiym (عليه السّلام) amehusishwa zaidi na Tawhiyd, ilhali Manabii wote wengineo wamelingania Tawhiyd?

Akajibu:  Manabii wote wamekuja na (kulingania) Tawhiyd. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ ﴿٢٥﴾

“Na Hatukutuma kabla yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Rasuli yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: Hakika hapana mwabudiwa wa haki ila Mimi, basi Niabuduni.” [Al-Anbiyaa (21:25)]

Lakini Ibraahiym ni baba wa Waarabu, na baba wa Waisrael, naye amelingania Tawhiyd khalisi, na Mayahudi na Manaswara wamedai kuwa ni wafuasi wake, na Waislamu ndio wafuasi wake. Kwa hiyo yeye (عليه السّلام) akahusishwa kuwa ni baba wa Manabii, na kwamba yeye ndiye mwenye Haniyfiyyah (sifa ya kuelemea haki na kujiweka kando na shirki). Na sisi tumeamrishwa kumfuata, kwa sababu sisi ndio tulio karibu zaidi Ibraahiym kama Anavyosema Allaah (عزّ وجلّ):

إِنَّ أَوْلَى النَّاسِ بِإِبْرَاهِيمَ لَلَّذِينَ اتَّبَعُوهُ وَهَـٰذَا النَّبِيُّ وَالَّذِينَ آمَنُوا ۗ وَاللَّـهُ وَلِيُّ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٦٨﴾

“Hakika watu walio karibu zaidi kwa Ibraahiym ni wale waliomfuata na huyu Nabii (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) na wale walioamini. Na Allaah Ni Mlinzi wa Waumini.” [Aal-‘Imraan (3:68)]

Na Akasema kuwaradi Mayahudi na Manaswaara:

مَا كَانَ إِبْرَاهِيمُ يَهُودِيًّا وَلَا نَصْرَانِيًّا وَلَـٰكِن كَانَ حَنِيفًا مُّسْلِمًا وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿٦٧﴾

“Ibraahiym hakuwa Yahudi wala Naswara, lakini alikuwa mwenye kujiengua na upotofu akaelemea Dini ya haki, Muislamu na hakuwa miongoni mwa washirikina.” [Aal-‘Imraan (3:67)]

 [Liqaa-a Al-Baab Al-Maftuwh Swali namba (7/189).  

(vi) Anatajwa katika kila Swalaah, kwenye Tashahhud, kwa Swalaah inayojulikana kama Swalaatul-Ibraahiymiyyah.

Na fadhila hii tukufu ni kutokana na sababu zilizotangulia kutajwa juu na Imaam Ibn ‘Uthaymiyn.  Pia kutokana na sababu zifuatazo kama walivyosema ‘Ulamaa: Kwamba (عليه السّلام) Ibraahiym  ni babu (kizazi kilichoanzia kwa Ismaaiyl) wa Nabii Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم).  Na ‘Allaamah Badr Ad-Diyn Al-Hanafiy (رحمه الله) ana maelezo mengineyo katika kubainisha sababu ya hili. Amesema: “Ikiwa mtu atauliza: Kwa nini Ibraahiym (عليه السّلام)  ameteuliwa yeye pekee kutajwa katika Swalaah badala ya Manabii wengine (عليهم السّلام)?

Nitajibu: Kwa sababu Nabii (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwaona katika usiku wa Mi’iraaj, Manabii na Rusuli wote, na akamtolea Salaam kila Nabii, na hakuna hata mmoja wao aliyesalimia ummah wake isipokuwa Ibraahiym (عليه السّلام) . Hivyo basi, Nabii (صلى الله عليه وآله وسلم) ametuamrisha tumswalie kila mwisho wa Swalaah mpaka Siku ya Qiyaamah, kama malipo ya wema wake. Na imesemwa: Ibraahiym (عليه السّلام)   alipomaliza kuijenga Al-Ka’bah, aliuombea Ummah wa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم)  akisema:  Ee Allaah! Atakayehiji Nyumba hii miongoni mwa Ummah wa Muhammad, basi Mpe amani kutoka kwangu. Pia akawaombea ahli zake na watoto wake kwa duaa hii. Hivyo basi tukaamrishwa tuwakumbuke katika Swalaah kama malipo ya wema wao.” Mwisho. Ufafanuzi wa Sunan Abi Daawuwd cha Al-‘Ayniy (4/260). Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

(vii) Kizazi chake kimepewa ufalme mkubwa: An-Nisaa (4:54). 

(viii) Nabii (صلى الله عليه وآله وسلم) alimkuta mbingu ya saba  akielemea Bayt Al-Ma’muwr inayozungukwa na Malaika elfu sabiini.  (Haya yapo katika Hadiyth ndefu iliyopokelewa na Imaam Muslim katika Kitaab Al-Iymaan,  na wengineo). 

(ix) Alijaaliwa Ar-Rushd (Uongofu) na Allaah (سبحانه وتعالى)  Alimjua vyema: Al-Anbiyaa (21:51).

(x) Ni Nabii ambaye amemshabihi Nabii Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم): Hadiyth ya Abu Hurayrah (رضي الله عنه)  [Al-Bukhaariy, Muslim]

(xi) Ni miongoni mwa Rusuli watano wa Ulul-‘Azmi: Al-Ahzaab (33:7).

(xii) Amewaombea Waislamu wawe wenye kuelekeza nyoyo zao kuipenda Makkah na Al-Ka’bah. Ibraahiym (14:37).

(xiii) Amewaombea duaa kizazi chake wasimamishe Swalaah, na Amewaombea Waumini maghfirah Siku ya Hesabu. Ibraahiym (14:40-41).

(xiv) Atakuwa wa kwanza kuvalishwa nguo baada ya kufufuliwa kutokana na vile washirikina katika kaumu yake  walivyomuingiza motoni akiwa  uchi   baada ya kuvunja masanamu yao. Yapo haya kwenye Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما):

Nabii (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Enyi watu, hakika mtafufuliwa na Allaah hali ya kuwa hamna viatu, mpo uchi na bila kutahiriwa  (na magovi). ”Kisha akasoma: 

كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ ۚ

“Kama Tulivyoanza umbo la awali Tutalirudisha tena.” [Al-Anbiyaa (21:104)]

Tanabahini! Hakika mtu wa kwanza atakayevishwa nguo ni Nabii Ibraahiym (عليه السّلام).   [Al-Bukhaariy na Muslim]

Na ‘Ulamaa wameeleza pia kuwa sababu ya kutangulizwa Ibraahiym kuvishwa nguo Siku ya Qiyaamah kabla ya wengine ni kuwa hapakuweko miongoni mwa watu wa mwanzo na wa baadae, waliomkhofu zaidi Allaah kuliko yeye. Hivyo basi, nguo zitamharakia ili kumhifadhi, na moyo wake upate kutulia.

Na sababu nyingine -kama ilivyoeleza Hadiyth- ni kuwa, inawezekana kwamba yeye alikuwa ni wa kwanza kuvaa suruali wakati anaposwali ili kupata sitara ya ziada isiyo na shaka na kulinda tupu yake isigusane na sehemu yake ya kuswalia, naye akafanya kama alivyoamrishwa, na akalipwa hilo kuwa wa kwanza kusitiriwa Siku ya Qiyaamah.

Kadhalika, inawezekana kuwa wale waliomtupa motoni, walimwacha uchi na wakamvua nguo zote mbele ya watu kama anavyofanywa mtu anayetekelezewa adhabu ya kifo. Hivyo atalipwa nguo zake Siku ya Qiyaamah, na atakuwa mtu wa kwanza kuvaa mbele ya halaiki, na haya ni malipo mazuri zaidi. [Al-Qurtwubiy katika At-Tadhkirah]

(xv) Nabii (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema kwamba yeye ni kiumbe bora kabisa:  Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه):  Alikuja mtu mmoja kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwambia: “Ee kiumbe bora kabisa!”  Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamjibu: “Huyo ni Ibraahiym (عليه السّلام). [Muslim]

Sifa Za Nabii Ibraahiym (عليه السّلام):

(i) Hakuwa mshirikina kabisa. Ametajwa kwa sifa hii katika Suwrah kadhaa kwenye Qur-aan ikiwemo Suwrah hii An-Nahl (16:120). Pia, kisa chake katika Al-An’aam (6:74-81) cha kutokuabudu nyota wala mwezi wala jua kinathibitisha sifa hii. Kadhalika, alimuomba Allaah Amuepusha yeye na  wanawe wasiwe washirikina: Ibraahiym (14:35). Isitoshe, alimnasihi baba yake pia asiwe mshirikina lakini hakumsikiliza bali alimfukuzilia mbali: Maryam (19:41-48) na Ash-Shu’araa (26:69-89).

(ii) Alikuwa ni mtimizaji ahadi: An-Najm (53:37).

(iii) Ni mwenye huruma mno na mvumilivu: At-Tawbah (9:114).

(iv) Ni mvumilivu sana, mnyenyekevu mno kwa Allaah, na mwingi wa kurejea Kwake. Huwd (11:75).

(v) Mkarimu mno: Huwd (11:69), na Adh-Dhaariyaat (51:24-26).

(vi) Mwenye utukufu: Rejea Tanbihi namba 1 ya Aayah namba (4) katika Suwrah Yuwsuf.

(vii) Mnyeyekevu, kwani aliomba duaa baada ya kujenga Al-Ka’bah: Al-Baqarah (2:128). Al-Ka’bah ni Nyumba Tukufu kabisa katika Vitukufu vya Allaah katika Mji Mtukufu kabisa. Lakini juu ya utukufu huu, alikuwa na wasiwasi juu ya kutaqabaliwa kitendo hiki, kwa maana hakuwa na kibri kuwa madamu amejenga kitu kitukufu kabisa cha Allaah, basi awe amesifika au ni mtu bora kabisa.

(viii) Ana kisa muhimu cha uthibitisho wa Tawhiyd iliyojikita moyoni mwake wakati alipoingizwa motoni na watu wake kwa sababu aliyavunja masanamu waliyokuwa wakiyaabudu: Al-Anbiyaa (21:51-70),  na Asw-Swaaffaat (37:83-99)

(ix) Mwenye moyo uliosalimika: Asw-Swaaffaat (37:84).

(x) Swiddiyq (mkweli wa kidhati): Maryam (19:41).

(xi) Mwenye akhlaaq na mfano wa maadili mema: Al-Mumtahinah (60:4).

(xii) Amekhitariwa duniani, na Aakhirah ni miongoni mwa Swalihina: Al-Baqarah (2:130).

(xiii) Mwenye nguvu na busara: Swaad (38:45). Na katika busara zake, alimwambia mwanawe Ismaa’iyl abadilishe kizingiti chake badala ya kumwambia moja kwa moja “mwache mkeo.” Hii ni kutokana na malalamiko ya mke huyo kuhusu maisha yao na shida zao. Kisha akamtaka athibitishe kizingiti chake, akimaanisha aendeleze ndoa yake na mkewe mwengine (asimtaliki), mke wa pili ambaye hakulalamika shida zao za kimaisha. Maelezo ya hili yapo katika Hadiyth ndefu ya Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)  iliyopokelewa na Al-Bukhaariy, Kitaab Ahaadiyth Al-Anbiyaa.

Pia katika busara zake ni kumtaka mfalme Namruwd aliyejifanya kuwa yeye ni Mola na mwabudiwa, alichomoze jua kutoka Magharibi badala ya Mashariki, lakini mfalme huyo akabakia kinywa wazi ameduwaa. Rejea Al-Baqarah (2:258) kwenye maelezo bayana katika faida ya Aayah hiyo.

Pia katika busara yake nyengineyo ni vile alivyovunja masanamu kisha akatundika shoka ya sanamu lilokuwa kubwa lao. Kaumu yake walipomuuliza nani aliyevunja masanamu yetu, alijibu: “Waulizeni wakiwa wanaweza kunena!” Akikusudia pia kama kweli  wanastahiki kuabudiwa ikiwa hawawezi kujihami wenyewe kusingiziwa uvunjaji wa masanamu yao. Rejea Al-Anbiyaa (21:57-63), na Asw-Swaafaat (37:88-96)

(xiv) Alikhofia familia yake wasije kuabudu masanamu. Naye mwenyewe tokea utotoni alichukia ibaada ya shirki na masanamu. Na alikhiari Dini kuliko dunia, napo ni pale alipowaacha familia yake katika bonde la Makkah ambako hapakuwa na chochote, na alitaja sababu yake kuwa ili wasimamishe Swalaah: Ibraahiym (14:35-37).

Utoto Wake Na Da'wah Kwa Watu Wake:

Tokea utoto wake Ibraahiym (‘alayhis-salaam), alikuwa akiyachukia masanamu kwani alishangaa kuwa vipi wanaabudu masanamu wanayachonga wenyewe na ambayo hayakuweza kumdhuru au kumfaa chochote mtu? Ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema kuwa Alimjua vizuri na Akampa uongofu tokea mdogo:

وَلَقَدْ آتَيْنَا إِبْرَاهِيمَ رُشْدَهُ مِن قَبْلُ وَكُنَّا بِهِ عَالِمِينَ ﴿٥١﴾

Na kwa yakini Tulimpa Ibraahiym uongofu wake kabla, na Tulikuwa Wenye kumjua vizuri. [Al-Anbiyaa:51]

Akawa anajadiliana na watu wake ili awatoe kutoka katika upotofu: 

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ مَا هَـٰذِهِ التَّمَاثِيلُ الَّتِي أَنتُمْ لَهَا عَاكِفُونَ ﴿٥٢﴾

Alipomwambia baba yake na watu wake: Nini haya masanamu ambayo nyinyi mnayakalia kuyaabudu. [Al-Anbiyaa: 52]  

Lakini kila walivyokuwa wakiitwa katika Tawhyid, jibu lilikuwa wamekuta wazazi wao wanafanya hivyo. Lakini Ibraahiym (‘alayhis-salaam) hakuacha kuendelea kujadiliana nao:

 وَلَقَدْ آتَيْنَا إِبْرَاهِيمَ رُشْدَهُ مِن قَبْلُ وَكُنَّا بِهِ عَالِمِينَ ﴿٥١﴾

Na kwa yakini Tulimpa Ibraahiym uongofu wake kabla, na Tulikuwa Wenye kumjua vizuri.

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ مَا هَـٰذِهِ التَّمَاثِيلُ الَّتِي أَنتُمْ لَهَا عَاكِفُونَ ﴿٥٢﴾

Alipomwambia baba yake na watu wake: Nini haya masanamu ambayo nyinyi mnayakalia kuyaabudu?

قَالُوا وَجَدْنَا آبَاءَنَا لَهَا عَابِدِينَ ﴿٥٣﴾

Wakasema: Tumewakuta baba zetu wakiyaabudu.

قَالَ لَقَدْ كُنتُمْ أَنتُمْ وَآبَاؤُكُمْ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٥٤﴾

Akasema: Kwa yakini mmekuwa nyinyi na baba zenu katika upotofu bayana.

قَالُوا أَجِئْتَنَا بِالْحَقِّ أَمْ أَنتَ مِنَ اللَّاعِبِينَ ﴿٥٥﴾

Wakasema: Je, umetujia kwa haki, au wewe ni miongoni mwa wafanyao mchezo?

قَالَ بَل رَّبُّكُمْ رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الَّذِي فَطَرَهُنَّ وَأَنَا عَلَىٰ ذَٰلِكُم مِّنَ الشَّاهِدِينَ ﴿٥٦﴾

Akasema: Bali Rabb wenu ni Rabb wa mbingu na ardhi, Ambaye Amezianzisha, nami ni katika wenye kushuhudia hayo. 

 [Al-Anbiyaa: 51-56]  

Akaendelea kuwalingania kwa kuwauliza vipi wanaabudu vitu visivyoona au kusikia wala kuwafaa au kuwadhuru? Na majibu yao yakawa ni hayo hayo tu:

وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ إِبْرَاهِيمَ ﴿٦٩﴾

Na wasomee (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) khabari za Ibraahiym.

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ مَا تَعْبُدُونَ ﴿٧٠﴾

Alipomwambia baba yake na watu wake: Mnaabudu nini?

قَالُوا نَعْبُدُ أَصْنَامًا فَنَظَلُّ لَهَا عَاكِفِينَ ﴿٧١﴾

Wakasema: Tunaabudu masanamu, na tutaendelea kuyakalia kwa kuyaabudu.

قَالَ هَلْ يَسْمَعُونَكُمْ إِذْ تَدْعُونَ ﴿٧٢﴾

Akasema: Je, yanakusikieni mnapoyaomba?

أَوْ يَنفَعُونَكُمْ أَوْ يَضُرُّونَ ﴿٧٣﴾

Au yanakunufaisheni au yanakudhuruni?

قَالُوا بَلْ وَجَدْنَا آبَاءَنَا كَذَٰلِكَ يَفْعَلُونَ ﴿٧٤﴾

Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo.

قَالَ أَفَرَأَيْتُم مَّا كُنتُمْ تَعْبُدُونَ ﴿٧٥﴾

Akasema: Je, mnaona hivyo mlivyokuwa mkiviabudu?

أَنتُمْ وَآبَاؤُكُمُ الْأَقْدَمُونَ ﴿٧٦﴾

Nyinyi na baba zenu waliotangulia?

 [Ash-Shu'araa: 69-76] 

Tawhiyd Inamdhihirikia Nabii Ibraahiym (‘Alayhis-salaam)

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) aliendelea kuhojiana na watu wake kuhusu ibaada zao za kuabudu masanamu, waliodai kuwa wanawakurubisha kwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), ilhali Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hahitaji kuombwa kwa kupitia mtu au kitu chochote, bali linalopasa ni kumuomba Yeye moja kwa moja bila ya kuweko yeyote kati Yake.

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akawa anawaza vitu wanavyoabudu zaidi ya masanamu, kama vile nyota, jua na mwezi. Ikawa haimuingiia akilini kabisa kuwa vitu hivyo vinapasa kuabudiwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akataka kumdhihirishia hayo. Ikawa kila usiku na mchana unapoingia, Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alikuwa anatoka na kuangaza mbinguni. Akatafakari na akatambua kuwa vyote hivyo ni vitu vyenye kutoweka na kwamba Yuko Muumba wa vitu hivyo Anayestahiki kuabudiwa kwa haki. Yametajwa hayo katika Kauli za Allaah (Subhaanahuu wa Ta’aalaa):

 وَكَذَٰلِكَ نُرِي إِبْرَاهِيمَ مَلَكُوتَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلِيَكُونَ مِنَ الْمُوقِنِينَ ﴿٧٥﴾

Na hivyo ndivyo Tunavyomwonyesha Ibraahiym ufalme mkubwa wa mbingu na ardhi na ili awe miongoni mwa wenye yakini.

فَلَمَّا جَنَّ عَلَيْهِ اللَّيْلُ رَأَىٰ كَوْكَبًا ۖ قَالَ هَـٰذَا رَبِّي ۖ فَلَمَّا أَفَلَ قَالَ لَا أُحِبُّ

Na ulipomwingilia usiku akaona nyota. Akasema: Huyu ni Rabb wangu. Ilipotoweka akasema: Hakika mimi sipendi wanaotoweka. 

فَلَمَّا رَأَى الْقَمَرَ بَازِغًا قَالَ هَـٰذَا رَبِّي ۖ فَلَمَّا أَفَلَ قَالَ لَئِن لَّمْ يَهْدِنِي رَبِّي لَأَكُونَنَّ مِنَ الْقَوْمِ الضَّالِّينَ ﴿٧٧﴾

Kisha alipoona mwezi umechomoza akasema: Huyu ni Rabb wangu. Ulipotoweka akasema: Asiponiongoza Rabb wangu bila shaka nitakuwa miongoni mwa watu waliopotea.

فَلَمَّا رَأَى الشَّمْسَ بَازِغَةً قَالَ هَـٰذَا رَبِّي هَـٰذَا أَكْبَرُ ۖ فَلَمَّا أَفَلَتْ قَالَ يَا قَوْمِ إِنِّي بَرِيءٌ مِّمَّا تُشْرِكُونَ ﴿٧٨﴾

Kisha alipoliona jua limechomoza akasema: Huyu ni Rabb wangu, huyu ni mkubwa zaidi. Lilipotoweka akasema: Enyi watu wangu! Hakika mimi simo katika yale mnayoyashirikisha (na Allaah). [Al-An'aam: 75-78]

Akahojiana na watu wake:

إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِي فَطَرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ حَنِيفًا ۖ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿٧٩﴾

Hakika mimi nimeelekeza uso wangu kwa Ambaye Ameanzisha mbingu na ardhi, nikijitenga na itikadi potofu na kuelemea haki, nami si katika washirikina.

وَحَاجَّهُ قَوْمُهُ ۚ قَالَ أَتُحَاجُّونِّي فِي اللَّـهِ وَقَدْ هَدَانِ ۚ وَلَا أَخَافُ مَا تُشْرِكُونَ بِهِ إِلَّا أَن يَشَاءَ رَبِّي شَيْئًا ۗ وَسِعَ رَبِّي كُلَّ شَيْءٍ عِلْمًا ۗ أَفَلَا تَتَذَكَّرُونَ ﴿٨٠﴾

Na watu wake wakamhoji. Akasema: Je, mnahojiana nami kuhusu Allaah na hali Amenihidi?  Na wala sikhofu hayo mnayomshirikisha Naye (kwani sitodhurika) isipokuwa Rabb wangu Akitaka jambo. Rabb wangu Amezunguka kila kitu (kwa Ujuzi).  Je, basi hamkumbuki?

وَكَيْفَ أَخَافُ مَا أَشْرَكْتُمْ وَلَا تَخَافُونَ أَنَّكُمْ أَشْرَكْتُم بِاللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ عَلَيْكُمْ سُلْطَانًا ۚ فَأَيُّ الْفَرِيقَيْنِ أَحَقُّ بِالْأَمْنِ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٨١﴾

Na vipi nikhofu yale mnayoyashirikisha, nanyi hamkhofu kwamba mnamshirikisha Allaah na ambayo Hakuyateremshia kwenu hoja. Je, basi kundi gani kati ya mawili linastahiki zaidi kuwa katika amani kama nyinyi mnajua? [Al-An'aam: 79-81

Nabii Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akazidi kuwachukia washirikina wa kaumu yake na akathibitisha Tawhiyd yake kwa Allaah:

فَإِنَّهُمْ عَدُوٌّ لِّي إِلَّا رَبَّ الْعَالَمِينَ ﴿٧٧﴾

Basi hakika hao ni adui zangu isipokuwa Rabb wa walimwengu.

الَّذِي خَلَقَنِي فَهُوَ يَهْدِينِ ﴿٧٨﴾

Ambaye Ameniumba, Naye Ananiongoza.

وَالَّذِي هُوَ يُطْعِمُنِي وَيَسْقِينِ ﴿٧٩﴾

Na Ambaye Ndiye Anayenilisha na Ananinywesha.

وَإِذَا مَرِضْتُ فَهُوَ يَشْفِينِ ﴿٨٠﴾

Na ninapokuwa mgonjwa, basi Yeye Ananiponyesha.

وَالَّذِي يُمِيتُنِي ثُمَّ يُحْيِينِ ﴿٨١﴾

Na Ambaye Atanifisha kisha Atanihuisha.

وَالَّذِي أَطْمَعُ أَن يَغْفِرَ لِي خَطِيئَتِي يَوْمَ الدِّينِ ﴿٨٢﴾

Na Ambaye natumai Atanighufuria makosa yangu Siku ya Malipo.

[As-Shu'araa: 77-82]


Mjadala Baina Ya Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) Na Mfalme Kafiri Nimruwdh Bin Kuwsh:

Nimruwdh alikuwa mfalme na alitoka katika kizazi cha Nuwh (‘alayhis-salaam) Jina lake ni Nimruwdh bin Kanaan, bin Kuwsh, bin Saam bin Nuwh.   [Amenukuu Mujaahid - Tafsyir Ibn Kathiyr 2:35]. 

Mujaahid vile vile amesema: "Wafalme waliotawala pande za Mashariki na Magharibi za dunia walikuwa wanne, wawili walioamini; Sulaymaan bin Daawuud na Dhul-Qarnayn. Ama waliokuwa makafiri ni; Nimruwdh na Nebuchadnezzar" [At-Twabariy 5:433] Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni Mjuzi zaidi.

Mfalme huyo alikanusha kuweko kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), akajiona kuwa yeye ndiye anayepasa kuabudiwa.  Na kilichomfanya Nimruwd ajifanye ni muabudiwa ni kutokana na kibri yake kwa kuwa alitawala kwa muda mrefu. Na kibri hiyo ni kama ya Firawni.

Aliposikia kuwa Ibraahiym (‘alayhis-salaam) Anasema kuwa kuna Yuko Anayepasa kuabudiwa kwa haki, na Mwenye kumiliki nafsi za wanaadam na Mwenye Kuhuisha na Kufisha, akahojiana na Ibraahiym (‘alayhis-salaam):

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِي حَاجَّ إِبْرَاهِيمَ فِي رَبِّهِ أَنْ آتَاهُ اللَّـهُ الْمُلْكَ إِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّيَ الَّذِي يُحْيِي وَيُمِيتُ قَالَ أَنَا أُحْيِي وَأُمِيتُ ۖ قَالَ إِبْرَاهِيمُ فَإِنَّ اللَّـهَ يَأْتِي بِالشَّمْسِ مِنَ الْمَشْرِقِ فَأْتِ بِهَا مِنَ الْمَغْرِبِ فَبُهِتَ الَّذِي كَفَرَ ۗ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ ﴿٢٥٨﴾

Je, hukumzingatia yule ambaye alimuhoji Ibraahiym kuhusu Rabb wake kwa vile Allaah Alimpa ufalme aliposema Ibraahiym: Rabb wangu ni Yule Ambaye Anahuisha na Kufisha. Akasema: Mimi (pia) nahuisha na kufisha. Ibraahiym akasema: Hakika Allaah Analileta jua kutoka Mashariki basi wewe lilete kutoka Magharibi. Aliyekufuru akabaki kinywa wazi bila jibu, akataghayuri rangi. Na Allaah Haongoi watu madhalimu. [Al-Baqarah: 258]

Kudai kwa Nimruwdh kuwa yeye ana uwezo wa kuhuisha na kufisha, ni kumwachia huru mmoja kati ya watu waliohukumiwa kufa, na kumuua mwengine. [At-Twabariy (5:433-437), imepokelewa na Qataadah, Muhammad bin Is-haaq na As-Suddi]

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akamhoji kuwa, ikiwa yeye anadai ana uwezo huo wa kuhuisha na kufisha, basi na aonyesha uwezo wa wa kulichomoza jua kutoka Magharibi, kwani Muumba wa wanaadamu Analichomoza kutoka Mashariki, basi yeye ageuze mwenendo huo alifanye litokeze upande wa Magharibi.  Akapigwa na mshangao na hakuweza kujibu lolote bali alitahayarika.

Allaah Akamuangamiza Nimruwdh kwa mbu ambaye ni kiumbe dhaifu kabisa. Kisa chake kimesimuliwa katika Hadiyth za Israaiyliyyaat na hakuna kosa kusimulia ili tupate kupata mafunzo yake. Allaah   Alimfisha mfalme aliyejidai kuwa yeye ndiye anayepasa kuabudiwa, kwa kidudu dhalili na kidogo mno! [Hadiyth ya ‘Amr bin Al-Aasw (Radhwiya-Allaahu ‘anhu) ameipokea Al-Bukhaariy]  

Imaam Atw-Twabariy ameitoa katika Jaami’u Al-Bayaan (14/204) kutoka kwa Zayd bin Aslam kwamba: “Nimruwdh hakika alikuwa dhalimu wa kwanza duniani. Allaah Akampelekea mbu, wakaingia masikioni na puani mwake.  Alibaki kujipiga kichwa chake kwa nyundo kwa miaka mia nne! Watu waliokuwa na huruma zaidi walikuwa ni wale waliounganisha mikono wakawa wanampiga kichwani (kutuliza mbu).  Alijifanya jabari na alikuwa dhalimu kwa muda wa miaka mia nne, basi Allaah Akamuadhibu miaka mia nne sawa na muda wa utawala wake. Kisha Allaah Akamfisha.”

Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) Anamuomba Allaah Amuonyeshe Vipi Anahuisha Wafu:

‘Ulamaa wamesema kwamba kuna sababu ya ombi hili la Ibraahiym (‘alayhis-salaam) kutaka kuonyeshwa vipi Allaah (Subhanaahu wa Ta’aalaa) Anahuisha aliyekufa. Mfano Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alipomuambia Nimruwd:

  رَبِّيَ الَّذِي يُحْيِي وَيُمِيتُ  

Rabb wangu ni Yule Ambaye Anahuisha na Kufisha. [Al-Baqarah: 258]

Nabii Ibraahiym alitaka kuyanika na Uwezo wa Allaah wa Kuhuisha na Kufisha akamuomba Allaah Amwonyeshea vipi Anahuisha wafu. Na Hadiyth ya Nabii (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ifuatayo inasema kwamba sisi tuna uwezekano mkubwa zaidi wa kutia shaka kuliko Ibraahiym. Yeye Ibraahiym alimwomba Rabb wake amwonyeshe jinsi ya kuwahuisha wafu ili ashuhudie na atulize moyo wake:

عن أبي هريرة، رضي الله عنه، قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم  ((نحن أحق بالشك من إبراهيم، إذ قال: (رَبِّ أَرِنِي كَيْفَ تُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۖ قَالَ: أَوَلَمْ تُؤْمِن ۖ قَالَ بَلَىٰ وَلَـٰكِن لِّيَطْمَئِنَّ قَلْبِي ۖ ) البخاري

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya-Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Sisi tuna uwezekano mkubwa wa kuonyesha shaka kuliko Ibraahiym aliposema: 

رَبِّ أَرِنِي كَيْفَ تُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۖ قَالَ أَوَلَمْ تُؤْمِن ۖ قَالَ بَلَىٰ وَلَـٰكِن لِّيَطْمَئِنَّ قَلْبِي   

Rabb wangu! Nionyeshe vipi Unahuisha wafu? (Allaah) Akasema: Je, kwani huamini? Akasema: Sivyo hivyo! Bali Naam (naamini)! Lakini ili moyo wangu utumainike.

[Hadiyth ameipokea Imaam Al-Bukhaariy]  

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamtakabalia Ibraahiym (‘alayhis- salaam) ombi lake na Akamtaka achukue ndege wanne.  (‘Ulamaa wa Tasfiyr wamekhtilafiana kuhusu aina ya ndege waliotajwa kwani haikuelezwa ndege aina gani.)  Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamtaka Ibraahiym (‘alayhis-salaam) awazoeshe kwanza ndege kwake, kisha awakate vipande vipande. [Ibn 'Abbaas, Ikrimah, Sa'iyd bin Jubayr, Abu Maalik, Abu Al-Aswad, Ad-Dili, Wahb bin Munabbih, Al Hassan na As-Sudi kutoka Ibn Haatim (3:109), (1040)]

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akawazoesha kwake, kisha akawachinja na kuwatoa manyoa na kuwakata vipande vipande, kisha akavichanganya vipande hivyo pamoja.  Kisha akagawa vipande na kuviweka katika vilima vinne au saba.  Ibn 'Abbaas amesema, "Ibraahiym (‘alayhis- salaam) aliweka vichwa vya ndege hao katika mikono yake." Kisha akafanya kama Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Alivyomuamrisha kuwaita hao ndege kwake.  Akashuhudia kwa macho yake manyoya yao, damu na viungo vya kila ndege, vikiruka kujikusanya pamoja katika umbile lake, wakawa wanafika   mbele ya Ibraahiym (‘alayhis- salaam) wakitembea haraka kuelekea kwake. Ikawa kila ndege alikwenda kwa Ibraahiym (‘alayhis-salaam) kuchukua kichwa chake kutoka mikononi mwa Ibraahiym (‘alayhis-salaam), na alipojaribu kumpa ndege mmoja kichwa cha ndege mwengine, ndege alikataa kupokea na kujiunga. Subhana Allaah! Kwa hiyo kila kichwa cha ndege kilijunga na kiungo chake kile kile cha asili yake, kwa Uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). [Al-Qurtubi 3:300].

Allaah Alifanya hivyo ili Ibraahiym (‘alayhis-salaam) ashuhudie kwa dhahiri kuhuishwa kwa ndege hao na apate na kutuliza moyo wake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ أَرِنِي كَيْفَ تُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۖ قَالَ أَوَلَمْ تُؤْمِن ۖ قَالَ بَلَىٰ وَلَـٰكِن لِّيَطْمَئِنَّ قَلْبِي ۖ قَالَ فَخُذْ أَرْبَعَةً مِّنَ الطَّيْرِ فَصُرْهُنَّ إِلَيْكَ ثُمَّ اجْعَلْ عَلَىٰ كُلِّ جَبَلٍ مِّنْهُنَّ جُزْءًا ثُمَّ ادْعُهُنَّ يَأْتِينَكَ سَعْيًا ۚ وَاعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٢٦٠﴾ 

Na pindi aliposema Ibraahiym: Rabb wangu! Nionyeshe vipi Unahuisha wafu? (Allaah) Akasema: Je, kwani huamini? Akasema: Sivyo hivyo! Bali Naam (naamini)! Lakini ili moyo wangu utumainike. (Allaah) Akasema: Basi chukua ndege wanne wazoeshe kwako, (uwachinje), kisha weka juu ya kila jabali sehemu ya hao (ndege), kisha waite watakujia mbio (wakiumbika upya), na jua kwamba hakika Allaah Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Baqarah 2:260]

Da'wah Kwa Baba Yake: 

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alikuwa akiumia kupita kiasi kumuona baba yake (Au ‘ammi yake aliyemlea kama walivyonukuu baadhi ya Mufassiriyn) kuwa anaabudu masanamu. Bali akiumia zaidi kwani yeye huyo baba yake ndiye aliyekuwa akichonga hayo masanamu. Hii ni tabia ya mwenye kufanya da'wah anapoona jamaa zake wenyewe wako katika upotofu na khaswa inapokuwa jamaa aliye karibu zaidi kama baba, mama, ndugu, watoto na kadhalika. Kwa hiyo, lilikuwa tamanio lake kubwa kumtoa baba yake kutoka katika upotofu na kumuingiza katika Tawhiyd. Akamuita kwa maneno ya upole kabisa na kumpa kila hoja ili atambue upotofu huo:  

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ يَا أَبَتِ لِمَ تَعْبُدُ مَا لَا يَسْمَعُ وَلَا يُبْصِرُ وَلَا يُغْنِي عَنكَ شَيْئًا ﴿٤٢﴾ يَا أَبَتِ إِنِّي قَدْ جَاءَنِي مِنَ الْعِلْمِ مَا لَمْ يَأْتِكَ فَاتَّبِعْنِي أَهْدِكَ صِرَاطًا سَوِيًّا ﴿٤٣﴾ يَا أَبَتِ لَا تَعْبُدِ الشَّيْطَانَ ۖ إِنَّ الشَّيْطَانَ كَانَ لِلرَّحْمَـٰنِ عَصِيًّا ﴿٤٤﴾ يَا أَبَتِ إِنِّي أَخَافُ أَن يَمَسَّكَ عَذَابٌ مِّنَ الرَّحْمَـٰنِ فَتَكُونَ لِلشَّيْطَانِ وَلِيًّا ﴿٤٥﴾

42. Pindi alipomwambia baba yake: Ee baba yangu! Kwa nini unaabudu vile visivyosikia na visivyoona na visivyokufaa kitu chochote? 43. Ee baba yangu! Hakika mimi imekwishanijia elimu isiyokufikia wewe; basi nifuate nikuongoze njia iliyonyooka.  44. Ee baba yangu! Usimwabudu shaytwaan. Hakika shaytwaan daima ni mwenye kumuasi Ar-Rahmaan. 45. Ee baba yangu! Hakika mimi nakhofu isikushike adhabu kutoka kwa Ar-Rahmaan, ukaja kuwa rafiki kwa shaytwaan. [Maryam: 42-45]

Lakini baba yake Ibraahiym (‘alayhis- salaam) hakutaka kuacha ibada yake na hakupendezewa na wito wa mwanawe, na ingawa Ibraahiym (‘alayhis- salaam) alimuita kila mara kwa upole na adabu kabisa kama aya hizo za juu "Ee baba yangu", baba yake hakumjibu kwa upole wala hakuonyesha adabu baina ya baba na mtoto, bali alimtisha kuwa akiendelea kumwita katika ibada yake atamfukuza na kumpiga mawe kama ilivyotajwa katika Kauli Zake Allaah (‘Azza wa Jalla):

قَالَ أَرَاغِبٌ أَنتَ عَنْ آلِهَتِي يَا إِبْرَاهِيمُ ۖ لَئِن لَّمْ تَنتَهِ لَأَرْجُمَنَّكَ ۖ وَاهْجُرْنِي مَلِيًّا ﴿٤٦﴾

(Baba yake) Akasema: Unachukia waabudiwa wangu ee Ibraahiym? Usipokoma, bila shaka nitakupiga mawe; na niondokelee mbali kwa muda mrefu! [Maryam:46]

Hata hivyo Ibraahiym (‘alayhis-salaam) anatupa mafunzo makubwa hapa kuwa juu ya kwamba alimuita baba yake kwa upole na adabu kisha baba yake akamjibu kwa kumkemea, majibu ya Ibraahiym (‘alayhis-salaam) yalikuwa ni ya uzuri zaidi kwa kumtakia amani iwe juu yake na kumuombea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amghufurie. 

قَالَ سَلَامٌ عَلَيْكَ ۖ سَأَسْتَغْفِرُ لَكَ رَبِّي ۖ إِنَّهُ كَانَ بِي حَفِيًّا ﴿٤٧﴾وَأَعْتَزِلُكُمْ وَمَا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَأَدْعُو رَبِّي عَسَىٰ أَلَّا أَكُونَ بِدُعَاءِ رَبِّي شَقِيًّا ﴿٤٨﴾

 47. (Ibraahiym) Akasema: Salaamun ‘Alayka. (Amani iwe juu yako). Nitakuombea maghfirah kwa Rabb wangu. Hakika Yeye daima ni Mwenye kunihurumia sana.  48.  Na natengana nanyi na mnavyoviomba badala ya Allaah; na namuomba Rabb wangu asaa nisijekuwa mwenye kunyimwa du’aa yangu kwa kumwomba Rabb wangu. [Maryam:47- 48]

Baba Yake Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) Atageuzwa Kuwa Fisi Siku Ya Qiyaamah Na Kutupwa Motoni:

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alijiombea Du'aa mwenyewe na kumuombea baba yake:  

رَبِّ هَبْ لِي حُكْمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ ﴿٨٣﴾وَاجْعَل لِّي لِسَانَ صِدْقٍ فِي الْآخِرِينَ ﴿٨٤﴾وَاجْعَلْنِي مِن وَرَثَةِ جَنَّةِ النَّعِيمِ ﴿٨٥﴾وَاغْفِرْ لِأَبِي إِنَّهُ كَانَ مِنَ الضَّالِّينَ ﴿٨٦﴾وَلَا تُخْزِنِي يَوْمَ يُبْعَثُونَ ﴿٨٧﴾يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿٨٨﴾إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّـهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿٨٩﴾

83. Rabb wangu! Nitunukie hikmah; elimu ya Dini na Unikutanishe na Swalihina.  84. Na Nijaalie kusifika kwa heshima kwa vizazi watakaokuja baadaye.   85. Na Nijaalie miongoni mwa warithi wa Jannah ya neema.  86. Na Mghufurie baba yangu, hakika yeye amekuwa miongoni mwa waliopotea.  87. Na wala Usinihizi Siku watakayofufuliwa.  88. Siku hayatofaa mali wa watoto. 89. Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika. [Ash-Shu'araa: 83-89]

Tunaona kwamba katika Du'aa hizo Ibraahiym (‘alayhis-salaam) amemuombea baba yake maghfira kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

وَمَا كَانَ اسْتِغْفَارُ إِبْرَاهِيمَ لِأَبِيهِ إِلَّا عَن مَّوْعِدَةٍ وَعَدَهَا إِيَّاهُ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ أَنَّهُ عَدُوٌّ لِّلَّـهِ تَبَرَّأَ مِنْهُ ۚ إِنَّ إِبْرَاهِيمَ لَأَوَّاهٌ حَلِيمٌ ﴿١١٤﴾

Na haikuwa Ibraahiym kumuombea maghfirah baba yake isipokuwa kwa sababu ya ahadi aliyoahidiana naye. Lakini ilipombainikia kwamba yeye ni adui wa Allaah, alijiepusha naye. Hakika Ibraahiym ni mwenye huruma mno na mvumilivu. [At-Tawbah:114]

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: "Ibraahiym (‘alayhis-salaam) aliendelea kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amghufurie baba yake mpaka alipokufa. Baada ya hapo alipotambua kwamba baba yake amekufa akiwa ni adui ya Allaah, akajitenga naye".   [At-Twabariy 14.519]

Katika kauli ya

وَلَا تُخْزِنِي يَوْمَ يُبْعَثُونَ ﴿٨٧﴾

Na wala Usinihizi Siku watakayofufuliwa. [Ash-Shu'araa 87]

Imaam Al-Bukhaariy amesimulia Hadiyth ifuatayo:

عن أبي هريرة، رضي الله عنه، عن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((إن إبراهيم رأى أباه يوم القيامة عليه الغَبَرَةُ والقَتَرَةُ))  البخاري 4768

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasul wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “ Ibraahiym atamuona baba yake siku ya Qiyaamah akiwa amefunikwa na vumbi na kiza” [Al-Bukhaariy 4768].

Usimulizi mwingine kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

يلقى إبراهيم أباه، فيقول: يا رب، إنك وعدتني أنك لا تخزيني يوم يبعثون. فيقول الله: إني حرمت الجنة على الكافرين

Ibraahiym atakutana na baba yake na atasema: "Ee Rabb, Umeniahidi kwamba Hutonihizi siku watakaofufuliwa viumbe vyote". Allaah Atasema: "Nimeiharamisha Jannah (Pepo) kwa makafiri" [Fat-h Al-Baariy 8:357]

Usimulizi mwingine vile vile:

((يلقى إبراهيم أباه آزر يوم القيامة، وعلى وجه آزر قَتَرَةٌ وغَبَرة، فيقول له إبراهيم: ألم أقل لك: لا تعصني فيقول أبوه: فاليوم لا أعصيك. فيقول إبراهيم: يا رب، إنك وعدتني ألا تخزيني يوم يبعثون، فأي خزي أخزى من أبي الأبعد؟ فيقول الله تعالى: إني حرمت الجنة على الكافرين. ثم يُقال: يا إبراهيم، ما تحت رجليك؟ فينظر فإذا هو بذبح متلطخ، فيؤخذ بقوائمه فيلقى في النار)) البخاري

Ibraahiym atakutana na baba yake Aazar siku ya Qiyaamah na kutakuweko na vumbi na kiza usoni mwa Aazar. Ibraahiym atamuambia: "Sikukuambia kwamba usiniasi?". Baba yake atasema: "Leo sikuasi". Ibraahiym atasema: "Ee Rabb, Umeniahidi kwamba hutonihizi siku watakaofufuliwa, lakini hizaa gani itakuwa kubwa zaidi ya kumuona baba yangu katika hali hii?". Allaah Atamuambia: "Nimeharamisha Jannah (Pepo) kwa makafiri". Kisha itasemwa: "Ee Ibraahiym! Tazama chini ya miguu yako". Atatazama na ataona (kwamba baba yake amebadilishwa kuwa) fisi amefunikwa katika samadi/kinyesi, atachukuliwa kwa miguu yake na kutupwa motoni. [Al-Bukhaariy 3350 katika kunukuliwa na Fat-h Al-Baariy 6:445]

Kugeuzwa baba yake Ibraahiym (‘alayhis-salaam) kuwa fisi ni Rahma kutoka kwa Allaah ili Ibraahiym (‘alayhis-salaam) asimuone baba yake katika sura yake akiwa anatupwa motoni. 

Kuvunja Masanamu:

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatuambia kuhusu Khaliyl Wake Ibraahiym (‘alayhis-salaam) na vipi Alivyomjaalia uongofu tokea zamani yaani tokea udogoni mwake. Alimpa moyo kwa kumuonyesha haki na dalili dhidi ya watu wake kwa yale waliokuwa wakiabudu kama Anavyosema:

وَتِلْكَ حُجَّتُنَا آتَيْنَاهَا إِبْرَاهِيمَ عَلَىٰ قَوْمِهِ ۚ .. ﴿٨٣﴾

Na hiyo ndio hoja Yetu Tuliyompa Ibraahiym juu ya watu wake... [Al-An'aam:83]

Na kumpa uongofu tokea alipokuwa mdogo Anasema Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa 

وَلَقَدْ آتَيْنَا إِبْرَاهِيمَ رُشْدَهُ مِن قَبْلُ وَكُنَّا بِهِ عَالِمِينَ ﴿٥١﴾

Na kwa yakini Tulimpa Ibraahiym uongofu wake kabla, na Tulikuwa Wenye kumjua vizuri. [A-Anbiyaa:51]

Na ndio maana alipokuwa mdogo alikuwa anashangazwa na ibada yao ya masanamu, akiyaendea masanamu hayo kuyatazama na kuona jinsi walivyokuwa wapumbavu watu wake kuabudu mawe yaliyochongwa ambayo akiona kuwa hayawezi kuwafaa kitu wala kuwadhuru kitu.

Akaapa Ibraahiym (‘alayhis-salaam) kuwa atayavunja haya masanamu, na alipoapa kiapo hicho mmoja wa watu wake alimsikia. Walikuwa wana sikukuu ambayo walikuwa wakienda wote kusherehekea. Yeye akabakia, na walipomuuliza sababu ya kutokwenda aliwajibu kuwa anaumwa. 

فَنَظَرَ نَظْرَةً فِي النُّجُومِ ﴿٨٨﴾فَقَالَ إِنِّي سَقِيمٌ ﴿٨٩﴾ 

Akatazama mtazamo katika nyota. 89. Akasema: Hakika mimi ni mgonjwa. [As-Swaaffaat: 88-89]

Ilikuwa siku moja baada ya kuapa kuwa atayavunja masanamu.  Watu wake wakatoka kwenda kwenye sherehe zao, huku nyuma Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akayavunja masanamu yote isipokuwa sanamu kubwa kabisa, akachukua shoka alilotumia kuwavunjia na kuliweka katika mikono ya hilo sanamu kubwa ili watu wafikiri kuwa hilo sanamu ndilo lililovunja masanamu mingine. Akaanza kwa kuapa kuwa atayafanyia hila masanamu yao:

وَتَاللَّـهِ لَأَكِيدَنَّ أَصْنَامَكُم بَعْدَ أَن تُوَلُّوا مُدْبِرِينَ ﴿٥٧﴾فَجَعَلَهُمْ جُذَاذًا إِلَّا كَبِيرًا لَّهُمْ لَعَلَّهُمْ إِلَيْهِ يَرْجِعُونَ ﴿٥٨﴾ 

57. Na naapa kwa Allaah, bila shaka nitafanyia hila masanamu yenu baada ya mkishageuka kwenda zenu. 58. Basi akayavunja vipande vipande isipokuwa kubwa lao ili wapate kulirejea. [Al-Anbiyaa: 57-58]

Walikuwa wanawaekea chakula masanamu yao na alipokwenda kuyavunja masanamu Ibraahiym (‘alayhis-salaam) aliyasemesha na kuyauliza masanamu kwa kejeli:

فَتَوَلَّوْا عَنْهُ مُدْبِرِينَ ﴿٩٠﴾ فَرَاغَ إِلَىٰ آلِهَتِهِمْ فَقَالَ أَلَا تَأْكُلُونَ ﴿٩١﴾مَا لَكُمْ لَا تَنطِقُونَ ﴿٩٢﴾ فَرَاغَ عَلَيْهِمْ ضَرْبًا بِالْيَمِينِ ﴿٩٣﴾

90. Wakaachana naye wakimgeukilia mbali kwenda zao.   91. Akaenda kwa siri kwa waabudiwa wao; akasema: Mbona hamli?  92. Mna nini! Mbona hamsemi?

93. Akayakabili (masanamu) kwa siri akawapiga kwa mkono wa kulia. [As-Swaaffaat: 90-93]

Waliporudi wakapatwa na mshangao mkubwa kuona masanamu yao wanayoyaabudu yamevunjwa! 

 قَالُوا مَن فَعَلَ هَـٰذَا بِآلِهَتِنَا إِنَّهُ لَمِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٥٩﴾ قَالُوا سَمِعْنَا فَتًى يَذْكُرُهُمْ يُقَالُ لَهُ إِبْرَاهِيمُ ﴿٦٠﴾قَالُوا فَأْتُوا بِهِ عَلَىٰ أَعْيُنِ النَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَشْهَدُونَ ﴿٦١﴾قَالُوا أَأَنتَ فَعَلْتَ هَـٰذَا بِآلِهَتِنَا يَا إِبْرَاهِيمُ ﴿٦٢﴾قَالَ بَلْ فَعَلَهُ كَبِيرُهُمْ هَـٰذَا فَاسْأَلُوهُمْ إِن كَانُوا يَنطِقُونَ ﴿٦٣﴾

59. Wakasema: Nani amefanya hivi kwa waabudiwa wetu? Hakika yeye ni miongoni mwa madhalimu.  60. Wakasema: Tulimsikia kijana akiwataja anaitwa Ibraahiym.  61. Wakasema: Mleteni mbele ya macho ya watu ili wapate kushuhudia.  62. Wakasema: Je, ni wewe uliyefanya hivi kwa waabudiwa wetu, ee Ibraahiym?   63. Akasema: Hapana, bali amefanya hayo hili kubwa lao. Hivyo waulizeni wakiwa wanaweza kunena! [Al-Anbiyaa:59-63]

Wakajirudi kidogo kuwaza kwamba kweli walikuwa wanaabudu miungu isioweza hata kujikinga na madhara, lakini kuwaza kwao kulikuwa kwa muda mdogo, kisha wakarudi katika upotofu ule ule:

 فَرَجَعُوا إِلَىٰ أَنفُسِهِمْ فَقَالُوا إِنَّكُمْ أَنتُمُ الظَّالِمُونَ ﴿٦٤﴾ثُمَّ نُكِسُوا عَلَىٰ رُءُوسِهِمْ لَقَدْ عَلِمْتَ مَا هَـٰؤُلَاءِ يَنطِقُونَ ﴿٦٥﴾قَالَ أَفَتَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكُمْ شَيْئًا وَلَا يَضُرُّكُمْ ﴿٦٦﴾أُفٍّ لَّكُمْ وَلِمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ ۖ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿٦٧﴾

64.  Basi wakajirudia nafsi zao, wakasema: Hakika nyinyi ndio madhalimu.   65. Kisha wakarudia hali yao ya mwanzo ya upotofu: (Wakasema): Umekwishajua kwamba hawa hawasemi.   66. (Ibraahiym) Akasema: Je, basi mnaabudu badala ya Allaah isiyokunufaisheni kitu chochote na wala kukudhuruni?   67. Aibu yenu nyinyi na vile mnavyoviabudu badala ya Allaah. Je, hamtii akilini?  [Al-Anbiyaa: 64-67]

Hii ndio ilikuwa sababu khaswa ya Ibraahiym (‘alayhis-salaam) ya kuyavunja hayo masanamu ili wajiulize na watambue ujinga wao wa kuabudu vitu visivyosema na wala visivyoweza kujihifadhi na madhara.   

Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) Anaingizwa Katika Moto:

Hapo tena ndipo walipotaka kumchoma moto:

قَالُوا حَرِّقُوهُ وَانصُرُوا آلِهَتَكُمْ إِن كُنتُمْ فَاعِلِينَ ﴿٦٨﴾

Wakasema: Muunguzeni na mnusuru waabudiwa wenu, mkiwa ni wafanyao (kunusuru). [Al-Anbiyaa:68]

Wakakusanya kuni nyingi kabisa za kuandaa moto mkubwa.  Wakachimba shimo na ukawashwa moto uliowaka kwa cheche kubwa, moto ambao haujapata kuwashwa moto kama huo kabla wakamtia Ibraahiym (‘alayhis- salaam). 

Yafuatayao ni maelezo mbali mbali kuhusu tukio hilo:

-Bwana mmoja Mkurdi aliyekuwa ni mhamajihamaji, ambaye ametokea Persia, alitoa rai kuwa Ibraahiym (‘alayhis-salaam) atiwe katika manati kubwa (chombo cha kurushia mawe) [Al-Qurtwubiy 11:303] 

-Shu'ayb Al-Jabaa'i kasema: (Bwana huyo) "Jina lake alikuwa ni Hayzan na kwa sababu ya rai yake hiyo aliyotoa, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Kamjaalia kumezwa na ardhi na ataendelea kudidimia hadi siku ya Qiyaamah.

-Alipotumbukizwa Ibraahiym (‘alayhis-salaam) katika moto alisema:

حَسْبُنا اللَّه وَ نِعْم الْوَكِيل

Ananitosheleza Allaah na Yeye Ndiye Mbora wa kupanga mambo yangu [At-Twabariy 18:465]

-Inavyosemekana kuwa zilikusanywa kuni kwa muda wa mwezi na alipotupwa kwenye moto huo alikuja Jibriyl (‘alayhis-salaam) akasema: Ee Ibraahiym, una haja yoyote? Akajibu: Ama kwako la!

حَسْبِيَ اللَّه وَنِعْمَ الْوَكِيِل

Hasbiya-Allaah Wa Ni'mal-Wakiyl [Aysarut-Tafaasiyr – Abu-Bakkar Al-Jazaairiy 3:426]

-Kutokana na wingi wa kuni zilizokusanywa ilifika hadi watu kuweka nadhiri, ya kupeleka kuni. 

-As-Sudi kasema: "Mwanamke alipokuwa akiumwa akiweka nadhiri kuwa akipona ataleta kuni za kumuunguza Ibraahiym (‘alayhis-salaam). [Al-Qurtubiy 11:303]

-Kutokana na Hadiyth ifuatayo, baadhi ya Mufassiriyn wamesema kwamba fadhila hii ya kuwa Ibraahiym (‘alayhi-salaam) atakuwa ni mtu wa kwanza kuvishwa nguo, ni kwa sababu yakutiwa motoni bila ya sababu yoyote ya haki bali kwa kushikilia Tawhiyd na kukanusha shirk:   

عن ‏ ‏ابن عباس ‏ ‏رضي الله عنهما ‏ عن النبي ‏ ‏صلى   الله عليه وسلم ‏قال: ((إنكم محشورون  حفاة عراة غرلا ثم قرأ ((كما بدأنا أول خلق نعيده)) وأول من يكسى يوم القيامة  إبراهيم)) البخاري ومسلم

Imetoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

amesema: “Mtafufuliwa bila ya viatu, uchi nabila ya kutahiriwa (khitaan) kisha akasoma”: ((Kama Tulivyoanza umbo la awali tutalirudisha tena)) na wa kwanza kuvalishwa nguo siku ya Qiyaamah ni Ibraahiym)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

-Sa'iyd bin Jubayr karipoti kwamba Ibn 'Abbaas kasema:  "Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alipotupwa katika moto, Malaika wa mvua alisema: Lini nitaruhusiwa kuteremsha mvua?  Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Alijibu haraka kama aya inavyosema:

قُلْنَا يَا نَارُ كُونِي بَرْدًا وَسَلَامًا عَلَىٰ إِبْرَاهِيمَ ﴿٦٩﴾

Tukasema: Ee moto! Kuwa baridi, na salama juu ya Ibraahiym! [Al-Anbiyaa: 69]

-Na kwa maneno hayo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) hakuna moto uliokuwa ukiwaka duniani wakati huo ila ulizimwa [At-Twabariy 18:466]

-Ibn 'Abbaas na Abu Al-Aliyah kasema: "Ingelikuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hakusema (Hakuuambia moto): 

.. وَسَلَامًا …﴿٦٩﴾

Na salama

Basi Ibraahiym (‘alayhis-salaam) angelidhurika kwa ubaridi wake [At-Twabariy 18:466, 465]

-Qataadah amesema: "Siku hiyo hakikuweko kiumbe kisichojaribu kuuzima moto wa Ibraahiym (‘alayhi wa sallam) ila mjusi" [At-Twabariy 18:467].

-Az-Zuhriy kasema: "Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamrisha kuwa (mjusi) auliwe na akaitwa 'mnyama mharibifu' [At-Twabariy 18:467 na pia imesimuliwa katika Muslim Namba 2238]

Mbinu zao za kutaka kumuunguza Ibraahiym (‘alayhis-salaam) katika moto hazikufaulu kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

وَأَرَادُوا بِهِ كَيْدًا فَجَعَلْنَاهُمُ الْأَخْسَرِينَ ﴿٧٠﴾

Na wakamkusudia njama; lakini Tukawajaalia wao ndio wenye kukhasirika.  [Al-Anbiyaa:70]

Moto ukamalizika kuwaka, watu wakiwa wanasubiri kwa hamu kubwa waone majivu tu, lakini dhana yao iliwashtua, na walitahayarika walipomuona Ibraahiym (‘alayhis-salaam) anatoka salama mbele ya macho yao akitembea mzima bila ya kudhurika popote.  Ni muujiza mkubwa hakika!

Lakini kama kawaida ya hali ya watu wa zamani walivyokuwa na ukaidi wao hawakumuamini Ibraahiym (‘alayhis-salaam) na wito wake wa ibada ya Tawhiyd kwamba kuna Ilaah Apasaye kuabudiwa Pekee, Ambaye Alifanya maajabu haya ya Moto kutokumuunguza Ibraahiym (‘alayhis- salaam).

Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) Anahama Iraq Kuelekea Shaam:

Hakuamini mtu isipokuwa Luutw (‘alayhis-salaam) ambaye alikuwa ni binamu (cousin) wake, na mke wake Saarah.  

فَآمَنَ لَهُ لُوطٌ ۘ وَقَالَ إِنِّي مُهَاجِرٌ إِلَىٰ رَبِّي ۖ إِنَّهُ هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢٦﴾

 Basi Luutw akamwamini; na (Ibraahiym) akasema: Hakika mimi nahajiri kwa Rabb wangu; hakika Yeye Ndiye Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [Al'Ankabuut: 26

Vile vile akasema Ibraahiym (‘alayhis-salaam):

وَقَالَ إِنِّي ذَاهِبٌ إِلَىٰ رَبِّي سَيَهْدِينِ ﴿٩٩﴾رَبِّ هَبْ لِي مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿١٠٠﴾

99. Akasema: Hakika mimi ni mwenye kwenda kwa Rabb wangu Ataniongoza. 100. Rabb wangu!  Nitunukie miongoni mwa Swalihina. [As-Swaaffaat: 99-100]

Hapo tena Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamhamisha na kumpeleka Shaam nchi ambayo ndio iliyokusudiwa kuwa 'nchi Tulioibariki'.

وَنَجَّيْنَاهُ وَلُوطًا إِلَى الْأَرْضِ الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا لِلْعَالَمِينَ ﴿٧١﴾

Na Tukamuokoa na Luutw kuelekea ardhi ambayo Tumeibariki humo kwa walimwengu. [Al-Anbiyaa:71]

Na kutokana na Du'aa yake hiyo ya:

رَبِّ هَبْ لِي مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿١٠٠﴾

Rabb wangu!  Nitunukie miongoni mwa Swalihin. [As-Swaaffaat:100]

Allaah (Subhaanahu Allaahu wa Ta’aalaa) Akamjaaliya kupata watoto kama aya zifuatazo zinavyotuelezea:

فَبَشَّرْنَاهُ بِغُلَامٍ حَلِيمٍ ﴿١٠١﴾

Basi Tukambashiria ghulamu mvumilivu. [As-Swaaffaat:101] 

Aayah hii imekusudiwa ni Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam)

Na katika Aayah nyingine Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)

وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ نَافِلَةً ۖ وَكُلًّا جَعَلْنَا صَالِحِينَ ﴿٧٢﴾

Na Tukamtunukia Is-haaq na (mjukuu) Ya’quwb kuwa ni ziada. Na wote Tumewajaalia kuwa Swalihina. [Al-Anbiyaa:72]

'Atwaa' na Mujaahid wamesema:  "Naafilatan (Na ziada) ina maana kwamba zawadi" [At-Twabariy 18:471]

Ibn 'Abbaas na Qataadah wamesema: "Zawadi ya mtoto mwenye mtoto, maana kwamba Ya'quwb alikuwa mtoto wa Is-haaq kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)

.. فَبَشَّرْنَاهَا بِإِسْحَاقَ وَمِن وَرَاءِ إِسْحَاقَ يَعْقُوبَ﴿٧١﴾

..Tukambashiria Is-haaq na baada ya Is-haaq ni Ya’quwb. [Huwd:71]

 KUHAMA IRAQ

((وَنَجَّيْنَاهُ وَلُوطًا إِلَى الْأَرْضِ الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا لِلْعَالَمِينَ))

((Na Tukamwokoa yeye na Luutw Tukawapeleka kwenye nchi Tuliyoibariki kwa ajili ya walimwengu wote)) [Al-Anbiyaa:71]

Ibraahiym عليه السلام aliondoka Iraq pamoja na Luutw عليه السلام na wakaelekea kwanza katika mji unaoitwa 'Aur, kisha Haraan, kisha tena Falastina (Palestine).

ALIVYOMPATA HAAJAR

Akaelekea Misri   na wakati wote alipokuwa safarini  ilikuwa hima yake ni kuwaita watu katika Tawhiyd, kuwaongoza katika haki na katika mambo mema. Alipokuwa anaelekea Misri alipita mji wa dhalimu mmoja akapiga kambi hapo. Matukio yote hapo yameelezwa katika Hadiyth Sahiyh ifuatayo:

  عن أبي هريرة رضي الله عنه؛ أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((إن إبراهيم، عليه السلام، لم يكذب غير ثلاث: ثنتين في ذات الله ، قوله: ( بَلْ فَعَلَهُ كَبِيرُهُمْ هَذَا ) وقوله (إِنِّي سَقِيمٌ ) قال: "وبينا هو يسير في أرض جبار من الجبابرة ومعه  سارة، إذ نـزل منـزلا فأتى الجبار رجل، فقال: إنه قد نـزل بأرضك رجل معه امرأة أحسن الناس، فأرسل إليه فجاء، فقال: ما هذه المرأة منك؟ قال: هي أختي. قال: فاذهب فأرسل بها إليّ، فانطلق إلى سارة فقال: إن هذا الجبار سألني عنك فأخبرته أنك أختي فلا تكذبيني عنده، فإنك أختي في كتاب الله، وأنه ليس في الأرض مسلم غيري وغيرك، فانطلق بها إبراهيم ثم قام يصلي. فلما أن دخلت عليه فرآها أهوى إليها، فتناولها، فأخذ أخذًا شديدًا، فقال: ادعي الله لي ولا أضرك، فدعت له فأرسل، فأهوى إليها، فتناولها فأخذ بمثلها أو أشد. ففعل ذلك الثالثة فأخذ، [فذكر] مثل المرتين الأوليين فقال ادعي الله فلا أضرك. فدعت، له فأرسل، ثم دعا أدنى حجابه، فقال: إنك لم تأتني بإنسان، وإنما أتيتني بشيطان، أخرجها وأعطها هاجر، فأخرجت وأعطيت هاجر، فأقبلت، فلما أحس إبراهيم بمجيئها انفتل من صلاته، قال: مَهْيَم؟ قالت: كفى الله كيد الكافر الفاجر، وأخدمني هاجر)

  قال محمد بن سيرين وكان: أبو هريرة إذا حدث بهذا الحديث قال: فتلك أمكم يا بني ماء السماء

Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema:  Ibraahiym عليه السلام hakuongopa ila mara tatu tu; mara mbili kwa ajili ya Allaah aliposema, ((Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao)) na aliposema, ((Hakika mimi ni mgonjwa!)). Na alipokuwa akisafiri katika mji wa dhalimu mmoja na Sarah alikuwa naye. Alipopiga kambi, mtu mmoja alikwenda kwa dhalimu na kumwambia, "Kuna mtu amepiga kambi katika ardhi yako na anaye mwanamke mzuri kupita wote". Dhalimu akamuita Ibraahiym عليه السلام kwake, na akamuuliza, "Nini uhusiano wa mwanamke huyu na wewe?". Akasema, "Yeye ni dada yangu". Dhalimu akasema, "Nenda kamlete kwangu". Ibraahiym عليه السلام akaenda kwa Sarah na akasema, "Dhalimu huyu ameniuliza kuhusu wewe, na nimemwambia kwamba wewe ni dada yangu, kwa hiyo usimfanye akajua kwamba nimeongopa, kwani hakika ni dada yangu kufuatana na kitabu cha Allaah, na hakuna Waislamu katika ardhi hii ila mimi na wewe". Ibraahiym عليه السلام akampeleka (Sarah) kwake, kisha akasimama na kuswali. Alipoingia kwa dhalimu na (dhalimu) alipomuona (Sarah), akataka kumshika kwa matamanio, lakini akagandishiwa (mkono) Akasema, "Niombee kwa Allaah na sitokudhuru". Sarah akamuombea, na akaachiliwa. Kisha akamfikia kwa matamanio,  lakini akapatwa tena (kuganda mkono) kama mwanzo au zaidi. Ikaendelea hivyo mara tatu, na kila mara alisema kama alivyosema mara ya mwanzo. Kisha akamwita mlinzi wake wa karibu naye kabisa na akasema, "Hukuniletea binaadamu bali umenilitea shaytwaan! Muondoshe na mpe Haajar". Akaondoshwa (Sarah) na kupewa Haajar, akarudi. Ibraahiym عليه السلام alipotambua kuwa (Sarah) amerudi, alimaliza kuswali na kugeuka akasema, "Imekuwaje?". Akasema, "Allaah Ametosheleza njama za kafiri dhalimu, na amenipa Haajar kama mtumwa")) [Al Bukhaariy na Muslim].

Muhammad bin Siriyn amesema, "Abu Huraryah amesimulia Hadiyth hii  na akasema: "Huyu ni mama yenu enyi wana wa maji ya mbinguni" (yaani Waarabu kizazi cha Ismaa'iyl عليه السلام, mwana wa Haajar ambaye ndiye aliyesababisha maji ya Zamzam). [Fat-h Al-Baariy 6:447, Muslim 4:1840]

Mke wa Ibraahiym عليه السلام Sarah, alikuwa tasa. Na Ibraahiym عليه السلام alikuwa anazeeka na nywele zake zikatawaliwa na mvi baada ya kuita watu miaka mingi katika dini ya Allaah. Sarah akafikiria kwamba yeye na Ibraahiym عليه السلام wako katika upweke kwa vile hawakupata mtoto. Kwa hiyo akampa mumewe mtumwa wake Haajar amuoe.  Haajar akamzaa Ismaa'iyl  عليه السلام ambaye ndiye mtoto wa mwanzo wa Ibraahiym عليه السلام.

Siku zikapita na Ibraahiym عليه السلام akawa na furaha ya kupata mtoto, lakini Sarah akawa na wivu sasa na Haajar, ingawa yeye mwenyewe ndiye aliyempa Ibraahiym عليه السلام Haajar amuoe. Wivu huo ukamfanya Haajar awe anajificha ili Sarah asimuone anapokwenda kwa mumewe. Akawa ni mwanamke wa kwanza kufunga mkanda kuficha alama zake kama ilivyotajwa katika Hadiyth ndefu kutoka kwa  Al-Bukhaariy iliyopokelewa na Ibn 'Abbaas kwamba "Haajar ni mwanamke wa mwanzo kutumia mkanda".

Makusudio hapo ni mkanda kiunoni kuzuia nguo yake ndefu inayoburuza ardhini isiache alama apitapo (ikaja ikajulikana na Sarah kuwa kapita). Inasemekana kuwa wakati huo wanawake walikuwa wakivaa nguo ndefu zinazoburuza. Na hii inaonyesha jinsi stara ilivyokuwa kwa wanawake tangu wakati huo.

Pia katika masimulizi kwenye Sahiyh Al Bukhaariy anasema, ''Wakati Nabii Ibraahiym عليه السلام alipomuoa Haajar na akamzalia Ismaa'iyl عليه السلام, mkewe wa mwanzo, Sarah, akapata wivu na akaapa kuwa atamkata mwili wake vipande vitatu, hivyo Haajar akajifunga mkanda kiunoni mwake na kukimbia huku akiburuza vazi lake nyuma yake ili kufuta alama za nyayo zake ili Sarah asiweze kujua alipoelekea. (Al Bukhaariy - Kitabu cha Visa Vya Mitume, hadiyth namba 3364)

Na Allaah Anajua zaidi. 

SAFARI YA KWENDA MAKKAH

Siku moja Ibraahiym عليه السلام aliamka na kumwambia mke wake Haajar ajitayarishe kwa safari ndefu. Baada ya siku chache, Ibraahiym عليه السلام akaanza safari yake pamoja na mkewe na mwanawe Ismaa'iyl عليه السلام ambaye alikuwa bado ananyonya.

Ibraahiym عليه السلام akatembea na kupitia ardhi zilizolimwa, majangwa na milima hadi akafika katika jangwa la kisiwa cha Uarabu (Arabian Peninsula) na akafika katika bonde lisilolimwa ambalo halikuwa na miti wala matunda wala chakula wala maji. Bonde hilo halikuwa na athari yoyote ya maisha. Baada ya kumsaidia mkewe kuteremka kipando cha safari, akawaacha hapo wakiwa na chakula na maji kidogo tu ya kuwatosheleza kama siku mbili tu.

Aligeuka nyuma na kuondoka. Nyuma yake mkewe akamkimbilia na kumuuliza: "Unakwenda wapi Ibraahiym عليه السلام na kutuacha sisi katika bonde hili tupu?".Ibraahiym عليه السلام hakumjibu kitu bali aliendelea kuondoka. Haajar alirudia kumuuliza tena, lakini alinyamaza kimya bila ya kumjibu. Mwishowe alifahamu kuwa hafanyi hivyo kwa matamanio au amri yake, na akatambua kuwa Allaah سبحانه وتعالى Amemuamrisha kufanya hivyo. Akamuuliza: "Je, Allaah Amekuamrisha ufanye hivyo?". Akamjibu: "Ndio". Haajar akasema: "Basi hatutapotea ikiwa Allaah Aliyekuamrisha Atakuwa nasi". Ibraahiym عليه السلام akaondoka na alipokuwa mbali kiasi ya kutowaona akaomba:

((رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُواْ الصَّلاَةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ)

((Mola wetu! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuriya zangu katika bonde lisilo kuwa na mimea, kwenye Nyumba Yako Takatifu, ewe Mola wetu, ili wasimamishe Swalah. Basi Zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao, na waruzuku matunda, ili wapate kushukuru)) [Ibraahiym :37]

KUPATIKANA ZAMZAM

Ibraahiym عليه السلام akamuacha mkewe na mwanawe katika jangwa na akarudi alikotoka kuendelea kufanya da'wah ya kuwaita watu katika katika Tawhiyd. Haajar akabakia kumlea mwanawe hapo alipoachwa. Chakula kiliwaishia, maziwa yakamkauka, jua lilikua kali mno, maji waliyokuwa nayo yalikwisha na kiu kikawashika, hali ikawa mbaya ya njaa ya kiu kikubwa.

Ismaa'iyl عليه السلام akaanza kulia kwa kiu, mama yake akamuacha kwenda kutafuta maji. Akatembea kwa haraka hadi akafikia kilima cha Swafaa. Akapanda kilima na kuangaza kama ataona kisima au aone kama kuna msafara au chochote ili apate maji, lakini hakuona lolote.  Akateremka kilima na akawa anahangaika kwenda baina ya kilima cha Swafaa na kilima cha Marwah akipanda vilima vyote kila anapofikia kuangaza kama ataona lolote, lakini hakufanikiwa, na huku mwanawe anagaragara na kulia kwa kiu. Akawa anatembea na huku akikimbia mara nyingine baina ya Swafaa na Marwah kwa mara saba. Na ndio maana Mahujaji huwa wanatekeleza kitendo hiki kitufu cha ibada wanapokwenda Hajj au 'Umrah.

Hakika hii taadhima kubwa Allaah سبحانه وتعالى Aliyomjaalia Haajar, na ni fakhari kwa wanawake wote wa Kiislamu kuwa kitendo hiki cha Haajar kimekuwa ni kitendo cha ibada tukufu na kinatekelezwa na milioni ya watu hadi siku ya Qiyaamah.

Alipofika Marwah kwa mara ya saba alisikia sauti, mara akamuona Malaika anachimba ardhini kwa mbawa zake na mara maji yakamwagika kwa nguvu kabisa, akawa anayateka na kuyazuia yasimwagike zaidi. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema:

عن ابن عباس رضي الله عنهما قال: قال النبي صلى الله عليه وسلم: ((يرحم الله أم إسماعيل لو تركت زمزم))  أو قال: ((لو لم تغرف من الماء لكانت زمزم عينًا معينًا)) البخاري

Imetoka kwa Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema:  (Allaah Amrehemu mama yake Ismaa'iyl عليه السلام  angeliacha (maji ya zamzam)) (yamwagike bila ya kuyazuia) au kasema ((asingelichota kutoka katika maji hayo, zamzam ingelikuwa chemchemu inayoendelea kumwagika katika ardhi)) [Al-Bukhaariy]

Akanywa maji na kumnywesha mwanawe. Kulikuwa na misafara ya watu kutoka Yemen na walipoona kuna ndege wanazunguka wakatambua kuwa ni sehemu yenye maji.  Walikuwa watu wa kabila la Jurhum kutoka Yemen wakaja kuishi hapo. Wakamuuliza Haajar: "Je, unaturuhusu tuishi hapa?". Akajibu: "Ndio lakini hamtakua na haki kumiliki maji haya ya Zamzam". Wakakubali na Haajar akaridhika na akafurahi kupata watu kuishi nao. Wakaleta familia zao na wakazidi kuwa wengi hapo.

MTIHANI MKUBWA ALIOPEWA IBRAAHIYM عليه السلام  

WA KUMCHINJA  ISMAAI'YL عليه السلام

Ismaa'iyl عليه السلام akakua na baba yake Ibraahiym عليه السلام akawa anamtembelea mara kwa mara, kisha Allaah سبحانه وتعالى Akataka kumpa mtihani mkubwa mwingine Ibraahiym عليه السلام kutokana na mapenzi ya mwanawe Ismaa'iyl عليه السلام.  Allaah سبحانه وتعالى Anatuelezea mtihani huu katika aya zifuatazo:

 وَقَالَ إِنِّي ذَاهِبٌ إِلَى رَبِّي سَيَهْدِينِ ﴿99﴾ رَبِّ هَبْ لِي مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿100﴾ فَبَشَّرْنَاهُ بِغُلَامٍ حَلِيمٍ ﴿101﴾ فَلَمَّا بَلَغَ مَعَهُ السَّعْيَ قَالَ يَا بُنَيَّ إِنِّي أَرَى فِي الْمَنَامِ أَنِّي أَذْبَحُكَ فَانظُرْ مَاذَا تَرَى قَالَ يَا أَبَتِ افْعَلْ مَا تُؤْمَرُ سَتَجِدُنِي إِن شَاء اللَّهُ مِنَ الصَّابِرِينَ ﴿102﴾ فَلَمَّا أَسْلَمَا وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ ﴿103﴾ وَنَادَيْنَاهُ أَنْ يَا إِبْرَاهِيمُ ﴿104﴾ قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا إِنَّا كَذَلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ ﴿105﴾ إِنَّ هَذَا لَهُوَ الْبَلَاء الْمُبِينُ ﴿106﴾ وَفَدَيْنَاهُ بِذِبْحٍ عَظِيمٍ ﴿107﴾ وَتَرَكْنَا عَلَيْهِ فِي الْآخِرِينَ ﴿108﴾ سَلَامٌ عَلَى إِبْرَاهِيمَ ﴿109﴾ كَذَلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ ﴿110﴾ إِنَّهُ مِنْ عِبَادِنَا الْمُؤْمِنِينَ ﴿111﴾                   

((Na akasema: Hakika mimi nahama, nakwenda kwa Mola wangu ; Yeye Ataniongoa)) 

((Ewe Mola wangu ! Nitunukie aliye miongoni mwa watenda mema))

((Basi Tukambashiria mwana aliye mpole)) 

((Basi alipofika makamo ya kwenda na kurudi pamoja   naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyoamrishwa, utanikuta mimi, In sha Allaah, katika wanaosubiri))

((Basi wote wawili walipojisalimisha, na akamlaza juu ya  kipaji)) 

((Tulimwita: Ewe Ibraahiym!)) 

((Umekwishaitimiliza ndoto. Hakika hivi ndivyo Tunavyowalipa wanaotenda mema)

((Hakika haya ni majaribio yaliyo dhaahiri)) 

((Basi Tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu)) 

((Na Tukamwachia (sifa njema) kwa watu waliokuja baadaye)) 

((Iwe salama kwa Ibraahiym!)) 

((Hivi ndivyo tunavyowalipa wanaofanya mema)) 

((Hakika yeye ni katika waja wetu walioamini)) 

[As-Swaaffaat: 99-111]

Hakika huu ulikuwa ni mtihani mkubwa kwa Ibraahiym عليه السلام wa kuoteshwa amchinje mwanawe ambaye ndiye huyo huyo mmoja tu aliyempenda sana na ambaye amempata baada ya miaka mingi akiwa ameshakuwa mzee na baada ya kukata tamaa kabisa. 

Ibraahiym عليه السلام anatupa fundisho ya malezi mazuri baina ya baba na mtoto, kwani angelitaka maadamu ni amri ya kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى angelimchinja tu kama alivyoamrishwa katika ndoto, kwani ndoto za Manabii ni wahyi, lakini ametuonyesha adabu njema aliyomfanyia mwanawe kwa kutaka shauri aliposema:

 (( يَا بُنَيَّ إِنِّي أَرَى فِي الْمَنَامِ أَنِّي أَذْبَحُكَ فَانظُرْ مَاذَا تَرَى))

((Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje?)) [As-Swaafaat: 102]

Na mtoto naye anatupa mafunzo kwa kuheshimu wito wa baba yake ambao anajua haukuja kwa matamanio yake bali ni kutimiza amri ya Allaah سبحانه وتعالى , amri ambayo baba yake alijua ni muhimu na ghali kuliko mapenzi, huruma kwa mwanawe. Naye Ismaa'iyl alimjibu:

   ((قَالَ يَا أَبَتِ افْعَلْ مَا تُؤْمَرُ سَتَجِدُنِي إِن شَاء اللَّهُ مِنَ الصَّابِرِينَ))

((Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyoamrishwa, utanikuta mimi, In shaa Allaah, katika wanaosubiri. [As-Swaaffaat:102]

Ibraahiym عليه السلام alitambua kuwa mwanawe mwenyewe anashindana naye katika mapenzi ya Allaah سبحانه وتعالى  kwani hakujali kuchinjwa bali aliona kutekeleza amri ya Mola wake ni muhimu kuliko maisha yake.

Hatujui ilikuwaje hisia ya Ibraahiym عليه السلام alipojisalimisha mwanawe Ismaa'iyl عليه السلام achinjwe, bila ya shaka ilikuwa ni huruma ya hali ya juu hata akamlaza kifudifudi ili asimuone wakati anapomchinja. Allaah سبحانه وتعالى Anasema: ((فَلَمَّا أَسْلَمَا وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ))

((Basi wote wawili walipojisalimisha, na akamlaza juu ya kipaji ))

[As-Swaaffaat::103]

Maana kwamba wote wawili walipotamka Shahada na kumkumbuka Allaah سبحانه وتعالى kwani alikuwa Ibraahiym عليه السلام anakaribia kumchinja Ismaa'iyl عليه السلام, hivyo ingelikuwa ni mauti yake.  Au 'walipojisalimisha' ina maana kwamba walipofuata amri ya Allaah سبحانه وتعالى, Ibraahiym عليه السلام alimtii  Mola wake na Ismaa'iyl عليه السلام pia alimtii baba yake.  Hii ni rai ya Mujaahid, Ikrimah, Qataadah, As-Sudi na Ibn Is-haaq na wengineo.[At-Twabariy 21:77]

Maana ya:

((وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ)) ((na akamlaza juu ya kipaji))

ni kwamba, alimuelekeza uso wake kifudifudi ili amchinje kutoka kwa nyuma ili iwe wepesi kwake kufanya hivyo (asipate kuuona uso wake akashikwa na huruma na kushindwa kutekeleza amri ya Mola wake).  Ibn 'Abbaas, Mujaahid, Sa'iyd bin Jubayr, Adhw-Dhwahaak na Qataadah wamesema ina maana kwamba, "Alimgeuza kifudifudi". [At-Twabariy 21:77,78]

SHAYTWAAN ANAMSHAWISHI IBRAAHIYM  ASIMCHINJE ISMAA'IYL, NA KUPATIKANA SUNNAH YA KURUSHA VIJIWE KWENYE HAJJ

Imaam Ahmad amerekodi kwamba Ibn 'Abbaas amesema: "Wakati alipokuwa anataka kutekeleza Ibraahiym عليه السلام amri ya kumchinja 'Ismaa'iyl عليه السلام, shaytwaan alimjia katika Mas'aa na akakimbia naye, lakini Ibraahiym عليه السلام alifika mwanzo. Kisha Jibriyl عليه السلام  akamchukua katika Jamratul-'Aqabah na shaytwaan akamjia tena huko, kwa hiyo akampiga vijiwe saba mpaka akatokomea. Kisha akamjia tena katika Jamratul-Wustwaa, akampiga vijiwe saba. Kisha akamlaza kifudifudi. Ismaa'iyl عليه السلام alikuwa amevaa shati jeupe na akasema: "Ewe baba yangu, sina nguo yoyote ambayo nitakafiniwa, kwa hiyo nivue ili iwe nikafiniwe nayo. Alianza kuivua ndipo alipoitwa nyuma:

((وَنَادَيْنَاهُ أَنْ يَا إِبْرَاهِيمُ))       ((قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا))

((Tulimwita: Ewe Ibraahiym!)) 

((Umekwisha itimiliza ndoto)) [As-Swaaffaat:104-105]

Ibraahiym عليه السلام aligeuka na akamuona kondoo mweupe mzuri mwenye pembe.

Ibn 'Abbaas kasema: "Tulikuwa tukitafuta aina kama ya huyo kondoo" (yaani wakati wa kuchinja katika 'Iydul-Adhwhaa)  [Ahmad:1:297]

As-Suddiy na wengineo wamesema kwamba alikipitisha kisu shingoni mwa Ismaa'iyl عليه السلام lakini hakikumkata kwa sababu aliwekewa bamba la shaba.

Na ndipo Ibraahiym عليه السلام alipoitwa:

((قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا))

((Umekwisha itimiliza ndoto)) [As-Swaaffaat:105]

[At-Twabariy 21:74]

Ibn 'Abbaas amesema kuwa: "Kondoo huyo alikuzwa Peponi kwa muda wa miaka arubaini".[At-Twabariy 21:90]

Kitendo hiki cha kuchinja ndicho kinachofanyika katika taratibu za Hajj, kufuata Sunnah ya baba yetu Ibraahiym عليه السلام.


UTHIBITISHO KWAMBA ALIYETAKA KUCHINJWA NI IS'MAA'IYL NA SI IS-HAAQ KAMA WANAVYODAI MAYAHUDI NA MANASWARA

Imaam Ahmad amerekodi kwamba Swafiyyah bin Shaybah alisema: "Mwanamke kutoka Bani Sulaym ambaye alikuwa mkunga (midwife) wa wengi katika jamii yetu, kaniambia kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alimtuma 'Uthmaan bin Talhah رضي الله عنه  akazifunike pembe katika Ka'abah ili zisiwashawishi watu wanaposwali: Akasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :

))إني كنتُ رأيت قرني الكبش، حين دخلت البيت، فنسيت أن آمرك أن تخمرهما، فَخَمَّرْهما، فإنه لا ينبغي أن يكون في البيت شيء يشغل المصلي". قال سفيان: لم يزل قرنا الكبش معلقين في البيت حتى احترق البيت، فاحترقا)) أحمد.

((Niliziona pembe za kondoo nilipoingia katika Nyumba (yaani Kaabah) nikasahau kukuambia uzifunike, zifunike kwani kusiweko na kitu katika nyumba (Ka'abah) cha kuwashawishi watu wanaofanya ibada)). 

 [Ahmad 4:68]

Wasimulizi waliosimulia kuhusu pembe hizo za kondoo:.   

 -Sufyan kasema: "Pembe za kondoo zilibakia zikining'inia katika Nyumba (Ka'abah) hadi zilipoungua wakati Nyumba ilipoungua"

-Sa'iyd bin Jubayr, 'Aamir Ash-Sha'abiy, Yuusuf bin Mihraan, Mujaahid, 'Atwaa' na wengineo wameripoti kutoka Ibn 'Abbaas kwamba alikuwa ni 'Ismaa'iyl عليه السلام.

-Ibn Jariyr amesimulia kwamba Ibn 'Abbaas amesema: "Aliyefidiwa alikuwa ni Ismaa'iyl عليه السلام. Mayahudi wamedai kuwa ni Is-haaq, lakini Mayahudi wameongopa". [At-Twabariy 21:83]

-Ibn Is-haaq amesema, "Nimemsikia Muhammad bin Ka'ab Al-Quraazi anasema, "Ambaye Allaah سبحانه وتعالى Ameamuamrisha Ibraahiym عليه السلام kumchinja miongoni mwa wanawe wawili alikuwa ni Ismaa'iyl عليه السلام.  Tunapata dalili hii kutoka kitabu cha Allaah سبحانه وتعالى kwa sababu Allaah سبحانه وتعالى Anapomalizia kisa cha mmoja wa wana wawili wa Ibraahiym عليه السلام ambaye alitakiwa kuchinjwa Amesema;

((وَبَشَّرْنَاهُ بِإِسْحَقَ نَبِيًّا مِّنَ الصَّالِحِينَ))

((Na Tukambashiria kuzaliwa Is-haaq, naye ni Nabii miongoni mwa watu wema)). [As-Swaaffaat:112]

Vile vile,

((فَبَشَّرْنَاهَا بِإِسْحَقَ وَمِن وَرَاء إِسْحَقَ يَعْقُوبَ))

((Basi Tukambashiria (kuzaliwa) Is-haaq, na baada ya Is-haaq Ya'aquwb)) [Huud:71]

Allaah سبحانه وتعالى Amemtaja mtoto na mwanawe, lakini Asingelimuamrisha kumchinja Is-haaq wakati Aliahidi kuwa mwanawe (Is-haaq) atazaa mtoto. Kwa hiyo  ni dhahiri kuwa yule aliyeamrishwa amchinje ni Ismaa'iyl عليه السلام". [At-Twabariy 21:84].

 Hadiyth nyingi zimenukuliwa kuhusu mas-ala haya [Tafiiyr Ibn Kathiyr 8:277-279]

ZIARA YA IBRAHIYM عليه السلام  KWA WAKE ZAKE ISMAA'IYL

[Maelezo haya yamenukuliwa kutoka Hadiyth ndefu ya Ibn 'Abbaas iliyosimuliwa na Al-Bukhaariy]

 Baada ya kufa mama yake Ismaa'iyl عليه السلام, Ibraahiym alikuja kumtembelea Ismaa'iyl عليه السلام nyumbani kwake (ambaye alikuwa amekwishaoa). Alipofika hakumkuta Ismaa'iyl عليه السلام bali alimkuta mkewe peke yake. Akamuuliza: "Yuko wapi Ismaa'iyl?". Akajibu: "Amekwenda kutafuta rizki". Ibraahiym عليه السلام akamuuliza kuhusu hali ya maisha yao, akajibu: "Tunaishi katika shida, dhiki na karaha". Akamwambia: "Atakaporudi mumeo mpe salam zangu na mwambie abadilishe kizingiti chake".

Aliporudi Ismaa'iyl عليه السلام alihisi hali sio ya kawaida yaani kama kumetokea kitu, akamuuliza mkewe: "Je, amekuja mtu yeyote kukutembelea?" Akajibu: "Ndio, bwana mmoja mtu mzima mwenye sifa kadha na kadha amekuja na ameniuliza kuhusu wewe nikamjulisha, kisha akaniuliza kuhusu hali ya maisha, nikamuambia kuwa tunaishi katika shida, dhiki na umasikini". Ismaa'iyl عليه السلام hapo akamuuliza: "Je, amekupa maagizo yangu yoyote?".  Akajibu: "Ndio, amenipa salam zako, kisha amesema nikuambie kuwa ubadilishe kizingiti chako". Ismaa'iyl عليه السلام akasema: "Huyo ni baba yangu, na ameniamrisha nikupe talaka, basi rudi kwenu". Ismaa'iyl عليه السلام akampa talaka, kisha akaoa mwanamke mwingine miongoni mwao (yaani kutoka kabila la Jurhumu).

Mara ya pili alipokuja Ibraahiym عليه السلام kumtembelea Ismaa'iyl عليه السلام alimkuta mke wake Ismaa'iyl عليه السلام wa pili, alipoumuuliza kuhusu Ismaa'iyl عليه السلام alisema: "Amekwenda kutafuta rizki". Ibraahiym عليه السلام akamuuliza kuhusu maisha yao, akajibu: "Tuko katika neema na tumebahatika (yaani tuna kila kitu cha kututosheleza)". Akamshukuru Allaah سبحانه وتعالى. Ibraahiym عليه السلام akamuuliza: "Aina gani ya chakula mnakula?". Akasema: "Nyama". Akasema: "Mnakunywa nini?", Akasema: "Maji". Akasema: "Ya Allaah Wabarikie nyama yao na maji yao".  (Mkewe amesema hivyo ingawa hali yao ilikuwa ni ya shida).

Ibraahiym عليه السلام akamwambia mke wa Ismaa'iyl عليه السلام: "Atakaporudi mumeo mpe salam zangu na mwambie ashikilie kizingiti chake". Aliporudi Ismaa'iyl عليه السلام alimuuliza mkewe: "Je, amekuja mtu yeyote?". Akajibu: "Ndio, amekuja bwana mmoja mtu mzima mwenye sura nzuri". Akamsifia kisha akaendelea: "Ameniuliza kuhusu wewe nikamjulisha, kisha akauliza kuhusu hali ya maisha yetu, nikamuambia kuwa tunaishi katika hali nzuri". Ismaa'iyl عليه السلام akamuuliza: "Je, alikupa nasiha yoyote?". Akajibu: "Ndio, amekupa salaam zake kisha anakuamrisha ushikilie kizingiti chako".

Kwa maneno haya, Ismaa'iyl عليه السلام akasema: "Huyo alikuwa ni baba yangu na  wewe ndio kizingiti, na ameniamrisha nibakie na wewe".

 KUJENGA KA'ABAH

Allaah سبحانه وتعالى  Akamuamrisha Ibraahiym عليه السلام ajenge Ka'abah.  Ibraahiym عليه السلام na Ismaa'iyl عليه السلام wakapandisha msingi wa nyumba (yaani Ka'abah). Ismaa'iyl عليه السلام akawa analeta mawe huku Ibraahiym عليه السلام anajenga.  Kuta za nyumba ziliponyanyuka juu, Ismaa'iyl عليه السلام alileta jiwe na kumpa Ibraahiym عليه السلام ili asimamie kuendelea kujenga huku Ismaa'iyl عليه السلام anamletea mawe.

Ibraahiym عليه السلام alikuwa akisimama juu ya jiwe hilo na kila alipomaliza kujenga upande mmoja alisogea upande mwingine kumalizia kujenga Ka'abah.

Jiwe hilo liliweka alama ya miguu yake Ibraahiym عليه السلام.  Alipomaliza kujenga aliliweka jiwe karibu na ukuta wa Ka'abah na hapo ndipo mahali lilipokuwa miaka yote hiyo hadi ilipofika zama za ukhalifa wa 'Umar رضي الله عنه ndiye aliyelisogeza kutoka kuta za Ka'abah. 'Umar  رضي الله عنه ni mmoja wa wawili ambao Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((اقتدوا باللَّذَين من بعدي أبي بكر وعمر

((Wafuateni watakaokuwa baada yangu, Abu Bakar na 'Umar)) [Tuhfat Al-Ahwadhiy: 569]

Na hii ndio  sehemu inayoitwa  'Maqaam Ibraahiym' (Kisimamo cha Ibraahiym) ambako anatakiwa mwenye kufanya Hajj au 'Umrah aswali Raka'ah mbili baada ya kufanya twawwaaf. Na amri ya kuswali Raka'ah mbili ilikuwa ni kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى kwa sababu ya 'Umar ibnul-Khatwaab رضي الله عنه .

Ibn Abi Haatim ameripoti kuwa Jaabir alipokuwa akisimulia Hajj ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  amesema: "Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipofanya Twawwaaf, 'Umar alimuuliza: "Hii ndio Maqaam ya baba yetu?" akasema: "Ndio". 'Umar akasema: "Je, tuifanye sehemu ya kuswalia?". Ikawa ndio sababu ya Allaah سبحانه وتعالى Kuteremsha aya hii:

   ((وَاتَّخِذُواْ مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى))

((Na alipokuwa akisimama Ibraahiym pafanyeni pawe pa kuswalia)) [Al-Baqarah:125]

UTUKUFU WA KA'ABA

Mahali pa salama na amani

Anasema Allaah سبحانه وتعالى  kuhusu utukufu wa Ka'abah:

((وَإِذْ جَعَلْنَا الْبَيْتَ مَثَابَةً لِّلنَّاسِ وَأَمْناً وَاتَّخِذُواْ مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى وَعَهِدْنَا إِلَى إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ أَن طَهِّرَا بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْعَاكِفِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُود))

((Na kumbukeni Tulipoifanya ile Nyumba (ya Al-Ka'abah) iwe pahala pa kukusanyikia watu na pahala pa amani. Na alipokuwa akisimama Ibraahiym pafanyeni pawe pa kuswalia. Na Tuliagana na Ibraahiym na Ismaa'yil: Itakaseni Nyumba Yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kutufu na wanaojitenga huko kwa ibada, na wanaoinama na kusujudu))

[Al-Baqarah:125]

Maana ya 'pahala pa amani' ina maana kwamba amani  kutokana na maadui. Na ikaendelea Ka'abah kuwa mahali patukufu tokea siku hizo mpaka hii leo inajulikana kwa utukufu wake. Hata zama za ujaahiliyyah watu mara nyingi walikuwa ni waathirika wa uvamizi na watekwa nyara, ila waliokuwa katika eneo la Ka'abah (Al-Masjidul-Haraam) ndio walikuwa salama kutokana na kutekwa nyara. [At-Twabariy 3:29]

Vile vile Mujaahid, 'Atwaa' As-Suddiy, Qataadah na Ar-Rabi' bin Anas wameripotiwa wakisema kwamba Aya hiyo ina maana: "Yeyote atakayeingia humo atakuwa salama". [Ibn-Abi Haatim 1:370].

Aya hii ina inaonyesha kwamba Allaah سبحانه وتعالى Ameitukuza nyumba hii tukufu ambayo Ameifanya iwe kimbilio na bandari ya salama. Kwa hiyo nafsi za watu huwa zina hamu kubwa ya kuweko hapo na hawachoshwi kutembelea kila mara au kila mwaka. Hii ni kwa sababu Allaah سبحانه وتعالى Aliikubali Du'aa ya Ibraahiym عليه السلام alipomuomba Allaah سبحانه وتعالى Ajaaliye nyoyo za watu zipende kuelekea huko wakati alipomuacha mkewe Haajar na mwanawe Ismaa'iyl عليه السلام mwanzo alipofika hapo.   [Al-Bukhaariy 3364]

Aliomba:

((رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُواْ الصَّلاَةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ))

((Mola wetu! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuriya zangu katika bonde lisilokuwa na mimea, kwenye Nyumba Yako Takatifu, ewe Mola wetu, ili wasimamishe Swalah. Basi Zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao, na Waruzuku matunda, ili wapate kushukuru)) [Ibraahiym :37]

Mahali patukufu pa kuswaliwa

Heshima ya mwanzo inamfikia Ibraahiym عليه السلام kwa kufanywa sehemu aliyosimama kujenga Ka'abah kuwa mahali patukufu pa kuswaliwa.

((وَاتَّخِذُواْ مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى))

((Na alipokuwa akisimama Ibraahiym pafanyeni pawe pa kuswalia)) [Al-Baqarah:125]

Nyumba iliyotakaswa

Vile vile ilikuwa ni amri kwa Ibraahiym عليه السلام na mwanawe Ismaa'iyl عليه السلام kwamba waitakase Ka'abah. ((وَعَهِدْنَا إِلَى إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ أَن طَهِّرَا بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْعَاكِفِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ))

((Na Tuliagana na Ibraahiym na Ismaa'iyl: Itakaseni Nyumba Yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kutufu na wanaojitenga huko kwa ibada, na wanaoinama na kusujudu)) [Al-Baqarah:125]

Hali kadhalika ilikuwa ni amri ya kuitakasa na shirki :

((وَإِذْ بَوَّأْنَا لِإِبْرَاهِيمَ مَكَانَ الْبَيْتِ أَن لَّا تُشْرِكْ بِي شَيْئًا وَطَهِّرْ بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْقَائِمِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ))

((Na pale Tulipomweka Ibraahiym pahala penye ile Nyumba Tukamwambia: Usinishirikishe na chochote; na isafishe Nyumba Yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kutufu, na wanaokaa hapo kwa ibada, na wanaorukuu, na wanaosujudu)) [Al-Hajj:26]

Maana: Ifanye iwe safi  kwa wale wanaomuabudu Allaah Pekee bila ya kumshikirikisha na mtu au msaidizi.

Nyumba ya pekee inayozungukwa kama ibada

Ni nyumba pekee katika ulimwengu wa Waislamu inayozungukwa kama ni kitendo cha ibada. Twawwaaf na Swalah zimetajwa pamoja katika aya hiyo, kwa sababu hakuna mahali popote kwengine kulikofaradhishwa ibada hizi mbili pamoja isipokuwa hapa katika Ka'abah.     

  • Ni Msikiti wa mwanzo ulimwenguni
  • Ni Msikiti wenye baraka na uongofu

Nayo ni nyumba ya mwanzo kabisa duniani iliyofanywa kuwa ya ibada, yenye baraka, uongofu kwa watu wote, na ndipo Waislamu huenda kutekeleza nguzo yao ya tano ya fardhi.

((إِنَّ أَوَّلَ بَيْتٍ وُضِعَ لِلنَّاسِ لَلَّذِي بِبَكَّةَ مُبَارَكًا وَهُدًى لِّلْعَالَمِينَ))

((Hakika Nyumba ya kwanza waliowekewa watu kwa ibada ni ile iliyoko Bakkah,(Makkah), iliyobarikiwa na yenye uongofu kwa walimwengu wote)) [Al'Imraan:96]

عن أبي ذَر، رضي الله عنه، قال قلتُ: يا رسولَ الله، أيُّ مَسجِد وُضِع في الأرض أوَّلُ؟ قال: ))الْمسْجِدُ الْحَرَامُ((. قلت: ثم أَيُّ؟ قال: ))الْمسجِدُ الأقْصَى(( قلت: كم بينهما؟ قال: ))أرْبَعُونَ سَنَةً((. قلتُ: ثم أَيُّ؟ قال (( ثُم حَيْثُ أدْرَكْت الصَلاةَ فَصَلِّ، فَكُلُّهَا مَسْجِدٌ)).  أخرجه البخاري، ومسلم، وأحمد

Imetoka kwa Abu Dharr amesema: "Nilisema Ewe Mjumbe wa Allaah, msikiti gani ulikuwa wa mwanzo kabisa kujengwa duniani?" Akasema: ((Al-Masjidul-Haraam)) (Ulioko Makkah).  Nikasema: Kisha upi? Akasema: ((Al-Masjidul-Aqswaa)) (Palestina). Nikasema: Ilikuwa muda gani kujengwa baina yao? Akasema: ((Miaka arubaini)) Akaongeza: ((Popote (mtakapokuwa) na Swalah ikawakuta, Swalini humo, kwani ardhi yote imefanywa kuwa ni msikiti)) [Al-Bukhaariy, Muslim na Imaam Ahmad]

Usemi mwingine kutoka kwa wataalamu wanaofasiri, wamesema kuwa kwa vile Adam عليه السلام ni kiumbe cha mwanzo katika ardhi, alipewa heshima kujenga nyumba ya mwanzo ya ibada. Aliijenga kisha akaizunguka kama Malaika wanvyozunguka juu katika Baytul-Ma'amuur huko juu katika 'Arshi ya Allaah سبحانه وتعالى iliyoko katika mbingu ya saba.  Na inasemekana alijenga hema akawa anafanya ibada yake hapo, lakini baada ya kufariki na karne nyingi kupia, ikapotea alama ya sehemu hiyo. 

Nguzo ya tano ya Kiislamu inatimizwa hapo

 (( فِيهِ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ مَّقَامُ إِبْرَاهِيمَ وَمَن دَخَلَهُ كَانَ آمِنًا وَلِلّهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلاً وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ الله غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ)) 

((Ndani yake zipo Ishara zilizo wazi - masimamio ya Ibraahiym, na mwenye kuingia humo anakuwa katika amani. Na kwa ajili ya Allaah imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea. Na atakayekanusha basi Allaah si mhitaji kwa walimwengu))  [Al-'Imraan: 97]

DU'AA ZA IBRAAHIYM عليه السلام BAADA YA KUJENGA KA'ABAH

Anasema Allaah سبحانه وتعالى :

((وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ وَإِسْمَاعِيلُ رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ))

((Na kumbukeni Ibraahiym na Ismaa'iyl walipoinyanyua misingi ya ile Nyumba wakaomba: Ewe Mola wetu! Tutakabalie! Hakika Wewe Ndiye Msikizi Mjuzi)) [Al-Baqarah:127]

Hapa tunapata fundisho kubwa kutoka kwa baba yetu Nabii Ibraahiym عليه السلام kwamba ingawa yeye na Ismaa'iyl عليه السلام wamejenga Ka'abah, nyumba ambayo inayozungukwa na mamilioni ya Waislamu kama ni ibada tukufu mpaka siku ya Qiyaamah, lakini hawakutegemea kwamba Allaah سبحانه وتعالى Atawapokelea amali hii moja kwa moja, bali kwanza wamemuomba Mola Awatakabalie. Hii ni tabia ya waumini wenye ikhlaas ambao wako baina ya khofu na matumaini wanapofanya vitendo vyema. Na sisi tunatakiwa tuwe tunaiomba Du'aa hii kila mara tunapomaliza kitendo au vitendo vyovyote vyema kwani vile vile hatujui kama vitendo hivyo vitakubaliwa na Mola wetu au havitakubaliwa. 

Akaendelea Ibraahiym عليه السلام kuomba pamoja na mwanawe Ismaa'iyl عليه السلام,

(( رَبَّنَا وَاجْعَلْنَا مُسْلِمَيْنِ لَكَ وَمِن ذُرِّيَّتِنَا أُمَّةً مُّسْلِمَةً لَّكَ وَأَرِنَا مَنَاسِكَنَا وَتُبْ عَلَيْنَآ إِنَّكَ أَنتَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ))

((Ewe Mola wetu! Tujaalie tuwe ni wenye kusilimu Kwako, na pia miongoni mwa vizazi vyetu wawe umma uliosilimu Kwako. Na Utuonyeshe njia za ibada yetu na Utusamehe. Bila shaka Wewe Ndiye Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu)) [Al-Baqarah: 128] ((وَأَرِنَا مَنَاسِكَنَا)) ((utuonyeshe njia za ibada yetu))

Ina maana ni Taratibu za Hajj na 'Umrah ambazo Waislamu wanazifuata kutekelea nguzo ya  tano ya Kiislamu.

  ((رَبَّنَا وَابْعَثْ فِيهِمْ رَسُولاً مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِكَ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُزَكِّيهِمْ إِنَّكَ أَنتَ العَزِيزُ الحَكِيمُ))    

((Ewe Mola wetu! Waletee Mtume anayetokana na wao, awasomee Aayah Zako, na awafundishe Kitabu na hikima na awatakase. Hakika Wewe Ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima)) [Al-Baqarah:129]

Du'aa hii: ((Waletee Mtume anayetokana na wao)) ndio sababu ya kutoka Mtume wa mwisho kutoka kizazi cha Ismaa'iyl عليه السلام naye ndiye Mtume bora kabisa kuliko mitume yote naye ni kipenzi cha Umma wa Kiislamu, Muhammad  صلى الله عليه وآله وسلم .

Vile vile maana ya ((awasomee Aya Zako, na awafundishe Kitabu na hikima)) ndio kitabu cha mwisho nacho ni Qur'aan aliyopewa Mtume Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم  ambayo ni uongofu kamili kwa watu wote ulimwenguni Waarabu na wasio Waarabu. 

Du'aa nyingine alizoomba Ibraahiym عليه السلام :

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ اجْعَلْ هَذَا الْبَلَدَ آمِنًا وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَن نَّعْبُدَ الأَصْنَامَ ﴿35﴾ رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ فَمَن تَبِعَنِي فَإِنَّهُ مِنِّي وَمَنْ عَصَانِي فَإِنَّكَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿36﴾ رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُواْ الصَّلاَةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ ﴿37﴾ رَبَّنَا إِنَّكَ تَعْلَمُ مَا نُخْفِي وَمَا نُعْلِنُ وَمَا يَخْفَى عَلَى اللّهِ مِن شَيْءٍ فَي الأَرْضِ وَلاَ فِي السَّمَاء ﴿38﴾ الْحَمْدُ لِلّهِ الَّذِي وَهَبَ لِي عَلَى الْكِبَرِ إِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَقَ إِنَّ رَبِّي لَسَمِيعُ الدُّعَاء ﴿39﴾ رَبِّ اجْعَلْنِي مُقِيمَ الصَّلاَةِ وَمِن ذُرِّيَّتِي رَبَّنَا وَتَقَبَّلْ دُعَاء ﴿40﴾ رَبَّنَا اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِلْمُؤْمِنِينَ يَوْمَ يَقُومُ الْحِسَابُ ﴿41﴾

((Na Ibraahiym aliposema: Ee Mola wangu! Ujaalie mji huu uwe wa amani, na Uniepushe mimi na wanangu na kuabudu masanamu)

((Ee Mola wangu! Hakika hayo yamewapoteza watu wengi. Basi aliyenifuata mimi huyo ni wangu, na aliyeniasi, hakika Wewe ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu)) 

((Mola wetu! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuriya zangu katika bonde lisilo kuwa na mimea, kwenye Nyumba Yako Takatifu, Ee Mola wetu , ili washike Swalah. Basi Zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao, na waruzuku matunda, ili wapate kushukuru))

((Ee Mola wetu ! Hakika Wewe Unajua tunayoyaficha na tunayoyatangaza. Na hapana kitu kinachofichikana kwa Allaah katika ardhi wala katika mbingu)). 

((AlhamduliLLaah! Himdi zote ni za Allaah Aliyenipa juu ya uzee wangu Ismaa'iyl na Is-haaq. Hakika Mola wangu ni Mwenye kusikia maombi))  ((Mola wangu! Nijaalie niwe mwenye kushika Swalah, na katika dhuriya zangu pia. Ewe Mola wetu , na Ipokee dua yangu)) 

((Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu))[Ibraahiym: 35-41]

KUWAADHINIA WATU WAITIKIE KWENDA HAJJ

Alipomaliza kujenga Ka'abah Ibraahiym عليه السلام, Allaah سبحانه وتعالى Alimtaka awatangazie watu waje kuhiji kama ilivyo katika aya hii ifuatayo:

((وَأَذِّن فِي النَّاسِ بِالْحَجِّ يَأْتُوكَ رِجَالًا وَعَلَى كُلِّ ضَامِرٍ يَأْتِينَ مِن كُلِّ فَجٍّ عَمِيقٍ))

((Na watangazie watu Hajj; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliyekonda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali)) [Al-Hajj:27]

Ibraahiym عليه السلام alisema: "Mola wangu, vipi niwatangazie watu hivyo na hali sauti yangu haitawafikia?" Akaambiwa: "Waite (waadhinie) na Sisi Tutawafikishia". Ibraahiym عليه السلام akasimama na kusema: "Enyi watu, Mola wenu Ameanzisha  Nyumba ili mje kuhiji".

Imesemekana kuwa milima ilijiinamisha ili sauti ifikie pande zote za dunia, na ikawafikia watu wote mpaka waliokuwa matumboni mwa mama zao na migongo ya baba zao (yaani waliokuwa hawakuzaliwa bado).

Na majibu yakaja kutoka kwa kila mtu kutoka kila miji, majangwa na mashamba, na hao ndio ambao waliokwishajaaliwa kufika Makkah kutimiza Hijjah na vile vile wale ambao bado hawakufika, lakini watakaojaaliwa kufika kutimiza Hijjah mpaka siku ya Qiyaamah, waliokuwa hai na waliokuwa bado hawakuzaliwa, itakuwa ndio sauti ya Ibraahiym عليه السلام imewafikia.  Majibu  ya watu yalikuwa

"لبيك اللهم لبيك"

"Labbayka Allaahumma Labbayk"  

Nimekuitika Ee Allaah nimekuitika,

Na hivi ndivyo anavyosema mwenye kufanya Hijjah anapoingia katika Ihraam akiwa tayari kutekeleza taratibu za 'Umrah na Hijjah.

KUONDOKA MAKKAH BAADA YA KUJENGA KA'ABA

Ibraahiym عليه السلام akaondoka Makkah kwenda kuendelea na da'awa ya kuwaita watu katika Tawhiyd, akiwa na mkewe Sarah na akamuacha Ismaa'iyl عليه السلام pamoja na familia yake Makkah.  

Siku moja Ibraahiym عليه السلام alikuwa amekaa katika kambi yake akimfikiria mwanawe Ismaa'iyl عليه السلام, ndoto ya kumchinja na fidia Aliyomteremshia Allaah سبحانه وتعالى. Moyo wake ukazidi kujaa mapenzi ya Allaah سبحانه وتعالى kwa neema Zake zisizohesabika. Chozi kubwa likamdondoka alivyokuwa akimfikiria Ismaa'iyl عليه السلام na umbali alioko, jinsi alivyokuwa akimkosa na hamu ya kuwa naye. Mara Malaika watatu wakateremka; Jibriyl, Israafiyl na Miykaaiyl. Walimjia kwa maumbo ya binaadamu wenye sura nzuri kabisa. Ibraahiym عليه السلام aliinuka na kuwakaribisha. Aliwaita ndani ya kambi huku akiwaza kuwa ni wageni asiowajua. Akawakaribisha vizuri na kuhakikisha kuwa wamestarehe, kisha akaomba idhini kwao ili aende kwa ahli yake. (kuagiza waletewe chakula).  

Sarah wakati huo ameshakuwa mzee, mvi zimemjaa kichwani. Ibraahiym عليه السلام akamuambia: "Tumepata wageni watatu".

Akamuuliza: "Ni nani hao?". Akamjibu: "Simjui hata mmoja wao". Akauliza Ibraahiym عليه السلام: "Tuna chakula gani?". Akajibu Sarah: "Tuna nusu kondoo". Ibraahiym عليه السلام akasema: "Nusu kondoo? Wachinjie nusu ndama, kwani wao ni wageni tusiowajua na hatujui pengine wana njaa".

Watumishi wakachinja nusu ndama na kumchoma vizuri. Kikaletwa chakula mbele ya hao wageni, Ibraahiym عليه السلام akawakaribisha wasogee kula. Akaona hawasogei kula, basi akaanza kula yeye ili awatie moyo nao watake kula lakini aliona kuwa hakuna hata mmoja wao aliyegusa chakula. Akawauliza: "Kwa nini hamli?". Akaendelea yeye kula, lakini wao walibakia vile vile bila ya kukaribisha mikono yao katika chakula. Ibraahiym عليه السلام akaanza kuogopa.

Khofu ya Ibraahiym عليه السلام ikazidi na Malaika wakawa wanamsoma mawazo yake, kisha mmoja wao akasema: "Usikhofu". Ibraahiym عليه السلام akasema: "Hakika nina khofu, kwani nimekukaribisheni mle lakini naona hamjanyoosha mikono yenu kutaka kula. Je, mmekusudia uovu?". Malaika mmoja akatabasamu na kusema: "Sisi hatuli, kwani sisi ni Malaika wa Allaah". Mmoja wao akageuka kwa mkewe Ibraahiym عليه السلام na kumbashiria bishara njema ya mwana Is-haaq. 

Ibraahiym عليه السلام na Sarah walishtuka kubashiriwa mtoto katika umri huo walionao. Lakini juu ya mshtuko huo, Sarah aliingiwa na furaha kubwa kuwa atapata mtoto ambaye alimtamani miaka mingi sana! Na furaha ilizidi alipoambiwa kuwa mtoto huyo atakuwa ni mtoto mwenye ujuzi.  

Allaah سبحانه وتعالى Ametuelezea matukio haya kwa kirefu katika Aya zifuatazo:

 وَنَبِّئْهُمْ عَن ضَيْفِ إِبْراَهِيمَ ﴿51﴾ إِذْ دَخَلُواْ عَلَيْهِ فَقَالُواْ سَلامًا قَالَ إِنَّا مِنكُمْ وَجِلُونَ ﴿52﴾ قَالُواْ لاَ تَوْجَلْ إِنَّا نُبَشِّرُكَ بِغُلامٍ عَلِيمٍ ﴿53﴾ قَالَ أَبَشَّرْتُمُونِي عَلَى أَن مَّسَّنِيَ الْكِبَرُ فَبِمَ تُبَشِّرُونَ ﴿54﴾ قَالُواْ بَشَّرْنَاكَ بِالْحَقِّ فَلاَ تَكُن مِّنَ الْقَانِطِينَ ﴿55﴾ قَالَ وَمَن يَقْنَطُ مِن رَّحْمَةِ رَبِّهِ إِلاَّ الضَّآلُّونَ ﴿56﴾ قَالَ فَمَا خَطْبُكُمْ أَيُّهَا الْمُرْسَلُونَ ﴿57﴾ قَالُواْ إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَى قَوْمٍ مُّجْرِمِينَ ﴿58﴾ إِلاَّ آلَ لُوطٍ إِنَّا لَمُنَجُّوهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿59﴾ إِلاَّ امْرَأَتَهُ قَدَّرْنَا إِنَّهَا لَمِنَ الْغَابِرِينَ ﴿60﴾

((Na uwape khabari za wageni wa Ibraahiym)) 

((Walipoingia kwake na wakasema: Salama! Yeye akasema: Hakika sisi tunakuogopeni))

((Wakasema: Usiogope. Sisi tunakubashiria kijana mwenye ujuzi))   

((Akasema: Mnanibashiria nami uzee umenishika! Basi kwa njia gani mnanibashiria?)) 

((Wakasema: Tunakubashiria kwa haki; basi usiwe miongoni mwa wanaokata tamaa)) 

((Akasema: Na nani anaye kata tamaa na Rehema ya Mola wake ila wale waliopotea?)) 

((Akasema: Hebu nini amri yenu, enyi wajumbe?)) 

((Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya wakosefu!)) 

((Isipo kuwa waliomfuata Luut. Bila ya shaka sisi tutawaokoa hao wote)) 

((Ila mkewe. Tunakadiria huyo atakuwa miongoni wa wataobakia nyuma))

[Al-Hijr: 51-60]

Waliposema kuwa wanakwenda kuangamiza mji wa Luut  عليه السلام Ibraahiym عليه السلام alikhofu kuwa vipi wataangamiza mji huo na hali yumo Luut عليه السلام? Majibu yao Malaika yamo katika aya zifuatazo:  

((وَلَمَّا جَاءتْ رُسُلُنَا إِبْرَاهِيمَ بِالْبُشْرَى قَالُوا إِنَّا مُهْلِكُو أَهْلِ هَذِهِ الْقَرْيَةِ إِنَّ أَهْلَهَا كَانُوا ظَالِمِينَ))

 ((قَالَ إِنَّ فِيهَا لُوطًا قَالُوا نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَن فِيهَا لَنُنَجِّيَنَّهُ وَأَهْلَهُ إِلَّا امْرَأَتَهُ كَانَتْ مِنَ الْغَابِرِينَ))   

((Na wajumbe wetu walipomjia Ibraahiym na bishara, walisema: Hakika sisi hapana shaka tutawahiliki watu wa mji huu, kwani watu wake hakika wamekuwa madhaalimu)) 

((Akasema: Hakika humo yumo Luutw. Wao wakasema: Sisi tunajua zaidi nani yumo humo. Hapana shaka tutamwokoa yeye na ahli zake, isipokuwa mkewe aliye miongoni mwa wataokaa nyuma. [Al-'Ankabuut: 31-32]

 هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ الْمُكْرَمِينَ ﴿24﴾ إِذْ دَخَلُوا عَلَيْهِ فَقَالُوا سَلَامًا قَالَ سَلَامٌ قَوْمٌ مُّنكَرُونَ ﴿25﴾ فَرَاغَ إِلَى أَهْلِهِ فَجَاء بِعِجْلٍ سَمِينٍ ﴿26﴾ فَقَرَّبَهُ إِلَيْهِمْ قَالَ أَلَا تَأْكُلُونَ ﴿27﴾ فَأَوْجَسَ مِنْهُمْ خِيفَةً قَالُوا لَا تَخَفْ وَبَشَّرُوهُ بِغُلَامٍ عَلِيمٍ ﴿28﴾ فَأَقْبَلَتِ امْرَأَتُهُ فِي صَرَّةٍ فَصَكَّتْ وَجْهَهَا وَقَالَتْ عَجُوزٌ عَقِيمٌ ﴿29﴾ قَالُوا كَذَلِكَ قَالَ رَبُّكِ إِنَّهُ هُوَ الْحَكِيمُ الْعَلِيمُ ﴿30﴾ قَالَ فَمَا خَطْبُكُمْ أَيُّهَا الْمُرْسَلُونَ ﴿31﴾ قَالُوا إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَى قَوْمٍ مُّجْرِمِينَ ﴿32﴾ لِنُرْسِلَ عَلَيْهِمْ حِجَارَةً مِّن طِينٍ ﴿33﴾ مُسَوَّمَةً عِندَ رَبِّكَ لِلْمُسْرِفِينَ ﴿34﴾

((Je! Imekufikia hadithi ya wageni wa Ibraahiym wanaohishimiwa?)) 

((Walipoingia kwake wakasema: Salama! Na yeye akasema: Salama! Nyinyi ni watu nisio kujueni)) 

((Akenda kwa ahali yake na akaja na ndama aliyenona)) 

((Akawakaribisha, akasema: Mbona hamli?)) 

((Akahisi kuwaogopa katika nafsi yake. Wakasema: Usiwe na khofu, nao wakambashiria kupata kijana mwenye ilimu.))

((Ndipo mkewe akawaelekea, na huku anasema na akijipiga usoni kwa mastaajabu, na kusema: Mimi ni kikongwe na tasa!)) 

((Wakasema: Ndivyo vivyo hivyo Alivyosema Mola wako. Hakika Yeye ni Mwenye Hiimah na Mwenye kujua)) 

((Akasema: Basi ujumbe wenu ni nini, enyi mliotumwa?)) 

((Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa watu wakosefu,)) 

((Tuwatupie mawe ya udongo)) 

((Yaliyotiwa alama kutoka kwa Mola wako kwa ajili ya wanaopindukia mipaka))

[Adh-Dhaariyaat: 24-34]

Malaika hao walikuwa wanakwenda katika mji wa Nabii Luut عليه السلام kuwaangamiza watu wake ambao walikuwa katika maasi. Baada ya hapo, na kutokana na kubashiriwa mtoto, Sarah akashika mimba na akamzaa Is-haaq عليه السلام.

Naye Is-haaq عليه السلام akamzaa Ya'aquub عليه السلامambaye amemzaa Yuusuf عليه السلام pamoja na ndugu zake wengine  kumi na mojo. Mmoja wa ndugu yake Yuusuf عليه السلام akiitwa Binyaamiyn ndiye aliyekuwa ni ndugu yake khalisa (ndugu kwa baba na mama).    Ibraahiym عليه السلام amefariki katika umri wa miaka mia na sabini na tano. [Qwisasul-Anbiyaa- Ibnu Kathiyr] na amezikwa Falastina katika mji ulioitwa Khaliyl.

Na Allaah Anajua zaidi.


MWISHO WA KISA CHA NABII IBRAHIYM عليه السلام


Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA YA NABII SULEIMAAN

The Story of Prophet Dhul Kifl

Full Story of the Prophet Ayyub