HISTORIA YA NABII ISMAIL(A.S)

 HISTORIA YA NABII ISMAIL(A.S)


KUZALIWA KWAKE

Ismail(a.s) ni mtoto wa kwanza wa Mtume Ibrahim(a.s.). Alizaliwa wakati uzee umekwishamfikia Ibrahim(a.s). Kama Qur’an inavyobainisha, katika umri huo wa uzeeni, MtumeIbrahiim(a.s) alimuomba Mola wake ampe mtoto mwema atakaendeleza harakati za Kiislamu.

“Ee Mola wangu! Nipe (mtoto awe) miongoni mwa watenda mema.” Ndipo tukampa habari njema ya (kuwa atapata) mtoto mpole. (Basi akapata. Naye ndiye Nabii Ismail).” (37:100-101).

MAMA YAKE

Historia ya mama yake Nabii Ismail inaanzia pale Nabii Ibrahim alipokwenda kutembelea nchi ya Misri akiwa amefuatana na mkewe, basi Firauni mfalme wa Misri aliwapokea na kuwaweka ndani ya qasri yake, na usiku ulipoingia Firauni alijaribu kumdhuru Bibi Sarah mke wa Nabii Ibrahim lakini Allaah Alimkinga na shari hiyo kwa kuufanya mkono wa mfalme upooze kila anapojaribu kumsogelea.

Alipoona dalili za qudra ya Allaah inayomlinda Bibi huyo, Firauni aliacha vitimbi vyake, na badala yake akaamua kumpa Sarah zawadi, na zawadi yenyewe ilikuwa binti yake aitwae Haajar, na Sarah akaikubali zawadi hiyo na akamuozesha binti huyo mumewe Ibrahim

Basi Ibrahim akarudi kwao akiwa amefuatana na wake zake wawili, Bibi Sarah na Bibi Haajar, na kutokana na mke mpya Allaah Akamruzuku mtoto wa kiume waliyempa jina la Ismail, jambo lililomfanya Bibi Sarah awe na wivu mkubwa juu ya mke mwenzake.

MASIMULIZI MENGINE

 ALIVYOMPATA HAAJAR

Akaelekea Misri   na wakati wote alipokuwa safarini  ilikuwa hima yake ni kuwaita watu katika Tawhiyd, kuwaongoza katika haki na katika mambo mema. Alipokuwa anaelekea Misri alipita mji wa dhalimu mmoja akapiga kambi hapo. Matukio yote hapo yameelezwa katika Hadiyth Sahiyh ifuatayo:

Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema:  Ibraahiym عليه السلام hakuongopa ila mara tatu tu; mara mbili kwa ajili ya Allaah aliposema, ((Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao)) na aliposema, ((Hakika mimi ni mgonjwa!)). Na alipokuwa akisafiri katika mji wa dhalimu mmoja na Sarah alikuwa naye. Alipopiga kambi, mtu mmoja alikwenda kwa dhalimu na kumwambia, "Kuna mtu amepiga kambi katika ardhi yako na anaye mwanamke mzuri kupita wote". Dhalimu akamuita Ibraahiym عليه السلام kwake, na akamuuliza, "Nini uhusiano wa mwanamke huyu na wewe?". Akasema, "Yeye ni dada yangu". Dhalimu akasema, "Nenda kamlete kwangu". Ibraahiym عليه السلام akaenda kwa Sarah na akasema, "Dhalimu huyu ameniuliza kuhusu wewe, na nimemwambia kwamba wewe ni dada yangu, kwa hiyo usimfanye akajua kwamba nimeongopa, kwani hakika ni dada yangu kufuatana na kitabu cha Allaah, na hakuna Waislamu katika ardhi hii ila mimi na wewe". Ibraahiym عليه السلام akampeleka (Sarah) kwake, kisha akasimama na kuswali. Alipoingia kwa dhalimu na (dhalimu) alipomuona (Sarah), akataka kumshika kwa matamanio, lakini akagandishiwa (mkono) Akasema, "Niombee kwa Allaah na sitokudhuru". Sarah akamuombea, na akaachiliwa. Kisha akamfikia kwa matamanio,  lakini akapatwa tena (kuganda mkono) kama mwanzo au zaidi. Ikaendelea hivyo mara tatu, na kila mara alisema kama alivyosema mara ya mwanzo. Kisha akamwita mlinzi wake wa karibu naye kabisa na akasema, "Hukuniletea binaadamu bali umenilitea shaytwaan! Muondoshe na mpe Haajar". Akaondoshwa (Sarah) na kupewa Haajar, akarudi. Ibraahiym عليه السلام alipotambua kuwa (Sarah) amerudi, alimaliza kuswali na kugeuka akasema, "Imekuwaje?". Akasema, "Allaah Ametosheleza njama za kafiri dhalimu, na amenipa Haajar kama mtumwa")) [Al Bukhaariy na Muslim].

Muhammad bin Siriyn amesema, "Abu Huraryah amesimulia Hadiyth hii  na akasema: "Huyu ni mama yenu enyi wana wa maji ya mbinguni" (yaani Waarabu kizazi cha Ismaa'iyl عليه السلام, mwana wa Haajar ambaye ndiye aliyesababisha maji ya Zamzam). [Fat-h Al-Baariy 6:447, Muslim 4:1840]

Mke wa Ibraahiym عليه السلام Sarah, alikuwa tasa. Na Ibraahiym عليه السلام alikuwa anazeeka na nywele zake zikatawaliwa na mvi baada ya kuita watu miaka mingi katika dini ya Allaah. Sarah akafikiria kwamba yeye na Ibraahiym عليه السلام wako katika upweke kwa vile hawakupata mtoto. Kwa hiyo akampa mumewe mtumwa wake Haajar amuoe.  Haajar akamzaa Ismaa'iyl  عليه السلام ambaye ndiye mtoto wa mwanzo wa Ibraahiym عليه السلام.

WIVU WA BI SARA KWA BI HAAJAR NA MWANAWE ISMAIL

 Siku zikapita na Ibraahiym عليه السلام akawa na furaha ya kupata mtoto, lakini Sarah akawa na wivu sasa na Haajar, ingawa yeye mwenyewe ndiye aliyempa Ibraahiym عليه السلام Haajar amuoe. Wivu huo ukamfanya Haajar awe anajificha ili Sarah asimuone anapokwenda kwa mumewe. Akawa ni mwanamke wa kwanza kufunga mkanda kuficha alama zake kama ilivyotajwa katika Hadiyth ndefu kutoka kwa  Al-Bukhaariy iliyopokelewa na Ibn 'Abbaas kwamba "Haajar ni mwanamke wa mwanzo kutumia mkanda".

Makusudio hapo ni mkanda kiunoni kuzuia nguo yake ndefu inayoburuza ardhini isiache alama apitapo (ikaja ikajulikana na Sarah kuwa kapita). Inasemekana kuwa wakati huo wanawake walikuwa wakivaa nguo ndefu zinazoburuza. Na hii inaonyesha jinsi stara ilivyokuwa kwa wanawake tangu wakati huo.

Pia katika masimulizi kwenye Sahiyh Al Bukhaariy anasema, ''Wakati Nabii Ibraahiym عليه السلام alipomuoa Haajar na akamzalia Ismaa'iyl عليه السلام, mkewe wa mwanzo, Sarah, akapata wivu na akaapa kuwa atamkata mwili wake vipande vitatu, hivyo Haajar akajifunga mkanda kiunoni mwake na kukimbia huku akiburuza vazi lake nyuma yake ili kufuta alama za nyayo zake ili Sarah asiweze kujua alipoelekea. (Al Bukhaariy - Kitabu cha Visa Vya Mitume, hadiyth namba 3364)

KUHAMA HAJAR NA MWANAWE ISMAIL MAKKA NA KUPATIKANA KISIMA CHA ZAMZAM

KUHAMIA MAKKA

Nabii Ibrahim akamchukua kwenda nae Makka Haajar pamoja na mwanawe Ismail na kufunga nao safari ndefu kutoka Palastina hadi nchi ya Hijaazi (Saudia hivi sasa)

Alipowasili mji wa Makkah penye bonde baina ya Swafa na Marwa mahali kilipo kisima cha maji ya zamzam hivi sasa, na wakati huo hapakuwa na mtu yeyote anayeishi hapo, na nyumba ya Allaah (Al-Ka’abah) ilikuwa mfano wa mnyanyuko tu uliokuwa ukishambuliwa na upepo mkali pamoja na mikondo ya maji ya mvua iliyokuwa ikizikwanguwa pembe nne za nyumba hiyo.

Hapakuwa na mtu anayeishi mahali hapo wala nyumba wala maji isipokuwa mti mmoja tu ambao chini yake aliwaacha mkewe na mwanawe. Aliwawekea birika la maji pamoja na chombo alichowatilia tende ndani yake, kisha akageuka na kuianza safari ndefu ya kurudi Palastina.

Bibi Haajar mama yake Ismail alipomuona mumewe akirudi na kuwaacha mahali hapo walipopafikia baada ya safari ndefu iliyowachukua siku nyingi njiani, mahali pasipo na mji wala kijiji, wala hata dalili ya mtu karibu na hapo, akamfuata mumewe na kumuuliza:

“Unatuachia nani mahali hapa pasipo na mtu yeyote?”

Alimuuliza hivyo mara nyingi lakini Nabii Ibrahim hakumjibu, na alipomuuliza:

“Allaah ndiye aliyekuamrisha?”

Nabii Ibrahim akajibu:

“Naam, ndiyo.”

Kwa imani iliyothibiti, na kwa utiifu mkubwa na moyo uliosalimu amri mbele ya maamrisho ya Allaah, Bibi Haajar akamwambia:

“Kwa hivyo Hatotupoteza”.

Kisha Nabii Ibrahim akageuka na kuianza safari ndefu ya kurudi Palastina akiwaacha nyuma mkewe na mwanawe wa mwanzo na wa pekee wakati ule, na baada ya kutembea muda kidogo, akasimama mahali ambapo mkewe hakuweza kumuona, kisha aligeuka nyuma na kuomba dua ifuatayo:

رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُواْ الصَّلاَةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ

“Mola wetu! Hakika mimi nimewaweka (nimewakalisha baadhi ya kizazi changu (mwanangu Ismaa’iyli na mama yake Haajar) katika bonde (hili la Makkah) lisilokuwa na mimea yoyote; katika nyumba yako takatifu (ya Al-Ka’abah utakayotwambia tuijenge).

Mola wetu! Wajaalie wasimamishe Swala. Na ujaalie nyoyo za watu zieleke kwao (wapende kuja kukaa hapa ili pawe mji) na uwaruzuku matunda ili wapate kushukuru.”

Nabii Ibrahim alikuwa mara kwa mara akija Makkah kuwazuru mkewe na mwanawe, na hapana anayejua uhakika wa idadi ya ziara hizo, isipokuwa wanahistoria wameelezea juu ya ziara nne maarufu.

Ya mwanzo ni pale alipooteshwa kumchinja mwanawe wa pekee Ismail  ndani ya ndoto (na ndoto za Mitume ni wahyi), 

Ya pili ni ziara ya Ibrahim kwa mke wa mwanaye Ismail 

Ya tatu ni ujenzi wa Al kaaba 

KUPATIKANA KISIMA CHA ZAMZAM

Baada ya Nabi Ibrahim kuondoka na kumuacha Bibi Haajar chini ya mtu ule, akawa anakula tende na kumnyonyesha mwanawe Ismail, na haukupita muda mrefu maji yakaanza kupungua na hatimaye yakamalizika, na baada ya kumuona mwanawe akiteseka kwa kiu, akaanza kuhangaika huku na kule kutafuta maji. Akaliendea jabali lililokuwa karibu yake ‘Jabal Swafaa’, akalipanda na kutazama huku na kule asione kitu.

Kisha akateremka na kutembea penye bonde baina ya Swafa na Marwa. Akawa anatembea taratibu, na alipofika katikati ya bonde akaanza kukimbia kidogo kidogo huku akiliendea jabali lililokabiliana nalo ‘Jabal Marwa’, akalipanda na kutazama huku na kule, na huko pia hakuona kitu.

Anasema Ibn ‘Abbaas Allaah amridhie kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hiyo ndiyo Sa'ayi mnayotembea baina ya Swafaa na Marwa.

Aliendelea kufanya hivyo mara saba, na alipokuwa akiliendea jabali Marwa alisikia sauti ngeni ikimsemesha, akasimama kimya apate kuiskia vizuri huku akitazama mahali alipo mwanawe, akamuona Malaika amesimama (mahali kilipo kisima cha Zamzam hivi sasa) huku akichimba kwa ubawa wake mpaka maji yalipopanda, na hapo ndipo mama yake Ismail alipoyaendea na kuanza kuyazuia kwa mikono yake huku akiyachota.

Imepokelewa kuwa Ibn ‘Abbaas Allaah amridhie amesema kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Allaah amrehemu mama yake Ismail, lau angeyaacha maji ya zamzam yaendelee basi yangegeuka kuwa chemchem.”

Mama yake Ismail akaanza kumnywesha mwanawe maji hayo na yeye mwenyewe akawa anakunywa, na Malaika akamwambia:

“Usiogope hutopotea, kwani hapa ndipo ilipo nyumba ya Allaah itakayojengwa na mtoto huyu pamoja na baba yake.”

MAISHA YA BI HAJAR NA MWANAWE ISMAIL KATIKA BONDE LA MAKKA

Haajar na Ismail waliendelea kuishi hapo peke yao muda mrefu mpaka ulipopita msafara wa watu wa kabila la Jurhum uliopiga kambi sehemu ya chini ya mji wa Makkah, mbali na alipo mama yake Ismail

Watu wa Jurhum walipomuona ndege akiruka sehemu ya mbali, mahali alipo mama yake Ismail wakasema: “Bila shaka ndege yule kule alipo ameona maji”, na kwa vile inajulikana kuwa sehemu zile si kawaida kupatikana maji, Jurhum waliamua kutuma mtumishi mmoja au wawili wakachunguze sehemu aliyoonekana ndege yule, watumishi wakakiona kisima cha maji ya Zamzam, na wakarudi kuwajulisha watu wao walioamua kuelekea huko haraka sana, na walipomuona mama yake Ismaa’iyl yuko pale wakamuomba wakae naye mahali hapo wakamwambia:

“Utaturuhusu tukae pamoja na wewe mahali hapa?”

Mama yake Ismail akawaambia:

“Nitakuruhusuni, lakini maji haya ni yangu.”

Wakasema:

“Tumekubali.”

Anasema Ibn ‘Abbaas Allaah amridhie kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Jambo hilo lilimfurahisha sana mama yake Ismaili kwa sababu alikuwa mwenye kupenda watu.

Kuinua Kuta za Ka’bah.

Kama tulivyoona katika maisha ya Mtume Ibrahim(a.s.), Nabii Ismail (a.s.) alishirikiana na baba yake kuinua kuta za Ka’abah ambayo ndiyo nyumba kongwe ya kufanyia Ibada na kituo kikuu cha kwanza cha harakati za Kiislamu duniani.“...........Na tulimwusia Ibrahim na Ismail (tukawaambia): Itakaseni nyumba yangu kwa ajili ya wale wanaoyoizunguka kwa ajili ya kutufu na wanaokaa hapo na (kwa ajili ya) wanaorukuu na kusujudu hapo pia” (2:125).

Na (kumbukeni khabari hii) Ibrahim alipoinua kuta za nyumba (hii ya Al-Ka’bah) na Ismail (pia) (wakaomba, wakasema): “Ee Mola wetu! Tutakabalie (amali yetu hii ya kujenga huu msikiti). Hakika wewe ndiwe Mwenye kusikia, na Mwenye kujua”. (2:127).

Ismail(a.s) na Taifa la Waarabu

Nabii Ismail(a.s) ndiye chimhuko la kabila la Quraysh. Baada ya kuachwa katika bonde la Makka lililokavu, Allah(s.w) alijaalia kupatikana maji na hatimaye watu kuhamia pale. Uhai wa mji ukaanza na kutokana na kizazi cha Ismail(a.s) wakapatikana Waarabu wa Hijaz (Saudi Arabia) ambao hufahamika kwa jina mashuhuri Banu Quraysh. Qur’an imemtaja Ismail(a.s) kuwa alikuwa Mtume mkweli wa ahadi aliyewausia watu wake swala na zakat. “Na mtaje katika kitabu (hiki) Ismail. Bila shaka yeye alikuwa mkweli wa ahadi, na alikuwa Mtume, Nabii. Na alikuwa akiwaamrisha watu wake Sala na Zakat na alikuwa mridhiwa mbele ya Mola wake”. (19:54-55).

Qur’an hapa haimtaji Ismail kwa wema kwa vile alikuwa mtoto wa Mtume Ibrahim(a.s.), bali kwa vile alikuwa mtumishi wa Allah aliye mkweli, muamrisha mema na mkataza maovu. Nasaba hapa haikutajwa kabisa.

Baada ya MtumeIbrahiim(a.s) na mwanae Ismail kujenga upya Ka’bah na kutangaza Hija, walimwomba Allah(s.w) alete Mtume atokanaye na kizazi chao ambaye ataendeleza harakati za Kiislamu kama walivyofanya wao. Aidha walikiombea kizazi chao kiwe ni cha watu wanyenyekevu: “Ee, Mola wetu! Utufanye tuwe wanyenyekevu kwako. Na miongoni mwa kizazi chetu (pia ufanye) umma mnyenyekevu kwako. na utuonyeshe njia ya Ibada yetu na utusamehe. Bila shaka Wewe ndiye Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.(2:128)

“Ee, Mola wetu! Waletee Mtume anayetokana na wao, awasomee Aya zako, na kuwafundisha kitabu (chako) na hikma na awafundishe kujitakasa (na kila mabaya). Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima” (2:129).

Dua hii ilikuwa kabuili. Ilipofika zama za kuletwa Mtume wa mwisho, Allah(s.w.) akamleta kupitia kizazi cha Bani Quraysh ambao wanatokana na Ismail(a.s). Ndiye Mtume wetu Muhammad (s.a.w.).

Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Nabii Ismail(a.s)

Kutokana na Historia ya Nabii Ismail(a.r) tunajifunza yafuatayo:

(i) Kila Muislamu anatakiwa kumuomba Allah(s.w) amruzuku mtoto mwema atakayesaidia kupeleka mbele harakati za kuhuisha na kusimamisha Uislamu katika jamii.

(ii) Mtoto mwema anayependwa na Allah(s.w) ni yule anayewatii wazazi wake katika mambo ya kheri.

(iii) Mtoto mwema hujitahidi kushiriki katika harakati za kuusimamisha Uislamu katika jamii.

(iv) Amri ya pili ya Allah(s.w) inayotukabili baada ya ile ya kusoma(kutafuta elimu) ni kusimamisha swala na kutoa katika vile Allah(s.w) alivyoturuzuku, kisha kuamrisha familia zetu na jamaa zetu wa karibu kufanya hivyo kisha tuilinganie jamii nzima kufanya hivyo.

(v) Kusema kweli na kutekeleza ahadi ni katika tabia njema anayoiridhia Allah(s.w).

(vi) Inatupasa kumuomba Allah(s.w) atupe yaliyo mema katika kila jambo tunalolikusudia kufanya.

(vii) Kuwa tayari kutoa nafsi zetu kwa ajili ya Allah(s.w)kama alivyokuwa tayari Ismail(a.s) kuchinjwa na baba yake katika kutekeleza amri ya Allah(s.w)

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA YA NABII SULEIMAAN

The Story of Prophet Dhul Kifl

Full Story of the Prophet Ayyub