KISA CHA NABII HUD
KISA CHA NABII HUD A.S
Jina lake, Ibn Jarir anaeleza kuwa jina lake kamili ni : Hud Ibn Shaalih Ibn Arfakhshadh Ibn Sam Ibn Nuuh (Alayhis salaam).
Zipo kauli zinazosema Nabii Huud (Alayhis salaam) ndie mtu wa kwanza kuzungumza kiarabu. Japo zipo kauli nyengine zinasema ni Nabii Nuuh (Alayhis salaam) na nyengine ni Nabii Adam (Alayhi ssalaam).
Aad
Nabii Huud (Alayhis salaam) aliletwa kwa watu wa Aad, kama anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'allah); Na kwa A’adi tulimpeleka ndugu yao, Hud.” [Suratul Al-Aaraf aya ya 65] Ibn Is-haq ameeleza kuwa kabila la Nabii Huud lilitokana na Aad Ibn Iram Ibn ‘Awas Ibn Sam Ibn Nuuh.
Watu wa Aad waliishi katika milima baina ya Yemen (Hadharamuut) na Oman katika sehemu inayoitwa Ahqaaf. Allaah (Subhaanahu wa Ta'allah) aliwajaalia nguvu pamoja mali nyingi kwa lengo wazitumie katika kumshukuru ila wao walikuwa wakizitumia neema hizo katika kufanya ufisadi. Watu hawa walikuwa na uwezo wa kujenga majumba marefu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'allah) : “Wa Iram, wenye majumba marefu? (7) Ambao haukuumbwa mfano wake katika nchi?(8)” Suratul Fajr. Katika kuitafsiri aya ya 8 ya Suratul Fajr Qatadah na Ibn Jarir wao wameirejesha dhamiri kwenye kabila ya Aad, maana haukuumbwa mfano wa kabila hilo katika miji maana katika zama zao. Na hii ndio kauli iliyo ya sawa [Tafsir ya Ibn Kathyr].
Na Allaah aliwajaalia neema kubwa ya kuweza kupanda mazao na kunawiri kwa uzuri. Neema hizi zote ziliwafanya wajione wao ndio wao na hakuna wa kuwashughulisha katika ulimwengu huu.
Daawa ya Nabii Huud Kwa Watu wa ‘Aad
Baada ya watu wa Aad kufanya ufisadi mkubwa ndani ya ardhi, Allaah (Subhaanahu Wa Ta'allah) alimpeleka Nabii Huud ili aende akawalinganie juu ya kuacha ibada za masanamu na wamuabudie Allaah (Subhaanahu wa Ta'allah) pekee. Anasema Allaah (Subhaanahu Wa Ta'llah): “Na kwa A’adi tulimpeleka ndugu yao, Hud. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Allaah. Nyinyi hamna mungu ila Yeye. Basi je, hamumchi?” [Suratul Al-Aaraf aya ya 65]
Na anasema tena Allaah (Subhaanahu Wa Ta'allah) ndani ya Suratu Huud: “Na kwa kina A’adi tulimtuma ndugu yao Hud. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Allaah! Nyinyi hamna mungu isipo kuwa Yeye. Nyinyi si chochote ila ni wazushi tu. (50) Enyi watu wangu! Sikuombeni ujira kwa ajili ya haya. Haukuwa ujira wangu ila kwa Yule aliye niumba. Basi hamtumii akili?. (51) Na enyi watu wangu! Muombeni msamaha Mola wenu Mlezi, kisha mtubie kwake. Atakuleteeni mbingu zenye kunyesha mvua ya kumiminika, na atakuzidishieni nguvu juu ya nguvu zenu. Wala msigeuke mkawa wakosefu. (52)”
Pia Allaah (Subhaanahu Wa Ta'allah) anasema tena ndani ya Suratu As-Shuaraa: “Alipo waambia ndugu yao, Hud: Je! Hamchimngu? (124) Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu (125) Basi mcheni Allaah, na nit’iini mimi. (126) Wala sikutakeni juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote (127).”
Ama katika aya zilizofuata ndani ya Suratu Shuaraa akaanza kuwakumbushia juu ya neema walizopewa na Allaah (Subhaanahu Wa Ta'allah) ili nyoyo zao zipate kuzinduka na zijue kuwa yupo aliewaumba ambae anastahiki kuabudiwa. Na waache ibada yao ya kuabudu masanamu. “Je Mnajenga juu ya kila mnyanyuko kumbusho la kufanyia upuuzi? (128) Na mnajenga majengo ya fakhari kama kwamba mtaishi milele! (129) Na mnapo tumia nguvu mnatumia nguvu kwa ujabari. (130) Basi mcheni Allaah, na nit’iini. (131) Na mcheni aliye kupeni haya mnayo yajua (132) Amekupeni wanyama wa kufuga na wana. (133) Na mabustani na chemchem. (134) Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Kubwa. (135).”
Na anasema Allaah (Subhaanahu Wa Ta'allah) ndani ya Suratul Ahqaaf: “Na mtaje ndugu wa kina A’di, alipo waonya watu wake kwenye vilima vya mchanga. Na kwa yakini waonyaji wengi walitokea kabla yake na baada yake kuwaambia: Msimuabudu isipo kuwa Allaah. Hakika mimi nakukhofieni isikupateni adhabu ya siku iliyo kuu.” (21)”
Majibizano baina ya Watu wa ‘Aad na Nabii Huud
Baada ya watu wa Aad kulinganiwa juu ya suala la kumcha Allaah (Subhaanahu Wa Ta'allah) wakaanza kumjibu Nabii Huud (Alayhis salaam). Anasema Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala): “Wakasema: Ewe Hud!Hujatuletea dalili wazi. Wala sisi hatuiachi miungu yetu kwa kufuata kauli yako. Na wala sisi hatukuamini wewe. (53) Sisi tunasema: Baadhi katika miungu yetu imekusibu kwa baa (54)” [Suratul Huud].
Nae Nabii Huud akawajibu kwa kuwaambia: “Akasema: Hakika mimi namshuhudisha Allaah, na nyinyi shuhudieni, ya kwamba mimi najitenga mbali na hao mnao wafanya washirika (54) Mkamwacha Yeye. Basi nyote nyinyi nipangieni vitimbi, na kisha msinipe muhula! (55) Hakika mimi nimemtegemea Allaah, Mola Mlezi wangu na Mola Mlezi wenu. Hapana kiumbe yeyote ila Yeye anamwendesha atakavyo. Hakika Mola wangu Mlezi yuko juu ya Njia Iliyo Nyooka.(56)” [Suratul Huud].
Ama katika Suratul Ash-Shuaraa majibu ya watu ‘Aad yalikuwa: “Wakasema: Ni mamoja kwetu, ukitupa mawaidha au hukuwa miongoni mwa watoao mawaidha (136) Haya si chochote ila ni mtindo wa watu wa tokea zamani (137) Wala sisi hatutaadhibiwa (138)” Ama ndani ya Suratul Ahqaaf, anasema Allaah (Subhaanahu Wa Ta'allah) “Wakasema: Je! Umetujia ili ututenge mbali na miungu yetu? Basi tuletee hayo unayo tuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.(22)” Nae Nabii Huud (Alayhis salaam) akawajibu “Akasema: Hakika ujuzi uko kwa Allaah. Mimi nakufikishieni niliyo tumwa. Lakini nakuoneni kuwa nyinyi mnafanya ujinga. (23)”
Mazungumzo baina ya Nabii Huud (Alayhis salaam) na Makafiri
Katika kitabu cha “Visa Vya Mitume” Ibn Kathyr anatuelezea mazungumzo haya yalivyokuwa:
Wakubwa wa kikafiri walimuendea Nabii Huud (Alayhis salaam) wakamwambia: “Ni ajabu kubwa mungu kutuletea mtu miongoni mwetu aje atuonye” Nabii Huud (Alayhi ssalaam) akawajibu “Mnaona ajabu kukufikieni mawaidha yanayo toka kwa Mola wenu Mlezi kwa mtu aliye mmoja wenu nyinyi ili akuonyeni? Na kumbukeni alivyo kufanyeni mshike pahala pa kaumu ya Nuhu, na akakuzidisheni katika umbo. Basi zikumbukeni neema za Allaah ili mpate kufanikiwa.” [Suratul Al-Aaraf aya ya 69].
Wale wakubwa wakikafiri wakamwambia “Nani huyo anaeweza kutuangamiza??” Nabii Huud (Alayhis salaam) akawajibu: “Allaah” Miongoni mwao wakajibu “Miungu yetu itatulinda” Hawa ni wale miungu wa kisanamu waliokuwa wakiiabudu. Nabii Huud (Alayhis salaam) akawaambia “Allaah pekee ndie anaestahiki kuabudiwa na yeye ndie anaeweza kuangamiza na anaeweza kuwaokoa watu kutokana na adhabu zake, na hakuna nguvu nyengine katika dunia inayoweza kunufaisha au kuleta madhara”
Majibizano baina ya watu wa Aad na Nabii Huud (Alayhis salaam) yaliendelea kwa miaka huku wakiendelea kumtukana na kumkataa kuwa si Mtume. Na walizidi kuwa na kiburi katika ardhi pamoja na kumfanyia istihzai Nabii Huud (Alayhis salaam).
Kuadhibiwa kwa Watu wa ‘Aad
Allaah (Subhaanahu Wa Ta'allah) alianza kuwaadhibu watu hawa kwa kutowapelekea mvua ambayo ilipelekea mazao yao kuwa ya rangi manjano na baadae kupelekea kukauka. Kundi la watu wakamfuata Nabii Huud na kumuuliza juu ya hali ile. Na yeye akawajibu Allah amekasirika na nyinyi. Ikiwa mtamuamini basi atakupokeeni na atakuleteeni mvua. Wale watu wakaondoka kwa Nabii Huud wakimcheka kwa maneno aliyoyasema na wala hawakuamini kile walichoambiwa.
Siku katika masiku wingu zuri lilitanda juu yao. Hivyo wote walitoka nje wakitaraji kunyesha kwa mvua. Ila ghafla hali ya hewa ikabdilika kutoka jua kali na kuanza kwa baridi kali na upepo. Upepo ulizidi kidogo kidogo na ikawa ndio sababu ya kuangamizwa kwao. Allaah (Subhaanahu Wa Ta'allah) anatuelezea: “Basi walipo liona wingu likielekea kwenye mabonde yao, walisema: Wingu hili la kutunyeshea mvua! Kumbe sivyo, haya ni hayo mliyo yahimiza, upepo ambao ndani yake imo adhabu chungu (24) Unaangamiza kila kitu kwa amri ya Mola wake Mlezi. Wakawa hawaonekani ila nyumba zao tu. Hivyo ndivyo tuwalipavyo wakosefu! (25)” [Suuratul Ahqaaf]
Kina A’di walikanusha. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu? (18) Hakika Sisi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku korofi mfululizo (19) Ukiwang’oa watu kama vigogo vya mitende vilio ng’olewa. (20)” [Suratul Al-Qamar]
“Na ama A’di waliangamizwa kwa upepo mkali usio zuilika. (6) Alio wapelekea masiku saba, na siku nane, mfululizo bila ya kusita. Utaona watu wamepinduka kama kwamba ni magongo ya mitende yalio wazi ndani. (7)” [Suratul Al-Haaqah]
Na hivi ndivyo walivyoangamizwa watu wa Aad. Ama wale wema waliomuamini Nabii Huud (Alayhis salaam) wao hawakuadhibiwa. Anasema Allaah (Subhaanahu wataala) _*“Ilipo fika amri yetu, tulimwokoa Hud na walio amini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu. Na tukawaokoa na adhabu ngumu.” [Suratu Huud aya ya 57]
Na huu ndio mwisho wa kisa cha Nabii Huud (Alayhis salam). Tunamuomba Allaah (Subhaanahu Wa Ta'allah) atujaalie mazingatio kutokana na kisa hichi. Aamiyn.
“Kwa hakika katika visa vyao yamo mazingatio kwa wenye akili. Si maneno yaliyo zuliwa, bali ni ya kusadikisha yaliyo kabla yake, na ufafanuzi wa kila kitu, na ni uwongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini.” [Yuusuf aya ya 111].
Comments
Post a Comment