HISTORIA YA NABII IDRISS

 HISTORIA YA NABII IDRIS

Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’an:“ Na mtaje Idris katika Kitabu (hiki).  Bila shaka yeye alikuwa mkweli sana (na) Nabii. Na Tulimuinua daraja ya juu kabisa.” (19:56-57)

Katika vitabu sahihi, imesimuliwa kutoka kwa Wahab kwamba Idris alikuwa mtu aliyejengeka kimwili akiwa na kifua kipana.  Alikuwa na vinyweleo vichache mwilini na nywele nyingi kichwani. Alikuwa na sauti ya chini pale alipozungumza. Alipokuwa akitembea, miguu yake ilikaribia kukutana.  Ameitwa Idrisa kwa sababu alikuwa na kawaida ya kufundisha ukarimu wa Mwenyezi Mungu na ubora wa Uislamu.

Idrisa alikuwa akiutafakari Utukufu na Ukubwa wa Mwenyezi Mungu kwamba anga, ardhi, jua, mwezi, nyota na mawingu na viumbe vyote vina Muumba ambaye, kwa Uweza Wake, kaviumba na kuvipa maumbo na kuvipangilia.

Ana hatia yule asiyemwabudu Yule Mwenye Haki ya kuabudiwa. Kwa kuzingatia hilo, alifanya mikutano ya faragha na watu wa jamii yake na kuwanasihi, mkumbukeni Mwenyezi Mungu.

Pia aliwahadharisha juu ya adhabu Yake. Aliwalingania watu kuielekea ibada ya Mola wao. Kutokana na ulingano huo, watu wakaanza kuungana naye.

Kwanza walikuwa watu saba, halafu wakafika sabini, kisha mia saba, na kisha watu elfu moja wakawa wafuasi wake. Halafu Idrisa akawaambia, “tuwachague watu mia moja wachaMungu.”

Basi, katika watu elfu moja, sabini wakachaguliwa, kisha katika hao sabini, kumi wakachaguliwa, na katika hao kumi, hatimaye watu saba wakachaguliwa.halafu akasema, “njooni, hebu sisi watu saba tuombe dua na wengine waitikie Amiin. Huenda Mola wetu Akatuongoza kutokana na dua zetu. Waliweka mikono yao chini, na kuomba, lakini hakuna kilichotokea. Wakanyoosha mikono yao mbinguni na kuomba. Mwenyezi Mungu akamshushia wahyi Idris na kumchagua kuwa Mtume.Mwenyezi Mungu akamwongoza Yeye na maswahaba zake kuilekea ibada Yake. 

Kwa hiyo, wakashughulika kumwabudu Mwenyezi Mungu na hawakumshirikisha nayeyote yule kiasi ambacho Mwenyezi Mungu alimpandisha daraja Idris. Idris akapazwa mbinguni.

Ukiondoa watu wachache, wengi miongoni mwa wale waliokuwa wamemwamini Idris wakakengeuka na kukawa na mifarakano na khitilafu miongoni mwao, 

Nuhu akateuliwa kuwaongoza.Kwa mujibu wa Hadiyth kutoka kwa Abu-Dharr, imesimuliwa kuwa vitabu thelathini vilishushwa kwa Idris na Hadiyth nyingine zinasema kuwa Idris ndiye mtu wa kwanza kuandika kwa kalamu.  Pia alikuwa akijishonea nguo na kuzivaa. Alikuwa Fundiwa kushona nguo na alikuwa mwingi wa kumwabudu na kumtukuza Mwenyezi Mungu.

Imesimuliwa katika Hadiyth sahihi kwamba Msikiti wa Sahla (Masjid as-Sahla) ndio ulikuwa makazi ya Idrisa ambako ndiko alikokuwa akishona nguo na kumwabudu Mwenyezi Mungu. Zipo simulizi ndefu kuhusu Idris ambazo zinaweza kupimwa katika vyanzo sahihi ili kupata usahihi wake.  Moja inasema kuwa katika kipindi cha mwanzo cha Unabii wa Idris, alipata kuishi mfalme dhalimu.  Siku moja mfalme huyo alipita katika ardhi iliyostawi nyasi za kijani kibichi ambayo ilikuwa ni mali ya muumini mmoja mchaMungu.

Muumini huyu alikuwa ameachana na dini zote potofu na alichukizwa na watu waliokengeuka. Akajitenga nao mbali.  Mfalme alikipenda kipande kile cha ardhi, hivyo akamuuliza Waziri wake kuhusiana na mmiliki wa ardhi hiyo.Waziri akamjibu kuwa ardhi hiyo ilikuwa ni ya muumini fulani.  Mfalme akamwita muumini huyo na kumwambia kuwa yeye aliihitaji ardhi hiyo. Muumini akajibu kuwa familia yake iliihitaji zaidi ardhi hiyo kuliko mfalme. Mfalme akaomba basi amuuzie lakini muumini akagoma jambo ambalo lilimkasirisha mfalme mpaka uso wote ukambadilika. 

Akiwa katika hali hiyo, mfalme akarejea nyumbani.  Mfalme huyo alikuwa na mke kutoka Iraq (Barak) ambaye alimpenda sana na ambaye alishauriana naye mara kwa mara.Mfalme alipofika kwenye kasri lake, akamwita mkewe. Mkewe aliona jinsi mumewe alivyobadilika usoni na akamuuliza nini kulichomuudhi. Mfalme akamuhadithia mkewe habari ya ardhi ya muumini.Mkewe akamwambia ‘anayeishia kununa ni mnyonge ambaye hana uwezo wa kulipiza.  Kama hutaki kumuua au kumkata kichwa pasipo sababu basi mimi nitakupa maarifa ya kumuua (muumini huyo) ili ardhi iwe yako hata watu wa familia yake hawatakulalamikia kwa kifo chake.’ Mfalme akamuuliza mkewe maarifa gani aliyokuwa nayo kichwani. Mkewe akajibu kuwa kundi moja la jamaa zake kutoka Azarak ndilo litakalotumwa kwenda kumkamata (muumini huyo) na ni kundi hilo litakalotoa ushahidi kuwa muumini huyo ametoka katika dini ya mfalme.“

Kwa njia hii wewe sasa unaweza kumuhukumu kifo na kutwaa ardhi yake.” Mfalme akakubaliana na ushauri wa mkewe.  Basi kundi hilo likaitwa kutoka Iraq ambako lilikuwa likifuata dini ya Malkia na ambalo liliamini kuwa ni halali kumchinja muumini huyo. Watu wa kundi hilo wakatoa ushahidi mbele ya mfalme kuwa mtu huyo ametoka katika dini ya mfalme (ambayo ndiyo dini ya serikali). Kwa kisingizio hicho, mfalme akatoa amri ya kumuua muumini huyo na kunyang’anya ardhi yake.

Mwenyezi Mungu akayaghadhibikia mauaji hayo ya muumini, na Akampelekea wahyi Idris aende akamwambie mfalme huyo dhalimu, “je, hakutosheka kumuua muumini mpaka pia uchukue ardhi yake kuitia umasikini familia yake?

Naapa kwa Utukufu na Uweza Wangu kwamba Nitamlipizia kuuawa kwake.  Siku ya Kufufuliwa na papa hapa duniani.Nitautokomeza utawala wako. Nitaigeuza heshima na hadhi yako kuwa udhalili na fedheha. Mbwa watamla nyama mkeo.

 Je, subira Yangu ya kukutahamini wewe ndiyo imekufanya uwe jeuri?” Idris akamwambia mfalme,  “Ewe mfalme uliyetakabari! Mimi ni mtume wa Mwenyezi Mungu!” Hapo akamfikishia mfalme ule ujumbe wa Mwenyezi Mungu.  Mfalme akamwamuru Idris aondoke kwenye kasri lake na akamuonya kuwa hataweza kubaki salama.Mfalme akamuhadithia Mkewe mazungumzo yake na Idris.  Mkewe akasema, “usiogope unabii wa Idris. Mimi nitatuma mtu wa kwenda kumuua huyo Idris ili unabii wake ufutikie mbali.”

Mfalme akakubaliana na ushauri wa mkewe na kuidhinisha mpango wa kumuua Idris. Miongoni mwa jamaa zake Idris, walikuwemo wale waliokuwa wakitumikia Kasri la mfalme. Idris akawafahamisha wahyi uliomfikia na akawafahamisha kuwa kaufikisha kwa mfalme. Jamaa zake hao wakaingiwa na hofu kuwa Idris atauawa. 

Malkia wa Iraq akatuma watu arobaini kwenda kumuua Idris.Wauaji hao wakafika mahali ambapo Idris alikuwa akipenda kukaa na maswahaba zake lakini hola! Hawakumkuta. Basi wakarudi zao. Jamaa zake Idris walipowaona watu hao wakati wanakuja kumuua Idris wakatawanyika na baade wakakutana na Idris. Wakamfahamisha kuwa watu wapatao arobaini wanamvizia wamuue, hivyo aishi kwa tahadhari.

Idris akamuelekea Mola wake na kuomba dua hii:  Ewe! Mola Mlezi wangu! Umenituma kwa mtawala dhalimu kufikisha ujumbe Wako akanitishia na sasa anaiwinda damu yangu.

Mwenyezi Mungu akamteremshia wahyi Idris kuwa akae mbali na mfalme huyo. 

“Naapa kwa Utukufu wangu kwamba Nitaitimiza Sharia yangu kwake na kuithibitisha kauli yako na kuuthibitisha unabii wako kuwa ni wa kweli.”

Idris akasema, “

Ewe Mwenye kuniruzuku! Nina ombi.” Mwenyeezi Mungu akasema, “Niombe, Nitakutimizia.” Idris akasema, “ isinyeshe mvua hadi nitakapoomba tena.”

Mwenyeezi Mungu akasema, “ Nchi itaangamizwa na watu watakumbwa na njaa hadi kufa.”  Idris akasema, “Chochote kiwacho ndiyo ombi langu.” mwenyeezi Mungu akajibu,  Naam, Nalikubali, hadi pale wewe utakapoomba (vinginevyo),Mimi sitateremsha mvua, Nami ndiye Mwaminifu zaidi kwa ahadi.”

Kusikia hivyo, Idris akawafahamisha maswahaba zake kuhusu mazungumzo yake na Mwenyezi Mungu, na akasema, “Enyi jamaa zangu, hameni nchi hii na kwenda mahali pengine.”  Walikuwa ni watu ishirini, na wakatawanyika sehemu mbalimbali. Watu wakapata habari ya dua aliyoomba Idris. Yeye mwenyewe Idris akaenda kutafuta hifadhi mlimani. Mungu akamteua Malaika ambaye alikuwa akimpelekea chakula kila jioni. Idris alikuwa akifunga nyakati za mchana na akawa anafungua swaumu jioni pale Malaika alipomletea chakula. Mwenyezi Mungu akaangamiza utawala wa mfalme dhalimu. Mfalme huyo aliuliwa, ufalme ukafutika, na nyama ya mwili wa mkewe ikaliwa na mbwa kwa sababu ya dhuluma waliyomfanyia Yule muumini waliyemuua na kupora shamba lake. Mtawala mwingine dhalimu,,

Mtawala mwingine dhalimu akakalia kiti cha ufalme. Miaka ishirini ikapita bila mvua. Watu walitaabika sana kwa shida na dhiki na hali yao ikawa mbaya sana.  Wakawa wanafuata chakula katika nchi za mbali.Hali yao ilipozidi kuwa mbaya, wakajadiliana miongoni mwao kwamba janga hilo lilitokana na dua ya Idris ambaye alimuomba Mwenyezi Mungu kuwa mpaka yeye atakapoomba mvua inyeshe, hakutakuwa na mvua.“

Hatufahamu mahali alipo Idris kwa sababu amejificha sisi tusimuone.” Wakakata shauri kuwa kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye Mwingi wa rehema kuliko Idris basi watubie na kumuomba ili mvua inyeshe kwenye nchi yao na katika maeneo ya jirani. Basi wakavaa nguo duni-duni na wakajipaka matope vichwani na wakasimama wima ardhini wakilia na kutubu kwa Mungu. 

Mwenyezi Mungu akawahurumia na akamteremshia wahyi Idris kwamba, “watu wako wanatubu, wanalia kwelikweli na Mimi Ndiye Mungu wa kuwahurumia na kuwafadhili na Ndiye ninayepokea toba na kusamehe dhambi. Nawahurumia na Ninataka kuwatimizia maombi yao ya mvua. Mimi sina kikwazo isipokuwa wewe uliniomba nisilete mvua mpaka uombe (tena). Hivyo, Ewe Idris! Niombe ili niwateremshie mvua.”

Katika kisa hicho, tunaweza kupata mafunzo kuwa mwisho wa jeuri na dhuluma huwa mbaya. Unaweza kujidanganya kwa sababu ya muda mrefu unaoweza kupita baada ya wewe kufanya dhuluma lakini mwishowe matokeo huwa ni mabaya. Aidha, matokeo ya kumuasi Mwenyezi Mungu ni mabaya kwa jamii yoyote ile. Kinyume chake, kutomuasi Mwenyezi Mungu ndiko kunakoleta hikima na rehema kubwa na ndiyo njia ya kuiendea kheri ambayo huchangia kukufungulia mlango wa neema na mlango wa mafuhumu.

Kwani pale Mwenyezi Mungu anapokufanya walii Wake (rafiki Yake) hukujaalia akili na hikima.  Manabii na Mawalii wake waliongozwa na Roho mtakatifu (Ruhulquds).Mawalii ni watu ambao Mapazia ya dunia hii hufunguliwa na ukweli huwadhihirikia kiasi kwamba wanasalimika na ujahili na kufuata uwongofu na nasaha ambazo hugandamana na nafsi zao.

Aidha inasisitizwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi kwani Mwenyezi Mungu anapoona mnamkumbuka, huzipokea dua zenu na kukutimizieni mahitaji yenu, na hukumiminieni neema kutoka kwenye Hazina Yake ambayo kamwe haifilisiki. Tunajifunza katika funga ya Idris kuwa falsafa ya funga ni kujiepusha na maovu yote. Na tufunge kwa nia safi na ikhilasi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. 

Funga safi hutakatisha nyoyo zetu.Funga huuandaa moyo kuwa makazi ya nia nzuri. Mwenyezi Mungu huzitazama nyoyo zetu, hivyo ni vema ziwe safi. Na katika kisa cha Idris kufunga bila kujua atapata wapi futari, tunajifunza kuwa haifai kuacha kufunga kwa kisingizio cha kukosa futari. Kuna simulizi nyingine kuwa Idris aliishi duniani kwa miaka 300. Wengine wametaja kipindi kirefu zaidi.

Usahihi Ndani ya Qur’an 

Idris ni nabii wa kale aliyetajwa katika Qur’an. Qur’an inamuelezea kama mtu mkweli na mwenye subira, na pia inasema kuwa alinyanyuliwa katika daraja ya juu. Kwa sababu hiyo, na kwa sababu ya sifa zinazofanana, Idris ametambuliwa kama ndiye Enoch aliyetajwa katika Biblia. Mara zote, Simulizi za Waislamu zimemwelezea Idris kama mtu wa vizazi vya mwanzo vya Nabii Adam, na vinamuhesabu kama ni mmoja wa Manabii wakongwe waliotajwa katika Qur’an, akiwekwa katikati baina ya Adam na Nuhu.  Daraja ya aina yake aliyopata Idris ndiyo iliyochochea hadithi na visa vingi vinavyo muhusu katika Uislamu.

Kwa mujibu wa Hadith iliyosimuliwa na Malik ibn Anas iliyomo katika Sahih Muslim, inaelezwa kuwa katika Usiku wa Miraj, Mtume, swallallahu alayhi wa sallam,aliposafiri kwenda mbinguni, alikutana na Idris katika mbingu ya nne.

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA YA NABII SULEIMAAN

The Story of Prophet Dhul Kifl

Full Story of the Prophet Ayyub